Morogoro. Kata ya Pemba wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, ni ya kupigiwa mfano katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira.
Miradi hiyo inakwenda sambamba na uboreshaji wa maisha ya wananchi kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia na biashara ya kaboni.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ya uboreshaji misitu asilia inayotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la PAMS Foundation, ambayo imeunganisha uhifadhi wa misitu na maendeleo ya kijamii, huku wananchi wakinufaika moja kwa moja.
Mratibu wa mradi huo, Richard Paul anasema makubaliano ya muda mrefu kati ya shirika hilo na vijiji sita vya Kata ya Pemba ambavyo ni Maskati, Gonja, Mafuta, Pemba, Semwali na Dibago, yamefungua ukurasa mpya wa uhifadhi endelevu.
Makubaliano hayo yalisainiwa mwaka 2022 yakilenga kupanda miti ya asili kurejesha uoto uliopotea kutokana na shughuli za kibinadamu. Wananchi walipatiwa mitungi ya gesi kama mbadala wa kuni na mkaa.
“Tunalenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuwaingiza wananchi kwenye biashara ya kaboni. Hadi sasa zaidi ya vijana 40 wamepata ajira za kudumu na zaidi ya ekari 300 zimeandaliwa kupitia ajira zisizo rasmi,” anasema.
Takwimu za mradi zinaonesha ekari 945 zimepandwa miti ya asili, kila moja ikipandwa takribani miti 450. Miti zaidi ya 200,000 imepandwa.
Vilevile, mashamba 538 yenye ekari 1,560 yamepimwa na kuingizwa kwenye mradi, huku wananchi wakipatiwa Sh250 milioni kama fidia ya mazao ya kudumu na malipo ya ushiriki.
Ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, wanufaika wa mradi wamepewa mitungi ya gesi kama motisha.
Paul anasema walinzi bora wa mashamba na wafanyakazi wa vitalu vya miche ndio wanaopewa kipaumbele cha kupata gesi.
Mwanzoni anasema mradi ulikabiliwa na changamoto, kwani baadhi ya wananchi walihofia kupokwa mashamba yao.
Hali hiyo ilitatuliwa kwa kushirikiana na halmashauri kuandaa hati miliki za kimila kwa wakulima, hatua iliyowapa uhakika wa umiliki na fursa ya kupata mikopo.
Mradi huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024/2034, unaolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuongeza matumizi ya nishati mbadala vijijini.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Maulid Dotto akiwa ziarani Gonja aliwataka wananchi kuilinda miradi hiyo.
“Mradi huu umebeba fursa nyingi za kiuchumi na kijamii, ikiwamo ajira na elimu ya uhifadhi. Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha malengo yanafanikiwa,” anasema.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Dk Mussa Ali Mussa, alipongeza PAMS Foundation kwa mchango wake wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kurejesha misitu.
“Wananchi wananufaika mara mbili, afya zao zinalindwa kwa kuepuka moshi wa kuni na mkaa, pia misitu inarejeshwa,” anasema.
Anasema juhudi hizo zinaunga mkono malengo ya kitaifa ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Kwa kuzingatia historia ya kilimo cha viungo katika Kata ya Pemba, Serikali ya mkoa imepanga kuendeleza sekta hiyo kwa kutoa miche bure ikiwamo ya karafuu na iliki ili kuongeza kipato cha wananchi sambamba na kulinda misitu.
Silili Anthony, mmoja wa vijana wanaofanya kazi kwenye kitalu cha miche Pemba, anasema: “Mbali na ajira, tumeelimishwa umuhimu wa mazingira. Nilikuwa natumia kuni lakini sasa natumia gesi niliyopatiwa na ninaona faida zake kiafya na kimazingira.”
Bibiana Kanyika, mkazi wa Kijiji cha Gonja, anaeleza: “Kupika kwa gesi kumeniondolea adha ya moshi na kero ya kutafuta kuni, hasa wakati wa mvua. Ombi langu, Serikali isaidie kupunguza gharama za gesi na kusogeza huduma karibu zaidi.”
Kwa mujibu wa Wizara ya Muungano na Mazingira, Tanzania inalenga kupata hadi Dola bilioni moja za Marekani (takribani Sh2.4 trilioni) kwa mwaka kutokana na biashara ya kaboni.
Hadi Machi 2024, miradi 24 ilikuwa imesajiliwa na tayari Dola milioni 12.63 (takribani Sh32 bilioni) zimelipwa kwa mamlaka za serikali za mitaa.
Mvomero ikiwa miongoni mwa maeneo yanayotekeleza miradi hiyo, imeanza kunufaika kupitia ajira, mapato na uhifadhi wa mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Dotto anasema biashara ya hewa ukaa ni fursa ya kiuchumi kwa vijiji na halmashauri, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu.
Habari hii imedhaminiwa na Taasisi ya Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.