::::::::::
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 zimeendelea Wilayani Karagwe ambapo Mwenge huo umefanya uzinduzi, uwekaji wa jiwe la msingi na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.58, leo tarehe 12 Septemba 2025.
Miradi iliyozinduliwa na kutembelewa ni pamoja na Kituo cha Afya Nyabiyonza, ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita tatu, vyumba 24 vya biashara katika stendi ndogo ya magari Bohari, mradi wa maji Rwamugurusi, mradi wa vijana wa kuchakata taka ngumu (KIUMA), nyumba ya Watumishi Shule ya Sekondari Omurushaka, pamoja na mradi wa uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi na salama.
Mbio hizo ziliambatana na kaulimbiu isemayo “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu” na ziliongozwa na Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi, ambaye alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Hafla ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Laizer, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani.
Akiongea na wananchi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, alipongeza mbio hizo kwa kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuipatia Wilaya ya Karagwe fedha nyingi za maendeleo.
Bashungwa alibainisha kuwa Wilaya ya Karagwe imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya kwa kuwa na Hospitali ya Wilaya yenye uwezo wa kutoa huduma zote muhimu, pamoja na vituo vya afya vilivyosambazwa katika tarafa zote za Wilaya hiyo.