Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameendelea na ziara zake katika baadhi ya matawi ya jijini Dar es Salaam kukutana na wateja ikiwa ni siku chache baada ya Benki kukamilisha maboresho makubwa ya mfumo wake mkuu wa utoaji huduma (Core Banking System).
Akiwa katika tawi la CRDB TPA lililopo katika jengo la Bandari jijini Dar es Salaam alikozungumza na mameneja wa matawi ya Kanda ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na wanahabari, Nsekela alipata fursa pia ya kuzungumza na wateja waliokuwa wakihudumiwa. Aliwashukuru wateja kwa ushirikiano na uvumilivu wao katika kipindi cha mabadiliko huku akiwahakikishia kuwa huduma za Benki zinaendelea kuimarika kila siku tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya.
“Kuanzia tarehe 8 Septemba tulihamia kwenye mfumo mkuu wa utoaji huduma za benki ambapo, kwa ukubwa wa mabadiliko yaliyofanyika, baadhi ya wateja wetu walipata changamoto katika akaunti zao na baadhi ya miamala kutofanikiwa. Juhudi za wataalamu wetu zimefanyika usiku na mchana, na hadi jana akaunti zilizokuwa na changamoto zilirudi katika hali yake ya kawaida. Aidha, wateja ambao miamala yao ilikwama walirudishiwa fedha katika akaunti zao na miamala kuendelea kufanyika kwa ufanisi,” amesema Nsekela.
Aidha, Nsekela amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika mfumo huu mpya umezingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wateja, na mabadiliko hayo yametekelezwa katika nchi zote ambako Benki ya CRDB inafanya biashara yaani Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) – huduma zinaendelea vizuri. Vilevile, ameongeza kuwa mageuzi hayo yanaweka msingi wa Benki kujitanua kimataifa, ambapo hivi karibuni Benki ya CRDB imepata leseni ya kuanzisha ofisi Dubai.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa pamoja na mabadiliko yaliyotokea, Benki bado imeendelea kufanya vizuri kibiashara ikithibitisha imani kubwa ya wateja waliyonayo kwa Benki yao. Vilevile ametumia fursa hiyo kuwashukuru wafanyakazi wote kwa kujitoa kwao katika kipindi hiki cha mabadiliko na akawahimiza kuendelea kusimamia weledi katika utoaji huduma ili kuhakikisha mfumo mpya unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela
(kushoto) akihudumia na kupokea maoni ya wateja kuhusu maboresho ya
mfumo mkuu wa uendeshaji wa huduma yaliyofanyika hivi karibuni katika
tawi la Benki ya CRDB TPA
lililopo katika Jengo la bandari jijini Dar es Salaam.
(katikati) akiangalia namna huduma zinavyotolewa kwa wateja kupitia
mfumo mkuu wa uendeshaji wa huduma ulioanza kutumika hivi karibuni.
Amefanya ukaguzi huo katika
tawi la Benki ya CRDB TPA lililopo katika Jengo la bandari jijini Dar
es Salaam alikotembelea kusikiliza na kupokea maoni ya wateja kuhusu
maboresho ya yaliyofanyika hivi karibuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela
(kushoto) akimsikiliza Lella Mushi, mmoja wa mawakala wanaotoa huduma
za Benki ya CRDB alipomkuta katika tawi la Benki ya CRDB TPA lililopo
katika Jengo la bandari
jijini Dar es Salaam alikotembelea ili kusikiliza na kupokea maoni ya
wateja kuhusu maboresho ya mfumo mkuu wa uendeshaji wa huduma
yaliyofanyika hivi karibuni.