Mwita: Ninaijua Kibamba, nitashughulikia changamoto zilizopo

Dar es Salaam. Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kibamba, Otaigo Mwita, amesema amedhamiria kutatua changamoto zilizopo katani humo atakapopewa ridhaa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni zake leo Septemba 12, 2025 eneo la Kibamba Shule, amesema anaielewa vizuri hali ya kata hiyo kwa sababu amekulia na kuishi eneo hilo.

“Mimi ni mwanafamilia wa Kibamba, nimeishi hapa na najua changamoto binafsi na za kijamii. Hivyo, nitahakikisha tunapiga hatua katika miundombinu na huduma nyingine muhimu,” amesema.

Otaigo amesema ingawa baadhi ya miradi imeanzishwa, bado kuna maeneo yanahitaji maboresho, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vivuko kwenye sehemu zenye changamoto ya kuvuka, hasa Hondogo na Kibwegere.

“Ipo miradi iliyokamilika na mingine haijakamilika, lakini nikiwa diwani, nitahakikisha tunamaliza haya yote kwa haraka,” amesema.

Amesema maeneo mengi ya Kibamba bado yameathirika na miundombinu chakavu, akiahidi akichaguliwa atashirikiana na wananchi kuiboresha.

Mgombea huyo ameahidi atahakikisha majina ya mitaa ambayo hayajaingizwa kwenye mfumo rasmi yanaingizwa ili kurahisisha usimamizi na maendeleo ya kata.

Kuhusu changamoto ya usafiri na maegesho, amesema atahakikisha kuna utaratibu mzuri wa kuegesha vyombo vya moto na kuboresha mazingira kwa wajasiriamali wadogo, ambao mara nyingi hupata shida katika maeneo ya biashara.

Katika mkutano huo, mgombea ubunge Kibamba, Angellah Kairuki, alimnadi Otaigo pamoja na kumuombea kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan.

Kairuki amesema endapo wananchi wa kata hiyo watawapigia kura wagombea wa chama hicho, miradi yote inayotekelezwa jimbo la Kibamba haitasimama.

“Najua changamoto zinazotuandama, kama vile barabara mbovu, huduma za afya na shida ya maji, lakini kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wananchi, tunahitaji kuchagua viongozi wenye dhamira ya dhati ya kutatua matatizo yetu,” amesema.

Aliyekuwa mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu, amesema aliwahi kuwa diwani wa kata hiyo, hivyo atashirikiana na atakayechaguliwa kushughulikia changamoto za miundombinu, hasa barabara za Hondogo na Kibwegere.

“Ni heshima kwetu kuwa na diwani atakayekamilisha kazi tuliyoianza. Tumemuomba kwa dhati aende bungeni na kuleta suluhu za Kibamba,” amesema.