Mwinyi, Othman kugawana visiwa kuzisaka kura Zanzibar

Unguja. Wakati kesho zikianza rasmi kampeni za Uchaguzi Mkuu Zanzibar, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT-Wazalendo vinatarajia kugawana visiwa katika ufunguzi.

CCM itazindulia kampeni zake katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Unguja kuanzia saa 2:00 asubuhi, huku ACT-Wazalendo kikizindua kisiwani Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 12, 2025, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi amesema wanatarajia kufanya kampeni za kistaarabu, mshikamano na umoja kwa kuwaeleza wananchi sera ambazo zitawanufaisha, badala ya kuzungumza masuala binafsi ya watu.

“Kesho tunazindua kampeni lakini niwasihi wagombea wenzangu kuzungmza sera badala ya kuongea mambo ya kuleta taharuki na vurugu, sisi tunaahidi tutahakikisha tunaeleza tutakayowafanyia wananchi iwapo wakitupa ridhaa ya kuongoza tena,” amesema Dk Mwinyi, Rais anayemaliza muda wake.

Dk Mwinyi amesema ni jambo la kushukuru Mungu mpaka sasa bado hakujaonekana viashiria vya chokochoko na kuvunja amani ukilinganisha na vipindi ambavyo vimetangulia.

Amesema ni imani yao hali itaendelea katika mazingira hayo, huku akiwataka wananchi wasikubali kuelezwa mambo yasiyokuwa na tija kwao.

Ameeleza pia mambo ambayo yatapewa kipaumbele iwapo CCM itapata ridhaa ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za maisha zinazosababishwa na mfumko wa bei.

Amesema mfumko huo unasababishwa na kuongezeka gharama za vyakula na mafuta, hivyo wanatarajia kujenga maghala ya kuhifadhi chakula na mafuta kukabiliana na changamoto hiyo.

“Kwanza tunakwenda kuwa na mpango unaitwa strategic food reserve, hii ina maana kwamba, tutakuwa na maghala makubwa kuhakikisha tunakuwa na chakula cha kutosha wakati wote, ili wananchi wapate huduma hiyo kwa wepesi,” amesema na kuongeza:

“Kwa sasa ugumu wa maisha unaosemwa unaweza kusababishwa na mfumuko wa bei unaosabaishwa na vitu viwili, chakula kupanda bei na mafuta, lakini tukiweza kudhibiti vitu hivi tuna imani tutaweza kumudu kupunguza hicho kinachoonekana kupanda kwa maisha.

ACT-Wazalendo kwa upande wake, baada ya mgombea wake kuteuliwa na ZEC, kampeni zinaanza leo katika viwanja vya Tibirizi, Chake Chake, Pemba.

Akizungumza juzi na viongozi katika ofisi za chama hicho kuhusu hatua hiyo juzi Septemba 10, mgombea wa Chama hicho, Othman Masoud Othman alisema wanajipanga kwa ushindi, akiwasisitiza wanachama kufanya kampeni kuhakikisha anapata ushindi na kushika madaraka.

Vyama 11 vimeteuliwa na ZEC kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ambavyo ni CCM, ACT-Wazalendo, Makini, Ada Tadea, NCCR-Mageuzi, NRA, ADC, NLD, AAFP, UPDP na TLP.

Katika hatua nnyingine, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kushirikiana na kamati ya amani kitaifa, wametoa mafunzo kwa wagombea uwakilishi, huku ikieleza vifaa vyote vilivyopangwa kutumika wakati wa uchaguzi mkuu vimekwishanunuliwa.

ZEC pia imesema karatasi za kupigia kura zinatarajiwa kukamilika wiki moja kuazia sasa.

Hayo yameelezwa leo Septemba 12, 2025 wakati wa mafunzo kwa wagombea wa ujumbe wa Baraza la Uawakilishi, majimbo na viti maalumu.

Licha ya ratiba ya ZEC kuruhusu kampeni kuanza Septemba 11, ratiba ya vyama zinaanza kesho Septemba 13, 2025.

Katika taarifa, Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Thabiti Idarous Faina leo Septemba 12, 2025 wakati wa mafunzo hayo, amesema maandalizi yameshakamilika, akiwataka wagombea kutoa ushirikiano kwa NEC kila utakapohitajika, ili kuepusha sintofahamu na malalamiko ambayo yanaweza kuepukika.

Faina amesema wameandikisha wapigakura 725,879, na idadi hiyo inajumuisha na wale ambao wamekosa sifa lakini hawajaondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura.

Kwa mujibu wa Faina mpaka sasa kuna watu 3,352 ambao wamekosa sifa na Tume inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuwabaini wengine ambao hawana sifa, hivyo idadi kamili ya watakaokuwa na sifa ya kupiga kura itatolewa Septemba 19, mwaka huu.

Amesema ZEC bado haijakamilisha kuhamisha taarifa kwa sababu sheria inawapa siku saba wagombea wa nafasi ya uwakilishi kuhamisha taarifa zao tangu walipoteuliwa, hivyo siku hizo zinatarajiwa kuisha Septemba 19.

Baadhi ya wagombea wa uwakilishi wamesema mpaka sasa wapo pamoja na utaratibu unaotumika na ZEC lakini changamoto huanza wanapoanza kampeni.

“Viongozi wetu wakuu wanapiga picha pamoja wanacheka na kufurahia, lakini huku unakuta watu wanapigana na kutoleana kauli zisizokuwa na msingi, tutumie mfano huu kama nyenzo ya kwenda nayo,” amesema Hamza Hassan Juma, mgombea kutoka CCM.

Mgombea kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Ali Saleh amesema kuna haja ya kutoa elimu kwa vikosi vya SMZ badala ya kutisha watu, wawe walinzi wa amani.

“Ipo haja ya kutoa elimu ili kuweka mazingira mazuri kwa vikosi hivi, maana kumekuwapo mazingira ya kutisha kwa wananchi,” amesema.

Hamida Abdalla kutoka CUF, amepongeza utaratibu wa kukutanishwa ili kuwekana sawa kuhusu namna ya kulinda amani wakati wa uchaguzi.

Katibu wa Baraza la Maaskofu Zanzibar, Timothy Kalenga amesema wanataka kuona uadilifu wa kila mmoja unapatikana katika kuwatumikia wananchi, kwani wakati mwingine wanajisahau wakishapata dhamana.

“Leo hii wengi wetu tutapiga na magoti ila mkishapata mnasahau hata simu hampokei, tunajisahau, ninyi mnapewa dhamana na wananchi,” amesema.

Amesema wanapaswa kuzingatia wajibu wao wa kuwatumikia wananchi waliowapa dhamana, badala ya kuwakimbia.

Sheikh Shaaban Batash kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, amesema wagombea wanawajibika kuhakikisha wanaleta amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

“Tunawajibu wa kuwafundisha wananchi kujua namna ya kutofautiana kimawazo na kimitizamo lakini isiwe kwa ugonvi na kuleta taharuki,” amesema.

Amesema wana wajibu kukemea ghasia na wananchi kuwa wastahimilivu kwa kuzingatia mafundisho kwa kuangalia masilahi ya jamii, badala ya kuangalia ya mtu mmoja mmoja.

Awali, akieleza wajibu wa vyama vya siasa kulinda hali ya usalama na amani, Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Sheria ZEC, Maulid Mohamed amesema vinatakiwa kulinda ushiriki wa makundi maalumu, kufuata maelekezo ya uchaguzi kuufanya uwe huru na haki.

“Ni wajibu wa chama cha siasa kuheshimu mgombea bila kusahau utu wake, wakiwamo wanawake na watu wenye ulemavu, pia kuheshimu muda wa kufanya kampeni,” amesema.

Amesema wajibu wa Tume ni kufuata sheria, Katiba na miongozo, kutopendelea chama chochote na kutoa taarifa na ufafanuzi wa jambo lolote linalofanyika na linalotakiwa kufanyika kwa uwazi.

“Pia inawajibika kuweka wazi kwa mgombea na chama ili wapate ufafanuzi au taarifa ya jambo linalotakiwa kufanyika na kushughulikia haraka malalamiko ya ukiukwaji wa maadili yanayofanywa na mtumishi wake,” amesema.

Kwa Serikali, amesema ina wajibu wa kutoa huduma kwa nafasi sawa kwa vyama vyote bila upendeleo, kuchukua hatua za kisheria kwa kiongozi atakayetaka kuhujumu na kutoa ulinzi wa vyama vyote vya siasa wakati wa kampeni.

“Marufuku watumishi wa Serikali kujiingiza kwenye siasa, kwenye ofisi za umma na ni wajibu wa vyombo vya habari vya Serikali kutoa nafasi sawa kwa kila mgombea,” amesema.

Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, amesema katika mchakato wa kuwapata wagombea mwaka huu umekwenda vizuri kuliko wakati mwingine wowote, akieleza hakukuwa na changamoto za pingamizi kubwa.

Katika msingi huo, amesema hakuna mgombea aliyeshindwa kuteuliwa kwa sababu ya kuwekewa pingamizi.