Kwa Yanga hii Folz anatamba nje, ndani

WANAYANGA wanaweza kutembea kifua mbele wakati msimu wa 2025-2026 ukikaribia kuanza kwani uongozi wa klabu hiyo umefanya uwekezaji mzuri katika kujenga kikosi imara.

Ukiangalia katika usajili wa dirisha kubwa uliofungwa Septemba 7, 2025, kuna nyota wapya 11 wamesajiliwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Ngao ya Jamii.

Nyota hao wapya ambao watatambulishwa rasmi mbele ya mashabiki leo, Septemba 12, 2025 katika kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi ni mabeki Frank Assinki, Mohamed Hussein na Abubakar Nizar Othuman ‘Ninju’.

Viungo kuna Moussa Balla Conte, Abdulnassir Mohamed Abdallah ‘Casemiro’, Mohamed Doumbia na Lassine Kouma.

Pia kuna Offen Chikola, Celestin Ecua na Edmund John wenye uwezo wa kucheza winga zote kulia na kushoto na Andy Boyeli ni mshambuliaji wa kati.

Katika kuimarisha kikosi hicho, Yanga ina jeshi la mauaji ambalo mpinzani akitia mguu kizembe, anaweza kuondoka na maumivu makali sana.

Wakati Yanga inasajili, kuna nyota wameondoka ambao wapo waliouzwa na wengine mikataba imeisha.

Nyota hao ni Aziz Ki ambaye ameuzwa kwenda Wydad Casablanca ya Morocco. Wengine ni Khalid Aucho, Clatous Chama, Kennedy Musonda na Jonas Mkude mikataba yao imemalizika, huku Nickson Kibabage akipelekwa Singida Black Stars kwa mkopo, bila ya kusahau Kouassi Attohoula Yao ambaye ana majeraha ya muda mrefu kidogo ikielezwa amewekwa pembeni.

Wakati wa maandalizi ya msimu, Yanga ilipiga kambi hapahapa nchini, ikienda mara moja Rwanda kucheza mechi ilipoalikwa na Rayon Sports, kisha ikarejea Dar.

Timu hiyo imeshinda mechi zote tano za kirafiki ilizocheza matokeo yakiwa hivi; Yanga 4-0 Yanga U20, Yanga 3-1 Rayon Sports, Yanga 2-1 Fountain Gate, Yanga 4-0 Tabora United na Yanga 2-1 JKT Tanzania.

Hapa Mwanaspoti linakuwekea kikosi cha mauaji cha Yanga SC kwa msimu wa 2025-2026. Kuna kikosi cha kwanza chenye wachezaji wote waliokuwepo msimu uliopita, huku kile cha pili kikiwa na nyota watatu pekee wa zamani, tisa wapya.

Jeshi la Yanga ambalo unaweza kusema lina majembe ya maana kabisa, golini anakaa Djigui Diarra, beki wa kulia Israel Mwenda na kushoto Chadrack Boka. Mabeki wa kati Dickson Job na Ibrahim Bacca.

Kiungo mkabaji anakaa Duke Abuya, namba nane anasimama Mudathir Yahya. Winga ya kulia Maxi Nzengeli, kushoto Clement Mzize. Mshambuliaji wa mwisho Prince Dube wakati Pacome Zouzoua akicheza nafasi ya mshambuliaji wa pili.

Hiki bila ya kuwaweka nyota waliokuwepo kikosi cha kwanza, nacho kina balaa lake na kinaundwa na nyota wengi wapya. Golini anakaa Khomeiny Abubakar, beki wa kulia Kibwana Shomari na kushoto Mohamed Husein. Mabeki wa kati anasimama Bakari Mwamnyeto na Frank Assinki.

Kiungo wa chini Moussa Balla Conte na kiungo wa juu Mohamed Doumbia. Winga ya kulia anasimama Edmund John, kushoto Celestine Ecua.

Andy Boyel anakuwa mshambuliaji wa mwisho, huku Offen Chikola akicheza namba 10 akiwa mshambuliaji wa pili.

MAJEMBE MENGINE HAYA HAPA

Aboutwalib Mshery (kipa), Abubakar Nizar ‘Ninju’ (beki wa kati na kulia), Aziz Andabwile (kiungo mkabaji na beki wa kati), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (kiungo mkabaji), Denis Nkane (winga), Lasine Kouma (kiungo mchezeshaji), Abdulnassir Abdallah ‘Casemiro’ (kiungo mchezeshaji), Shekhan Khamis (kiungo mshambuliaji) na Farid Mussa (winga).