Na Mwamvua Mwinyi, Pwani, Septemba 12, 2025
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imerejesha kiasi cha shilingi 1,376,250 kwa wananchi wa Kitongoji cha Nyakahamba, kata ya Kerege, wilayani Bagamoyo, waliotozwa kinyume cha utaratibu na Mwenyekiti wa Kitongoji kwa ajili ya kulipia huduma ya maji, licha ya kuwa mkandarasi wa mradi tayari alikuwa amelipwa.
Akitoa taarifa kuhusu ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, Domina Mukama, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, alisema urejeshwaji huo wa fedha ni sehemu ya mafanikio ya jitihada za taasisi hiyo katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo.
Kwa mujibu wa Mukama, ufuatiliaji huo ulifanyika katika mradi wa upanuzi wa vituo vya kuchotea maji katika Kitongoji cha Nyakahamba, wenye thamani ya shilingi milioni 60.
“Kazi zilizopaswa kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ulazaji wa mabomba, ufungaji wa ‘fittings’, na ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji.”
Hata hivyo, wananchi walilalamikia kutozwa fedha kinyume cha utaratibu,” alisema Mukama.
Alibainisha, uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa wananchi hawakustahili kulipia huduma ya maji, kwani mkandarasi alikuwa tayari amelipwa gharama zote za kipindi cha majaribio, kabla ya mradi kukabidhiwa kwa RUWASA (Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini), kata ya Mapinga, kwa ajili ya uendeshaji rasmi.
Mukama alisema, fedha hizo zilizorejeshwa zitatumika kusaidia wananchi kulipia huduma ya maji pindi mradi utakapoanza rasmi baada ya kukabidhiwa kwa RUWASA.
Alieleza kuwa, hadi kufikia kipindi hicho TAKUKURU imefuatilia jumla ya sh. bilioni 32.7 zilizotumika katika miradi 40 ya maendeleo kutoka sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, na barabara.
Katika hatua nyingine, Mukama alieleza TAKUKURU Pwani ilipokea jumla ya taarifa 29 za malalamiko kati ya taarifa hizo 16 hazikuhusu vitendo vya rushwa, huku taarifa 13 zikiwa zinahusiana moja kwa moja na vitendo vya rushwa na zinaendelea kushughulikiwa katika hatua za uchunguzi.
Katika upande wa mashtaka alisema kesi mpya 14 zilifunguliwa mahakamani, na kesi 24 zinaendelea kusikilizwa,kati ya kesi 17 zilizotolewa uamuzi, kesi 15 ziliamuliwa kwa upande wa Jamhuri kushinda, huku kesi 2 Jamhuri ikishindwa.