Dar es Salaam. Licha ya jitihada zinazoendelea kufanyika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Watanzania wengi bado wanatumia isiyo salama, hali inayohatarisha afya zao na kuharibu mazingira.
Hatua hiyo inaifanya Serikali kusimama kikamilifu katika utekelezaji wa mkakati unaolenga kufikia 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, akizungumza leo Septemba 12, 2025 kwenye kongamano la nishati safi ya kupikia lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) lililobebwa na mada isemayo: “Nishati safi ya kupikia: Okoa maisha, linda mazingira” ameeleza kuwa matumizi ya nishati isiyo safi bado ni tatizo kubwa.
Amesema takribani asilimia 80 ya kaya zinategemea nishati ya kuni na mkaa.
Mramba amesema: “Idadi hii ni kubwa na kwa pamoja tunahitaji kufanya kitu kwa ajili ya kurekebisha hali hiyo. Inawaweka wananchi katika hatari za kiafya, inachochea ukataji miti hovyo na kuongeza mzigo mkubwa wa kiuchumi kwa kaya, hasa kwa wanawake na watoto.”
“Takwimu tulizonazo takribani hekta elfu 466 za misitu hupotea kila mwaka kutokana na kukata miti, tunaharibu mazingira na kutumia fedha nyingi wakati tafiti zinaonyesha nishati isiyo safi ni ghali zaidi kuliko nishati safi zilizoko kwa sasa,” amesema.
Akitoa mfano, amesema kwa kutumia jiko la umeme mlo mmoja unaweza kupikwa na kugharimu kati ya Sh200 hadi Sh250 na mlo kama huo ukipikwa kwa mkaa unagharimu si chini ya Sh1,000.
Mbali ya athari za mazingira na gharama, zipo athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ikielezwa takribani watu 33,000 hufariki dunia kwa mwaka nchini kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua, ambayo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na uvutaji wa moshi unaotokana na matumizi ya nishati ya kupikia isiyo safi.
“Mama anaweza kuwa anapika na mtoto wake mgongoni au jirani yake anapika katika mazingira ya moshi kwa miaka mingi, ile athari ya moshi inaathiri miili yao. Kwa sababu ya athari hizo, ndipo Serikali ikaja na mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa miaka 10,” amesema.
Akizungumza kwenye jukwaa hilo, amesema lazima elimu iendelee kutolewa pamoja na nguvu kuwekezwa zaidi ili watu waendelee kuhama kutoka nishati isiyo safi kuja kwenye nishati safi.
Mramba amesema miongoni mwa malengo ya mkakati wa miaka 10 ni kuongeza uelewa wa watu juu ya matumizi ya nishati safi. Pia, kuimarisha miundombinu na malighafi za nishati safi ya kupikia ili kufikia malengo.
Amebainisha kuwa hatua kubwa imepigwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, takwimu zikionyesha mwaka 2021 asilimia 6.9 ya kaya ndizo zilikuwa zinatumia nishati hiyo, lakini kufikia mwaka 2024 kiwango kilifikia asilimia 20.3.
“Kwa juhudi zinazoendelea, tunaamini ifikapo 2030 tunaweza kufikia kati ya asilimia 75 na 80 ya kaya zitakazokuwa zinatumia nishati safi,” amesema.
Mratibu wa kitaifa wa wanawake kwenye LPG, Winners Lukumay, amesema mahitaji ya gesi ya kupikia nchini yamefikia futi za ujazo 30,000 kwa mwezi, wakati ambao uwezo wa bandari katika kupokea gesi bado ni mdogo.
Amesema hadi sasa bandari inaweza kupokea meli ya gesi yenye futi za ujazo 5,000 pekee kwa wakati mmoja.
“Hii inamaanisha kuwa, meli sita zinapaswa kuingia kwa mwezi ili kukidhi mahitaji kama nchi. Tukiboresha bandari hata gharama za usafirishaji ambazo zinaongeza gharama ya gesi kwa mlaji wa mwisho zitapungua,” amesema.

Mratibu wa Kitaifa wa Wanawake kwenye LPG, Winners Lukumay akizungumza katika Ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Septemba 12, 2025 wakati wa Jukwaa la Nishati Safi ya Kupikia 2025 linaloandaliwa na MCL kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Amesema changamoto nyingine ambayo bado inafifisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kukosekana elimu ya fedha.
Ametoa mfano wa mama lishe ambao hawana shida ya kulipia gesi kwa sababu ni wafanyabiashara wenye uwezo wa kuingiza hadi Sh150,000 kwa siku lakini wanakosa elimu ya fedha, ambayo inamfanya ashindwe kununua gesi kwa wakati mmoja.
“Yuko radhi anunue mkaa wa Sh3,000 kila siku. Tuna programu maalumu ambayo itawezesha mama lishe kununua gesi kidogokidogo,” amesema.
Eneo lingine amesema ni watumiaji wengi kushindwa kupata majiko kulingana na mahitaji yao, kwani yanayogawiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) hayakidhi mahitaji yao, hivyo wanapogawiwa huyaweka pembeni au wanakwenda nayo nyumbani hawayatumii.
“Ni vyema kutengeneza majiko yanayoendana na mahitaji ya watumiaji. Pia, watu wa nyumbani hawana ujuzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia mbali na gharama. Unafuu wake ni vyema kuhamasisha umuhimu wake wa kila siku katika mazingira na afya,” amesema.
Changamoto nyingine iliyotajwa kukwamisha matumizi ya nishati ya kupikia ni ukosefu wa elimu hali inayowafanya wananchi kuendelea kubaki kwenye matumizi ya nishati isiyo salama kiafya.
Akizungumzia hilo, Said Mdungi, Mkurugenzi idara ya nishati na madini, Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, amesema ili kuhakikisha wanaziba pengo la ukosefu wa elimu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia wameanza kutoa elimu kuanzia shule za msingi, kwani ndipo mbegu imara inapoweza kupandikizwa.

“Unapompa ule ujuzi ataenda kushawishi nyumbani, siku mzee wake akipata uwezo itakuwa ni rahisi kupata nishati safi ya kupikia. Pia, mtoto huyu akikua na kuanza kujitegemea si rahisi kuchagua nishati za jadi, bali atatumia nishati safi ya kupikia,” amesema.
Amesema hiyo itasaidia kujenga kizazi cha baadaye ambacho kitakuwa tayari kutumia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa wananchi waliopo mitaani, wamekuwa wakitumia vyombo vya habari na kuwafikia katika maeneo yao kwa kushirikiana na wadau ili kuwaelekeza athari za kutumia njia za kizamani kupika.
“Tumekuja na teknolojia ambazo mwananchi anaweza kutumia fedha kidogo kwa ajili ya kutumia nishati safi ya kupikia kama ambavyo angeweza kutumia fedha hiyo kununua nishati nyingine,” amesema.
Miongoni mwa mikakati inayotekelezwa ili kuongeza matumizi ya nishati safi ni kuhakikisha taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 zinaitumia kupikia.
Mhandisi kutoka Wizara ya Nishati, Anita Ringia amesema moja ya lengo lililowekwa na Serikali ni kuhakikisha zaidi ya taasisi 30,000 zinahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kinachoendelea Mlimani City kongamano la Nisha safi
Hadi sasa zaidi ya taasisi 900 zimeshahama na nyingine zinaendelea kuhama, huku bajeti ikiwa kikwazo.
“Taasisi nyingi zina bajeti ya kila mwezi lakini zinatosha kumudu nishati nyingine tofauti na hii safi, changamoto iliyopo ni katika kuweka miundombinu ya mwanzoni, hivyo uwepo wa mifuko ya kusaidia kampeni hii itafanikisha suala hili,” alisema.
Amesema hadi sasa matumizi ya nishati safi ya kupikia yamefikia asilimia 20.3 ikiwa ni mwendelezo wa safari kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania mwaka 2034.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia amesema kampeni ya nishati safi ya kupikia katika muktadha wa Dira ya Taifa 2050 inalenga kuokoa maisha, kuboresha afya za wanawake na watoto, kulinda misitu na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
Hilo linaweka jukumu kwa watu wote kuhakikisha ifikapo 2034, kaya nane kati ya 10 zinapata nishati safi ya kupikia.
Amesema katika kutambua umuhimu wa nishati safi, MCL imejitolea kuhakikisha ajenda hiyo haiishii leo (jana) tu, bali kupitia magazeti, tovuti, mitandao ya kijamii na ushirikiano na redio zilizopo kote nchini itahakikisha mjadala huo unafika kila kijiji, kaya na kwa kila mtu.
“Tunapanga pia mikusanyiko ya moja kwa moja mashinani ili kushirikisha jamii na tunakaribisha ushirikiano wa kifilantropia na wadau wengine kuhakikisha uendelevu wa ajenda hii,” amesema.
Amewaita wadau kushirikiana kuelimisha, kuhamasisha na kuunda mustakabali bora wa nishati safi na kwa wale waliopo mtandaoni aliwataka kushiriki, kuuliza na kutuma mawazo akieleza jukwaa hilo ni la kila mmoja.
“Ni kweli changamoto ni kubwa, lakini mafanikio yanawezekana. Kwa pamoja tunaweza kujenga Tanzania yenye afya, usalama na ustawi kwa vizazi vijavyo. Safari ni hatua,” amesema.
Amewashukuru wawezeshaji wa Jukwaa la Fikra ambao ni Wizara ya Nishati kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Nishati na Madini–Zanzibar, African Enterprise Challenge Fund (AECF), EWURA, Azania Group, Taifa Gas, NBC Bank, Tanesco, Natkern na Zura.
“Tunatambua pia mashirika na wadau wengine ambao kutokana na changamoto mbalimbali hawakuweza kushiriki nasi leo, lakini mchango wao umesaidia kuunda uzoefu huu wa pamoja. Tunawashukuru nyote,” amesema na kuongeza:
“Tunawaalika kushirikiana nasi ili kupitia majukwaa ya Mwananchi Communications Limited na nguvu ya vyombo vyetu vya habari, uwekezaji wenu uwe na matokeo ya kudumu. Pamoja tunaweza kusukuma mbele ajenda hii na kuibadilisha kuwa kipaumbele cha bajeti za kitaifa, tukihakikisha kila kaya inafikiwa.”