Tabora. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuupa hadhi yake Mkoa wa Tabora kama kitovu cha historia ya chama hicho iliyofanikisha uhuru wa Taifa hili.
Samia amebainisha hayo leo Septemba 12, 2025 mjini Tabora, wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, ukihudhuriwa na maelfu ya wananchi na wafuasi wa chama hicho.
Amesema Tabora ina nafasi ya pekee katika historia ya kisiasa ya Tanzania. Amesema mmoja wa waasisi na mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, Mwalimu Julius Nyerere alisoma Tabora na hata alipohitimu masomo yake Chuo Kikuu cha Makerere, alirudi Tabora kufundisha katika Shule ya St. Mary.

Vilevile, amesema uamuzi muhimu wa kihistoria uliofanyika Tabora mwaka 1958, ulifanywa na mkutano mkuu wa Tanu, wa kushiriki uchaguzi, uamuzi ambao uliisogeza Tanzania karibu na uhuru wake.
“Haya yote yamethibitisha kwamba CCM ina historia kubwa hapa Tabora. Mnara wa uamuzi ule wa busara wa Tanu, upo hapa Tabora hadi leo, na ambao ulikuwa hatua kuelekea uhuru wetu, leo nchi yetu inaendelea na mapambano ya uhuru wa kiuchumi.
“Uhuru wa kujenga Taifa lenye uchumi jumuishi linalotegemea ustawi wa watu wote. Tunataka kujenga uchumi jumuishi unaomgusa kila mtu,” amesema mgombea huyo.
Ili kufikia malengo hayo ya kuupa hadhi mkoa huo, Samia amesema wametekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba katika miaka mitano ijayo, wanakwenda kufanya mambo mengine ya kuukuza mkoa huo hususani Tabora mjini.

Amesema wanakwenda kujenga kituo cha kupooza umeme katika mkoa huo ili kuleta upatikanaji wa umeme katika vitongoji ndani ya mkoa huo.
Pia, ameongeza kuwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora unaendelea na sasa umefikia asilimia 95, ukikamilika unatarajiwa kuufungua mkoa huo.
Kwenye sekta ya kilimo, Samia amesema wataendelea kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima na pia wataboresha minada na kujenga majosho ili wazalishe na kuhudumia mifugo yao vizuri.
“Kwa upande wa maji, tumefanya kazi kubwa, miradi mbalimbali ya maji inatekelezwa katika mkoa huu. Tunatarajia kila mwana Tabora awe na maji ya kutosha. Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na ule wa miji 28, itakwenda kumaliza kabisa shida ya maji,” amesema.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, amesema watajenga barabara mpya ya mzunguko, itakayokuwa na urefu wa kilomita 82, ili magari yasiyokuwa na ulazima wa kupita ndani ya mji, yapite nje kwa kutumia barabara hiyo.
“Tunataka Tabora yenye historia kubwa, iwe na hadhi kubwa pia,” amesema Samia huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi kwenye mkutano huo.

Katika hatua nyingine, amesema wanakwenda kujenga madaraja 133 katika barabara ambazo zimewekwa kwenye ilani ya uchaguzi. Pia, amesema wanakwenda kuweka taa za barabarani 2,300 ili vijana wa Tabora wafanye shughuli zao wakati wote.
“Tunakwenda kuweka taa za barabarani 2,300, kwa hiyo, Tabora na wilaya za Tabora zitapata fursa ya kufanya biashara kwa saa 24 kwa sababu umeme ni usalama, umeme ni mwanga,” amesema Samia.
Wagombea ubunge waeleza mikakati yao
Mgombea ubunge wa Tabora Mjini, Hawa Mwaifunga amesema akiwa mjumbe wa kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, amejionea kazi kubwa iliyofanywa na Samia katika miaka minne ya uongozi wake.
Amesema Samia amefanya kazi kubwa katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya kwenye kata zote za jimbo hilo, jambo ambalo limeboresha huduma na kuzisogeza kwa wananchi.
Kwa upande wa elimu, amesema wamejenga shule za msingi mpya nne na kwamba tayari wana Sh2 bilioni kwa ajili ya kujenga shule nyingine mbili za msingi.

“Mkoa wetu ulikuwa moja ya mikoa mitatu ambayo watoto wanapata ujauzito wakiwa wadogo, kwa kuliona hilo, ulijenga shule za sekondari katika kata za pembezoni, leo hii idadi ya watoto wanaopata mimba imepunguza kwa sababu wanakwenda shule,” amesema.
Mgombea huyo amemuomba kuukarabati uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ili utumike katika michezo mbalimbali na pia ili iwe kumbukumbu nzuri kwa jina hilo la Rais wa awamu ya pili.
Kwa upande wake, Aziza Ally, mgombea ubunge wa viti maalumu, amesema matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, figo na moyo yamekuwa na gharama kubwa, kaya nyingi zinashindwa kuwahudumia wagonjwa hawa, hivyo ahadi yake ya kuwapatia matibabu ni faraja kwao.
“Wakati unazindua kampeni, ulisema Serikali itawatibu wagonjwa hawa wasio na uwezo. Kwa uamuzi huo ndugu mgombea, umegusa familia nyingi za Watanzania, tunakushukuru sana,” amesema.
Kwa upande wake, Christina Mndeme, mgombea wa viti maalumu, amempongeza Samia kwa kuwanyanyua wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi, akiwemo yeye ambaye alimteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM na pia Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Amesema Watanzania wameipokea kampeni ya nishati safi kwani inalenga kulinda afya za wananchi na kutunza mazingira, ameahidi kuendeleza kuilinda kampeni hiyo ili wananchi wote watumie nishati safi.
“Sisi wana Tabora tunajivunia kazi kubwa uliyoifanya mkoani kwetu, tunakuahidi kura nyingi za kishindo, wanawake wa Tabora tumejipanga, kura zote kwa Samia,” amesema Mndeme.
Mgombea ubunge wa Sikonge, Amos Maganga amemshukuru Samia kwa kuwatafutia masoko na malipo yao wakulima wa tumbaku katika mkoa huo.
Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewataka wananchi wa Tabora kulinda historia ya chama chao kwani mwaka 1958, mkutano mkuu wa Tanu uliofanyika Tabora ulifanya uamuzi wa busara.
Amesema uamuzi huo ulikuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa chama hicho, hivyo amewataka wazee wa mkoa huo kuhifadhi historia hiyo kwa ajili ya vizazi vijavyo.
“Wakati vijana na wanawake mnasema mna jambo lenu, wazee nao wana jambo lao. Niwaombe vijana mnaopata nafasi za uongozi, fuateni busara za wazee,” amesema Dk Bashiru.