MSANII wa singeli kutoka lebo ya WCB, alimaarufu D Voice baada ya kupanda jukwaani kutumbuiza katika tamasha la Wiki ya Mwananchi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, ameamsha shangwe la mashabiki ambao wameonekana kupenda anachofanya.
D Voice alikuwa anaimba wimbo huku akitumia staili ya kuwagandisha mashabiki kisha wanaanza kucheza tena.
Utumbuizaji wake umeamsha shangwe la mashabiki ambao muda wote walikuwa wanashangilia wakati anapafomu na wakati mwingine kuimba naye.
Wakati anaendelea kuimba wachezaji wa Yanga wameingia na kujiunga naye kwa muda mafupi ambapo alianza nahodha Bakari Mwamnyeto akacheza kidogo jambo ambalo limekoleza shagwe la mashabiki.
Kisha akafuatia beki mpya wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyesajiliwa kutoka Simba aliimba kidogo akamalizia kiungo Pacome Zouazoa aliyeingia kati kucheza huku akishangiliwa na mashabiki.
‘Pafomansi’ ya D Voice imewavutia wengi mbali na singeli pia aliimba nyimbo mbili za taratibu za mapenzi ambazo pia zimewakosha mashabiki waliokuwa wanaitikia.
Yanga inahitimisha Wiki ya Mwananchi leo Septemba 12 ikicheza mechi ya kirafiki dhidi Bandari ya Kenya anayokwenda kuichezea Moubarack Amza, raia wa Cameroon msimu uliopita aliyeitumika Kagera Sugar ya Ligi Kuu Bara.