Hamu ya mashabiki Yanga kuwaona mastaa laivu

YANGA leo Septemba 12 inafanya tamasha la saba la Wiki ya Mwananchi tangu lilipoanzishwa 2019, huku shauku kubwa ya mashabiki ni kutaka kuwaona wachezaji wapya laivu na burudani mbalimbali zinazoendelea.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao wamezungumzia furaha ya na namna tamasha hilo linavyozidi kuwa bora kila mwaka huku pia linawakutanisha pamoja kama mtoko.

Shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Cosmas Komba amesema hamu yake kubwa ni kuwaona wachezaji waliosajiliwa kupitia mechi ya kirafiki Yanga dhidi ya Bandari itakayopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Yanga wameondoka majembe kama Aziz Ki, Clatous Chama, Khalid Aucho lakini umakini wa viongozi wameingiza vyuma vingine kama Conte,Ecua,Andy Boyeli, Offen Chikola hao wote ni wachezaji wazuri,” amesema Komba na kuongeza:

“Pia natamani kuona watakavyocheza na Bandari ili nipate picha ya namna ambavyo mtani wetu Simba atakwenda kupigwa tena katika mechi ya Ngao ya Jamii inayotumika kama ufunguzi wa Ligi Kuu kwa msimu mpya.

“Yanga ni zamu yetu kuichapa Simba kwanza tuna kikosi bora cha wachezaji waliyozoeana pia tunajiamini zaidi kuliko wao.”

Shabiki wa Yanga lialia aliyejitambulisha kwa jina la Jesca Manji amesema: “Kwanza siku hii ni kubwa sana kwa Wanayanga kukutanika kwa pamoja kabla ya kuanza kwa msimu wa 2025/26 tunapata picha ya nini kinakwenda kufanyika.”

Ameongeza: “Nitakwenda kuwaona wachezaji laivu, burudani ya maana, pia mimi ni mfanyabiashara naingiza pesa.”

Shabiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ashati amesema: “Kwa namna ninavyoipenda Yanga nimeacha ratiba zangu za leo na kuja kujionea kila kitakachofanyika leo. Tamasha hilo linafanyika mara moja kwa mwaka.”