Hati ya Uwanja Yanga, ya kabidhiwa Lupaso, GSM aachiwa msala

KLABU ya Yanga imekabidhiwa rasmi hati ya ongezeko la kiwanja cha Jangwani, kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, huku viongozi wa timu hiyo wakimtangaza GSM kuwa mwekezaji wa uwanja huo.

Waziri wa Ardhi Deogratias Ndejembi, ndiye aliyefichua hayo alipotangaza katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi iliyofanyika leo Kwa Mkapa ambapo amesema sasa rasmi Yanga imepata kibali cha kuongezewa eneo, ili kukamilisha moja kati ya mpango wa muda mrefu waliojiwekea.

Waziri huyo ambaye naye ni Mwananchi, amesema hati hiyo ilitakiwa kutolewa ndani ya wiki mbili, lakini hata hivyo uongozi wa Wizara ya Ardhi umekamilisha mchakato huo kwa haraka kabla ya wiki mbili zilizotangazwa katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Jumapili iliyopita.

“Tunataka klabu kubwa kama Yanga ipate uwanja wake kwa haraka, ili kuhakikisha mashabiki ambao ni Watanzani wanapata burudani.”

KUHUSU MWEKEZAJI
Mara baada ya Waziri Ndejembi kumaliza kuzungumza, Rais wa Yanga, Hersi Said, amemtangaza Gharib Said Mohammed, kama mwekezaji wa uwanja huo.

“Nataka niwatangazie rasmi baada ya kupata hati kuwa, mwekezaji aa ujenzi wa uwanja huo ni ni GSM, ambaye amekuwa na Yanga bega kwa bega,” amesema Hersi.

GSM amekuwa mfadhili wa Yanga kwa misimu minne mfululizo, huku rekodi hiyo ikienda sawa na ile ya ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho mbali na timi kufanya vyema hata katika michuano ya kimataifa.