Unayajua mahaba binafsi wewe? Soma hapa! Shabiki mmoja wa Simba ameshtua baada ya kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi akimfuata beki wake mmoja wa zamani.
Shabiki huyo, Shakur Abubakar, ambaye amegoma asipigwe picha akihofia kuchukiwa na wenzake wa Simba, amesema bado haamini kama Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amehamia Yanga.
Shakur amesema ameamua kutinga mwenyewe uwanjani ili kujiridhisha kuwa beki huyo amekimbilia Yanga.
“Kaka mimi siamini unajua nimeona picha tu akili yangu inaniambia kwa teknolojia ya sasa inawezekana kabisa imetengenezwa sio halisi,” amesema Shakur.
“Wenzangu wananiambia amehamia Yanga ila mimi siamini. Unajua wakati akiwa Simba napenda sana kukaa jukwaa la chini na alipokuwa akifunga au kushangilia mabao yetu alikuwa anaonekana ana mahaba makubwa,” amesema Shakur.
“Moyo wangu unaniambia Tshabalala amekaa ndani ya Simba muda wote huu ni kutokana na kuipenda Simba. Sasa nachojiuliza anaweza kweli kutufanyia hivi au wamemuudhi viongozi?
Hata hivyo, Shakur amesema mara atakapomuona Tshabalala kwa uhalisia uwanjani atatoka na anaweza hata kujikuta analia kutokana na anavyompenda nahodha wake huyo wa zamani.
Tshabalala baada ya kumaliza mkataba wake Simba, mara moja Yanga imemsajili ambapo leo ataonekana uwanjani kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki wa timu yake mpya.