UFAFANUZI KUHUSU WANAODAIWA KUWA WAANDISHI WA HABARI KUSHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOANI ARUSHA

Dar es Salaam, 12 Septemba, 2025

KWA mujibu wa Kifungu cha 13(a) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ina wajibu wa kutoa ithibati na vitambulisho rasmi kwa waandishi wa habari waliokidhi vigezo vya taaluma, sambamba na kusimamia uzingatiaji wa maadili ya uandishi wa habari nchini.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, Bodi imepokea na kufuatilia taarifa zinazozagaa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, zinazodai kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu wawili wanaodaiwa kuwa waandishi wa habari kwa tuhuma za kuendesha televisheni za mtandaoni (Online TV) zisizosajiliwa kisheria.

Bodi inapenda kutoa ufafanuzi rasmi kwamba watu waliotajwa kwa majina ya Ezekiel Mollel (Manara TV) na Baraka Lucas (Jambo TV) SIO waandishi wa habari kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 19(1) cha Sheria hiyo, imeelezwa wazi kuwa:

“Mtu hataruhusiwa kufanya kazi za uandishi wa habari isipokuwa awe amethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.”

Taarifa za Bodi zinaonyesha kuwa watu hao hawajawahi kujisajili katika mfumo rasmi wa usajili wa waandishi wa habari ujulikanao kama TAI HABARI, kwa ajili ya kuomba ithibati na kupata Vitambulisho vya Uandishi wa Habari (Press Cards) vinavyotolewa kisheria.

Hivyo basi, kwa mujibu wa sheria, hawana hadhi ya kisheria ya kutambulika kama waandishi wa habari.

Waandishi wa habari waliokidhi vigezo na kupatiwa ithibati na vitambulisho halali wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa uhuru, heshima na kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya habari. Wale ambao bado hawajakidhi vigezo wanahimizwa kujiendeleza kielimu ili waweze kushiriki ipasavyo katika taaluma hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Bodi inatoa wito kwa vyombo vya habari, wanahabari, na wadau wote wa sekta ya habari kuendelea kushirikiana na Bodi ya Ithibati katika kuhakikisha kuwa sekta ya habari nchini inasimamiwa kitaaluma, kwa kuzingatia:

Maadili ya taaluma ya uandishi wa habari,

Maslahi mapana ya Taifa,

Na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi.