Mwongozo wa kupunguza swala ukiwa safari

Dar es Salaam. Miongoni mwa hukumu za safari ni kwamba inaruhusiwa msafiri kupunguza Sala (qasr) zenye rakaa nne ambazo ni Adhuhuri, Alasiri na Isha, kwa kuzisali rakaa mbili kila moja.

Hii ndiyo ilikuwa ni Sunna na muongozo wa Mtume(Rehema na amani ziwe juu yake) ambaye hakuwahi kusali kamili (rakaa nne) katika safari zake. Riwaya zinazodai kuwa aliwahi kusali kamili hazina usahihi.

Hukumu ya upunguzaji Sala zenye rakaa nne kwa msafiri ni sunna iliyo thabiti. Baadhi ya wanazuoni wamefikia kusema kuwa ni wajibu, kiasi kwamba anayesali rakaa nne badala ya mbili katika safari anakuwa ameacha jambo la lazima.

Hata hivyo, rai iliyo karibu zaidi na usahihi ni kwamba upunguzaji Sala Safarini si wajibu, bali ni sunna yenye kusisitizwa.

Khalifa wa tatu Uthman bin Affan (Allah Amridhie) alipokuwa Mina (akitoka Madina) alikamilisha Sala rakaa nne, baadhi ya Maswahaba walimkosoa. Ibn Masud (Allah Amridhie) aliposikia,  alishangaa jambo hilo na kuona kuwa ni mtihani mkubwa.

Hata hivyo, bado aliendelea kusali nyuma ya Uthman rakaa nne. Kama ingekuwa ni wajibu wa lazima, basi kusali rakaa nne kungekuwa ni haramu na kungebatilisha sala. Lakini kwa kuwa Maswahaba  walimfuata khalifa Uthman na wakaona sala yao ni sahihi, basi inaonyesha wazi kuwa kupunguza sala kwa msafiri si wajibu, bali ni sunna yenye kusisitizwa.

Iwapo msafiri atasali nyuma ya imamu anayekamilisha rakaa nne, basi ni wajibu naye asali rakaa nne, awe ameungana na imamu kuanzia mwanzo wa sala au aliungana naye katikati ya sala.
Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume wa Allah: “Imamu amewekwa (aongoze) ili kufuatwa (utendaji wake)”  Ibn Abbas (Allah Amridhie) alipo ulizwa: Kwa nini msafiri akisali peke yake anasali rakaa mbili, lakini akisali nyuma ya imamu (asiyekuwa msafiri) husali rakaa nne?” alijibu:

“Hiyo ndiyo sunna.”Vilevile, Ibn Umar (Allah Amridhie) alikuwa akisali rakaa mbili akiwa peke yake katika safari, lakini akisali nyuma ya imamu aliyekamilisha, naye alisali rakaa nne.

Watu wengi wa kawaida hudhani kuwa msafiri hatakiwi kuswali jamaa ya msikitini anapokuwa safarini. Lakini dhana hii si sahihi. Msafiri analazimika kuswali jamaa kwa mujibu wa maandiko ya Kisharia.

Allah Mtukufu ameamrisha hata waumini walioko vitani waswali kwa jamaa. “Na ulipo kuwa miongoni mwao ukawaswalisha, basi na wasimame pamoja nawe sehemu ya watu, na waichukue silaha zao…” (4: 102).

Ikiwa wapiganaji safarini wamelazimishwa kuswali jamaa, basi msafiri asiye katika vita ni zaidi ya kustahiki hilo. Kuna hali maalumu zinazoweza kumpa msafiri ruhusa ya kutoenda msikitini kuswali jamaa, nazo ni: Ikiwa ni msafiri wa kupita tu (transit) na kusimama kuswali jamaa kutasumbua safari yake.

Ikiwa yuko mbali sana na msikiti kiasi cha kumtaabisha. Ikiwa yupo katika nchi isiyo ya Kiislamu isiyokuwa na misikiti. Ikiwa yupo katika mji lakini hajui msikiti ulipo. Kwa hivyo, msafiri ana wajibu wa kuswali jamaa na Waislamu katika misikiti, isipokuwa awe na udhuru wa Kisharia. Hivyo basi, kinyume na wanavyodhani baadhi ya watu, si kweli kwamba msafiri hajawekewa sharti la kuswali jamaa.

Kwa upande wa msafiri, jambo bora zaidi ni kuswali kwa kupunguza Sala (qasr), kwani ni Sunna iliyosisitizwa (Sunna mu’akkada).Msafiri kadhalika anaruhusiwa kuunganisha sala (Jam’u), iwe ni wakati wa safari au akiwa amepumzika mahali (amekaa).

Sababu ni kwamba, kama vile sharia ilivyopunguza idadi ya rakaa katika safari, vivyo hivyo imeruhusu kupunguza sifa ya swala kwa kuunganisha badala ya kuswali kila moja katika wakati wake. Ikiwa msafiri yupo safarini akitembea, basi kuunganisha sala ni bora zaidi kuliko kutoziunganisha.

Ikiwa msafiri amepumzika na amekaa mahali (amepiga kambi), basi kutoziunganisha ni bora zaidi. Mfano wake ni Mtume alipokuwa Mina katika Hijja ya kuaga, hakuzijumuisha sala wakati amekaa (amepiga kambi).

Kuhusu ipi bora zaidi kati ya kuzikusanya mapema (jam‘ taqdim) mfano Sala ya Alasiri kuisali wakati wa Adhuhuri, au kuchelewesha (jam‘ ta’khir) mfano Sala ya Adhuhuri kuisali wakati Alasiri? Jawabu ni kwamba bora zaidi ni lile lililo rahisi kwa msafiri: Ikiwa ni rahisi zaidi kwake kuzikusanya mapema (jam‘ taqdim), basi hilo ndilo bora kwake.

Ikiwa ni rahisi zaidi kuchelewesha (jam‘ ta’khir), basi hilo ndilo bora kwake. Mtume alipokuwa akianza safari kabla ya jua kupinduka (kutoingia adhuhuri), alikuwa akichelewesha adhuhuri na kuunganisha na alasiri katika wakati wa alasiri.

Lakini jua lilipopinduka (kuingia adhuhuri) kabla ya kusafiri, alikuwa akiswali adhuhuri na alasiri kwa pamoja katika wakati wa adhuhuri kisha anaondoka. Kwa hiyo, kuunganisha sala (jam‘u) ni ruhusa kwa msafiri, na kuchagua kati ya kutaguliza au kuchelewesha kunategemea urahisi kwa msafiri.