Hiki hapa chanzo cha ahaji ajali migodini

Dar es Salaam. Wakati mara kadhaa Serikali ikinyooshewa kidole pale zinapotokea ajali kwenye migodi, Kamishna Msaidizi Wizara ya Madini, Terrence Ngolo amesema ajali hizo haziwezi kuisha kutokana na watu kukiuka maelekezo ya wataalamu.

Amesema wakati mwingine ajali hizo hutokea kwa uzembe hasa pale wachimbaji wanapokiuka maelekezo ya tahadhari yanayotolewa na wataalamu.

Ngolo amesema hayo leo katika kipindi cha Hoja yako Mezani kilichoandaliwa na HakiRasilimali, kwamba usimamizi na ukaguzi unafanyika kwa kiasi kikubwa ila kinachotokea ni watu kupuuza maelekezo.

“Kwa ukaguzi kwenye migodi kwa sasa unafanyika kwa ufanisi zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma. Mojawapo ya sababu ya kuanzisha Tume ya Madini ni kuongeza na kuboresha usimamizi wa nyanja hiyo.

“Ninachoweza kusema ajali kwenye migodi haziwezi kuisha kwa sababu zipo zinazotokea kwa uzembe na nyingine ni za asili tu, imenyesha mvua watu hawakujiandaa inatokea ule mgodi umeanguka, sio kila kitu ni uzembe wakati mwingine ni mazingira tu,” amesema na kuongeza;

“Udhibiti wa sekta wakati mwingine unakuwa mgumu, huwezi kuweka polisi kwenye migodi. Nina mfano wa taarifa niliyopata kwa mmoja wa wakaguzi alienda kukagua mgodi akaona una hali mbaya akaweka geti ili watu wasiingie lakini walilivunja wakaingia.”