Uhamiaji yaja na siku 28 za kukagua vibali

Arusha. Idara ya Uhamiaji imetangaza siku 28 za ukaguzi na uhakiki wa vibali vya ukaazi na hadhi mbalimbali za kiuhamiaji kwa raia awa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana Septemba 11, 2025 na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, ukaguzi huo utafanyika kuanzia Septemba 11, 2025 hadi Oktoba 8, 2025.

Kupitia taarifa hiyo, msemaji huyo amewataka waajiri na wamiliki wa kampuni kutoa ushirikiano kwa maofisa Uhamiaji watakaoendesha ukaguzi huo.

“Idara ya Uhamiaji inapenda kuwataarifu waajiri, wamiliki wa kampuni na umma kwa ujumla kuwa kutakuwa na zoezi la ukaguzi na uhakiki wa vibali pamoja na hadhi mbalimbali za kiuhamiaji kwa wageni wanaoishi na kufanya kazi nchini.

“Aidha, wageni wenyewe wanaweza kufika ofisi za Uhamiaji Kurasini, Afisi Kuu Zanzibar au ofisi za uhamiaji za mikoa yote nchini wakiwa na pasipoti pamoja na vibali vyao kwa ajili ya uhakiki huo,” amesema msemaji huyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (Tato), Elirehema Maturo, amesema baada ya kuona tangazo hilo jana wameshasambaza kwa kampuni 418 ambazo ni wanachama wake ili wenye changamoto zozote waziwasilishe kwao kwa ajili ya kuwasaidia utatuzi.

“Ukaguzi ni jambo jema na tumeshambaza ujumbe kwa wanachama wetu tangu jana na wote wana taarifa ili mwenye changamoto tumsaidie kuitatua. Tunaomba ukaguzi ufanyike vizuri na usiwe wa kusumbua watu, sisi kama taasisi tunasihi wanachama wetu kuzingatia sheria na taratibu,” amesema.

Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazoingizia taifa kiasi kikubwa cha mapato, ambayo mbali na wageni, imeajiri raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali.

Aidha, baada ya kilio cha wafanyabiashara kuhusu uwepo wa rai wa kigeni wanaofanya bishara ndogondogo nchini Tanzania, idara hiyo iliwakamata raia 7,069 wanaofanya shughuli hizo.

Kwa mujibu wa Uhamiaji, kukamatwa kwa raia hao kulitokana na uchunguzi wa miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili 2025, katika mikoa yote nchini.

Aidha, uchunguzi wa idara hiyo ulitanguliwa na ripoti ya kamati ya kufuatilia na kuhakikisha raia wa kigeni hawajishughulishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa maeneo ya Kariakoo iliyoongozwa na Profesa Edda Lwoga.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika eneo la Kariakoo pekee, maduka 75, yalikutwa na raia wa kigeni 152 walioajiriwa huku asilimia 97 wakijishughulisha na biashara za rejareja.

Taarifa ya kukamatwa kwa raia hao, ilitolewa Aprili 24, 2025 na Msemaji wa Idara hiyo, kuwa kati ya waliokamatwa 1,008 walifikishwa mahakamani, huku 703 wakihukumiwa kifungo gerezani na 257 wakihalalisha ukazi wao.

Taarifa hiyo, ilieleza kuwa wengine 4,796 waliondoshwa nchini na watuhumiwa 305 uchunguzi ulikuwa ukiendelea.

“Idara ya uhamiaji kwa kushirikisna na vyombo vingine vya usalama wamefanya ukaguzi maalumu eneo la Kariakoo ambapo raia wa kigeni 62 walikamatwa kutoka mataifa mbalimbali.

“Waliondoshwa nchini kwa kosa la kuishi na kufanya biashara bila kuwa na vibali, baadhi yao walikiuka masharti yaliyoainishwa katika vibali vyao vya biashara.

“Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa rai awa kigeni kuzingatia matakwa ya masharti ya vibali vyao ili kuepuka hatua za kisheria au usumbufu unaoweza kujitokeza,” ilieleza taarifa hiyo.