SIMBA juzi usiku ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya katika tamasha la Simba Day, lakini kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids amefunguka kuhusu maandalizi ya kikosi kwa ajili ya msimu mpya akiweka bayana mfumo mpya anaokuja nao anaoamini utawatesa wapinzani.
Kocha huyo Msauzi anayeinoa Simba kwa msimu wa pili, juzi amesema msimu ujao atapenda zaidi kutumia mastraika wawili kwa mpigo katika kila mechi tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita alipokuwa akiwapishanisha kwa kupenda kuanza na mshambuliaji mmoja tu.
Kwa mara ya kwanza juzi mashabiki wa Simba walishuhudia washambuliaji watatu wa kati, Jonathan Sowah, Steven Mukwala na Seleman Mwalimu wakigawanywa dakika na kocha huyo, ikiwa ni siku chache tu kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga itakayopigwa Jumanne.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema; “Tulicheza kipindi cha kwanza vizuri kwa kutumia washambuliaji wawili. Hii ndiyo njia tunayotaka kwenda nayo msimu huu, kuwaweka washambuliaji wawili mbele. Tuna nguvu ya Mwalimu, Mukwala, Sowah na bila kusahau Kibu ambaye pia anaweza kucheza kama namba tisa. Ukiwa na wachezaji wa aina hiyo lazima uwatumie vizuri.”
Hata hivyo, Fadlu hakusita kueleza upungufu aliouona.
“Tunapaswa kufanya kazi zaidi kwenye muundo wa kushambulia kwa presha, nafasi tunapokuwa tunajilinda bila ya kuwa na mpira. Tulianza na wachezaji wapya watano, ilikuwa changamoto kuona namna walivyobeba presha ya mashabiki 60,000. Lakini nimefurahishwa na uchezaji binafsi, ingawa kushinda mechi kubwa kunahitaji kiwango kizuri cha timu kwa jumla,” alisema Fadlu.
Wachezaji wapya alioanza nao ni beki wa kati, Rushine De Reuck, beki wa kushoto Anthony Mligo, viungo mkabaji na mshambuliaji Naby Camara na Neo Maema na mshambuliaji wa kati Jonathan Sowah.
Kocha huyo alifafanua pia tofauti ya mechi za kirafiki walizocheza Misri na mtihani walioupata dhidi ya Gor Mahia.
“Leo (jana) ilikuwa zaidi ya kupata taarifa, kujua ni wachezaji gani wanashirikiana vizuri, nani anakamilisha uwezo wa mwingine. Tunatafuta uwiano sahihi wa mfumo huu wa 4-4-2 diamond pamoja na mingine ambayo tumekuwa tukiifanyia kazi,” alisema Fadlu.
Akizungumzia maandalizi ya dabi ya Ngao ikiwa ni mechi ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi, Fadlu alisema: “Tunapumzika kesho (jana) na kisha tunaanza maandalizi ya mechi ya Yanga. Huo ni mtihani mkubwa, ni fainali, ni mechi ya heshima. Baada ya hapo tutaelekeza nguvu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Tutafanya uchambuzi, mikutano binafsi na ya pamoja, ili kuweka mambo sawa.”
Kwa mashabiki wa Simba, Fadlu hakuwaacha nyuma alisema; “Naamini Ligi Kuu itaturuhusu kucheza mechi zetu za nyumbani hapa kwa sababu mashabiki wengi zaidi wataweza kutuona. Natoa shukrani kubwa kwa mashabiki waliokuja leo (juzi) na kutumia siku yao nasi. Tunahitaji msaada wao zaidi wiki ijayo, nusu ya uwanja uwe mwekundu. Hizo ndiyo mechi kubwa zinazohitaji umoja wa mashabiki na wachezaji. Tunaitazama mechi kwa shauku kubwa.”
Kwa upande wa kocha wa Gor Mahia maarufu kama ‘K’Ogalo, Charles Akonnor alisema licha ya kipigo hicho, wamejifunza mambo mengi ambayo anaamini yatakuwa msaada kwao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Kenya.
“Nadhani tumefanya vizuri sana, tulicheza kwa kujiamini. Tatizo letu lilikuwa kwenye kujilinda, goli la kwanza yalikuwa makosa binafsi lakini kwa ujumla nimefurahishwa na mchezo,” alisema Akonnor na kuongeza; “Kipindi cha pili nilifurahishwa zaidi kwa sababu wachezaji tuliowabadilisha walionyesha mambo mengi mazuri. Imetupa picha halisi ya kikosi chetu. Tumekuwa tukicheza mechi za kirafiki zenye viwango vya chini lakini hii ilikuwa ya kiwango cha juu sana, jambo ambalo ni jema kwetu.”
Akizungumzia Simba, Akonnor alisema; “Simba ni timu imara. Wanajua namna ya kucheza katika maeneo mihumu. Tulipata shida nao kipindi cha kwanza kwa sababu ya kasi yao, tulitaka kuwabana juu lakini tulishindwa. Baadaye tulibadili mbinu. Ni timu bora sana na msimu uliopita walifika hatua ya juu kwenye mashindano ya CAF. Nimevutiwa sana na nilichokiona, wana mustakabali mzuri. Niwape pongezi.”