Mambo yanayowasibu wachimbaji wadogo migodini, ufumbuzi watajwa

Dar es Salaam. Licha ya kuwa uchimbaji wa madini ni moja ya shughuli zinazovutia watu wengi, hususan wachimbaji wadogo, bado kundi hilo linakabiliwa na changamoto nyingi zinazohatarisha usalama na afya zao.

Miongoni mwa changamoto kubwa ni matumizi ya kemikali hatari kama zebaki, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa takribani asilimia 71 ya shughuli za uchimbaji nchini zinahusisha matumizi ya kemikali hiyo.

Akizungumza leo Septemba 12, 2025 katika kipindi cha Hoja yako Mezani kilichoandaliwa na HakiRasilimali, Irene Mosha amesema kati ya migodi 237 iliyopo nchini matumizi ya zebaki yamebainika katika migodi 197.

“Asilimia 71 ya uchimbaji unaotumia zebaki uko karibu  na makazi ya watu unaweza kupata picha ni madhara kiasi gani. Hii inatuambia kwamba bado kuna matumizi makubwa ya zebaki na athari zake ni kubwa.Ule mvuke unaharibu mapafu, ini, figo,” amesema.

Irene amesema wachimbaji wadogo wanawake ni waathirika wakubwa katika hilo ambapo takwimu zinaonesha wapo asilimia 40.

Amesema changamoto nyingine inayolikabili kundi hilo ni urasimu wa kupata vibali na leseni za uchimbaji, hali inayosababisha wengi wao kufanya shughuli za uchimbaji bila kufuata taratibu.

Kukabiliana na hilo Irene amesema HakiRasilimali kwa kushirikiana na ubalozi wa Canada inatekeleza mradi unaowafundisha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa.

“Huwa tunawapa elimu ni jinsi gani wanaweza kufuata viwango vya kimataifa, wakajipima. Ni muhimu kwao wajue ni kitu gani wanapaswa kufanya na wajumuishe katika sera na sheria.

“Mabadiliko mengi ya sheria yanatokana lakini wachimbaji wadogo hawana uelewa wa hayo yanayofanyika,” amesema.

Utaratibu wa kuzingatia sheria

Kwa upande Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Terence Ngole, amesema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia sekta hiyo.

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa masuala ya mazingira, jamii, na usimamizi wa shughuli za uchimbaji wa madini yanazingatiwa kwa kufuata utaratibu unaostahili.

Ngole ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo, kutasaidia kulinda mazingira ya maeneo yanayofanyika shughuli hizo na kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo wanapata manufaa ya moja kwa moja.

Ameongeza kuwa usimamizi huo ni endelevu kwa vizazi na vizazi.

“Kuna sheria inayozungumzia usalama, afya na mazingira katika maeneo yanayofanyika shughuli hizo iwe migodi mikubwa au midogo,” amesema.

Ametolea mfano kabla ya mgodi kuanza kuchimba wahusika huwasilisha mpango wa uchimbaji ‘Mining Plan’ kuhakikisha unakidhi viwango vya kimazingira na kiusalama.

“Kuna sheria inayosimamia wachimbaji wadogo ambayo inakataza kuajiri mtu mwenye chini ya miaka 18, lengo ni kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa,” amesema.

Amesisitiza kuwa yeyote anayekiuka sheria zinazoongoza shughuli huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya Madini, Filbert Rweyemamu amesema shughuli za uchimbaji madini zimeidhinishwa katika Katiba ya nchi kupitia sheria nne na hakuna uchimbaji unaofanyika bila sheria hizo kufuatwa.

Amezitaja sheria hizo kuwa Sheria ya Uhifadhi ya Mazingira ya mwaka 2004 na Sheria ya Madini 2010 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2017

Sheria nyingine ni ya Serikali za Mitaa ya 1982 ambayo inahusu ushirikishwaji wa jamii na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sheria ya ardhi ya vijiji mwaka 1999 ambayo inalinda haki za wananchi katika kuchukua ardhi.

“Shughuli zote za madini kuanzia utafiti ni lazima ziwe zimepita kwenye hatua hizo ikihusisha upatikanaji wa vibali ambavyo huwa havipatikani bila kuhusisha wananchi na mamlaka zinazowalinda wananchi kwenye eneo husika.

“Hakuna uchimbaji utakaotokea bila kupitia ngazi zote. Malalamiko yapo ila cha msingi ni kwamba sheria za ardhi zinalinda haki ya jamii, hakuna namna utakiuka. Watu wanajadiliwa, wanahusishwa na kuna namna ya watu kuwasilisha malalamiko yao.

Amesema Sheria ya Hifadhi ya Mazingira inamlazimisha mwekezaji kupitia Serikali kujua vipaumbele vya wananchi ili kuhakikisha madhara yanayoweza kuletwa kutokana na uchimbaji yanazuiwa.

“Kampuni zinatakiwa kuwajibika yanapotokea malalamiko. Ila inawezekana malalamiko yanatokea kwa sababu hawana uelewa wa kutosha au waliyokubaliana hayakutimizwa.”