Dar es Salaam. Kampeni ya nishati safi ya kupikia katika muktadha wa Dira ya Taifa 2025 inalenga kuokoa maisha, kuboresha afya za wanawake na watoto pamoja na kulinda mazingira.
Kutokana na mikakati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia amesema kuna kila sababu kwa wadau na Serikali kuunganisha nguvu kuhakikisha Taifa linapata matokeo chanya.
Amesema kutekelezwa kwa mikakati hiyo sio tu kutaokoa maisha bali kunakwenda kufungua fursa mpya za kiuchumi ikiwemo kuhakikisha kwamba, ifikapo 2034, kaya nane kati ya 10 zinapata nishati safi ya kupikia.
Rosalynn ameyasema hayo leo Ijumaa ya Septemba 12, 2025 katika Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na MCL lililobebwa na mada isemayo ‘Nishati Safi ya Kupikia: Okoa Maisha, Linda Mazingira’.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa nishati safi, MCL imejitolea kuhakikisha ajenda hiyo inasambaa nchini kote na nje ya mipaka kupitia magazeti, tovuti, mitandao ya kijamii na kupitia ushirikiano na redio mbalimbali ili kufikisha mjadala huo unafika kila kijiji, kila kaya na kwa kila mtu.
“Tunapanga pia mikusanyiko ya moja kwa moja mashinani ili kushirikisha jamii moja kwa moja na tunakaribisha ushirikiano na wadau wengine kuhakikisha uendelevu wa ajenda hii,” amesema.
Amewaita wadau kushirikiana katika kuelimisha, kuhamasisha na kuunda mustakabali bora wa nishati safi.
“Changamoto ni kubwa, lakini mafanikio yanawezekana tunapoamua kusimama kidete. Kwa pamoja tunaweza kujenga Tanzania yenye afya, usalama na ustawi kwa vizazi vijavyo kwa sababu ni hatua,” amesema Rosalynn.
Kongamano hilo linatarajiwa kuwa na zaidi ya washiriki 250, ukumbini na mtandaoni.
Kongamano hilo limewezeshwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Nishati, Wizara ya Maji, Nishati na Madini–Zanzibar, African Enterprise Challenge Fund (AECF), EWURA, Azania Group, Taifa Gas, NBC Bank, TANESCO, Natkern, na ZURA.
“Tunatambua pia mashirika na wadau wengine ambao kutokana na changamoto mbalimbali hawakuweza kushiriki nasi leo, lakini mchango wao umesaidia kuunda uzoefu huu wa pamoja. Tunawashukuru nyote,” amesema.