Kagere ‘ajilipua’…. Asema jambo zito akimtaja Fei Toto

STRAIKA wa zamani wa Simba, Meddie Kagere amesema Tanzania ina wanasoka wazawa wenye vipaji vya juu na miongoni mwao ni kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, aliyempa ujanja kwamba siku atakapoamua kwenda kucheza soka la kulipwa nje atakuwa moto zaidi.

Kagere aliyekuwa akiitumikia Namungo na kumaliza na mabao mawili msimu uliyopita, alichambua uchezaji wa Fei Toto namna anavyoweza kufunga eneo lolote kitu ambacho ni adimu sana kufanyika kwa wachezaji wengi.

“Fei Toto ni kijana mwenye kipaji cha aina yake akiwa na mpira ana uwezo wa kuona nafasi ya kufunga eneo lolote analokuwepo kwa maana ya mbali na karibu mchezaji wa aina hiyo anawapa kazi makipa kumsoma vizuri,” alisema Kagere na kuongeza:

“Angefanikiwa kwenda kucheza nje anaweza akaongeza vitu vikubwa sana ambavyo vitaisaidia timu ya taifa ya Tanzania. Nasema hilo nina ushahidi nalo. Nimecheza nje, nilijifunza vitu vingi.”

Kagere anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu na kutetea taji, huku akiwa pia ni nyota wa kigeni aliyewahi kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu kwa msimu mmoja alisema: “Kati ya vitu vikubwa nilivyojifunza nje ni kwenda na muda kwa kila jambo, kuishi katika misingi ya kazi ambayo itakufanya uwe katika muendelezo wa kiwango kwa muda mrefu. Ukiacha Fei Toto wachezaji wengine baadhi wenye vipaji vya juu ni Jonas Mkude, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, John Bocco alikuwepo mwingine alikuwa beki wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro.”

Kagere kwa misimu nane aliyecheza hapa nchini amefunga jumla ya mabao 77 akiwa ndiye kinara wa nyota wa kigeni waliofunga mabao mengi zaidi katika ligi akimpiku Amissi Tambwe aliyefunga 75 kupitia misimu saba pia.

Kwa Fei Toto aliyekuwa akiwindwa na vigogo Simba na Yanga sambamba na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kabla ya kuamua kuongeza mkataba wa kusalia Azam FC, msimu uliopita ndiye aliyekuwa kinara wa asisti akiwa na 13 na kufunga mabao manne.

Kabla ya hapo msimu wa 2023-2024, Fei alimaliza kama mfungaji namba mbili wa Ligi akiwa na mabao 19 nyuma ya aliyekuwa kinara, Stephane Aziz KI aliyemaliza na 21.