Majaliwa azindua kampeni za ubunge Nachingwea

Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua kampeni za ubunge Nachingwea, akitoa wito kwa wananchi kuchagua wagombea wote wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza kwenye kampeni zilizofanyika uwanja wa maegesho ya malori Nachingwea mjini, leo Septemba 12, 2025 amesema wagombea hao wakichaguliwa wataendelea kuitekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 na kuiwezesha Nachingwea kupaa kwa kasi kimaendeleo.

“Jitokezeni kwa wingi kwenda kupiga kura ifikapo Oktoba 29, nendeni mkamchague Samia (Suluhu Hassan) kwa kura nyingi, kamchagueni pia Fadhili Liwaka, hatupaswi kulala. Hata kama ni mgombea pekee nendeni mkaweke tiki muda utakapofika,” amesema.

Majaliwa amesema wilaya za Ruangwa na Nachingwea zimeendelea kunufaika na miradi ya maendeleo ukiwamo wa maji kutoka Nyangao, Ruangwa hadi Nachingwea ambao unaendelea kutekelezwa.

“Mradi huu utakaonufaisha vijiji vya Ruangwa na Nachingwea utagharimu Sh119 bilioni,” amesema.

Pia amesema Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nachingwea.

Majaliwa amesema amefanya kazi kwa karibu na Liwaka kwa kipindi kirefu, anamfahamu kwa uchapakazi wake na anaamini atajitoa kwa ajili ya maendeleo ya wana Nachingwea.

Mgombea ubunge Nachingwea, Liwaka ameahidi atajielekeza katika sekta za maendeleo zikiwamo za miundombinu, elimu, afya, kilimo na ufugaji.

“Kiu yangu kubwa katika sekta ya miundombinu ni ujenzi wa barabara ya Nachingwea hadi Masasi kwa kiwango cha lami, pamoja na hili, elimu ni ajenda niliyonayo ninataka kupunguza idadi ya wanafunzi, hasa wa kike wanaolala nyumbani na kwenda shuleni asubuhi kwa kujenga mabweni,” amesema.

Liwaka amesema ndoto yake ni kuhakikisha anamaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.