Usichojua kuota, kung’oka meno ya watoto

Shinyanga. Kuota meno ni kitendo cha meno kuanza kuchomoza kutoka kwenye fizi za mtoto, na ni hatua muhimu katika ukuaji wa mtoto, ambapo umri wa uotaji hutofautiana kati ya mtoto mmoja na mwingine.

Hata hivyo, kitendo hicho kwa jamii nyingi kimekuwa kikitazamwa kwa sura na imani tofauti ikiwamo hata ile potofu zenye madhara kiafya

Kwa mfano wapo wanaohusisha uotaji na magonjwa kama kuharisha, homa, kutapika, huku wengine wakiamini meno ya awali ya watoto maarufu meno ya maziwa yanapaswa kufukiwa chini ya ardhi, kuchomwa moto au kutupwa baharini.

Ukweli kuhusu meno ya watoto

Daktari wa upasuaji wa afya ya kinywa na meno kutoka Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Dk Paschal Pius, anasema mtoto anaweza kuzaliwa na meno ya awali, hali ijulikanayo kama meno ya kuzaliwa au akaota meno mwezi mmoja baada ya kuzaliwa.

 “Mtoto anapozaliwa na meno au kuota meno mwezi mmoja baada ya kuzaliwa, wazazi wasitafsiri kama ni mkosi ndani ya familia, bali mtoto apelekwe kwa daktari wa kinywa na meno kwa uchunguzi zaidi. Wasiyachokonoe kienyeji au kuyasugulia majivu au kuwapeleka kwa vikongwe, ni kumuumiza mtoto, “anasema.

Anaongeza: “Mtoto anaweza kuwa anang’ata ulimi wake au chuchu za mama na kumsababishia maambukizi, lakini pia haya meno sio imara yanaweza kulegea yakatoka, mtoto akayameza yakamletea shida kwenye mfumo wake wa hewa. Wawalete kwa wataalamu.”

Anasema hali hiyo inatambulika kisayansi na husababishwa na mambo mbalimbali kama lishe, uzito wakati wa kuzaliwa. Watoto wengine huanza kuota meno kati ya miezi 4-7 baada ya kuzaliwa, japo imezoeleka watoto wengi huota meno kuanzia miezi 6 -12 baada ya kuzaliwa.

 “Tafiti zilizofanyika maeneo mengi zinaonyesha kuwa watoto wengi huota meno wakiwa na umri wa miezi sita tangu kuzaliwa, lakini wapo wanaochelewa hadi miezi 12, hivyo mzazi asiwe na wasiwasi,”anasema.

Dk Pius anasema meno yanayoanza kuota ni ya mbele ya chini,   ya katikati ya taya ya chini , ambayo huanza kuonekana kati ya miezi 4-7 baada ya kuzaliwa.

Anasema yanayoanza ni mawili ya chini, yakifuatiwa na meno manne ya juu, na baada ya hapo huanza kuota kwa namna tofauti.

“Miezi 11 meno manne huota, meno manane baada ya miezi 15, meno 12 baada ya miezi 19, na meno 16 baada ya miezi 23, lakini ikitokea utaratibu huo haukufuatwa mzazi/mlezi asipate wasiwasi ni hali ya kawaida,” anasema.

Hata hivyo anaeleza kuwa kuharisha, kutapika na mtoto kupata homa kali sio matokeo ya kuota kwa meno,  bali ni matokeo ya mazingira ya mtoto, kwani katika umri huo mtoto huanza kuokota kila kitu na kuweka mdomoni, hivyo kumsababishia hatari ya kuharisha au kutapika.

Kuota na kung’oka kwa meno ya maziwa

Kuota meno kwa mtoto pia ni mchakato wa kibaiolojia, unaoanza kabla ya mtoto kuzaliwa, wiki ya 6-8 ya mimba, huanza mchakato wa uundwaji wa meno ya maziwa ndani ya mfupa wa taya.

Anasema kuota kwa meno ya maziwa huanzia miezi 4-7 baada ya kuzaliwa,huku wengine wakiendelea mpaka miezi 12, kung’oka kwake huanzia miaka sita, na meno ya kudumu huota kuanzia miaka 6-13, ambapo meno ya mwisho (meno ya hekima) huanza kuota kuanzia miaka 17-25.

Kwa mujibu wa Dk Pius zipo sababu za kisayansi za kuanguka kwa meno ya awali kwa mtoto maarufu pia kwa jina la meno ya maziwa kuanguka na kutoa nafasi kwa meno ya kudumu kuota.

Sababu hizo ni pamoja na uwepo wa meno ya kudumu chini ya meno ya maziwa’ ambapo meno ya kudumu huanza kuundwa ndani ya mfupa wa taya hata kabla ya meno ya maziwa kutoka.

Mizizi ya meno ya maziwa huanza kulegea hatimaye hubaki bila mzizi na kuanguka. Sababu ya pili anasema ni mabadiliko ya taya na uso.

‘’ Kadri mtoto anavyokua, taya huongezeka ukubwa ili kutoa nafasi kwa meno makubwa ya kudumu. Meno ya maziwa ni madogo na hayatoshi kwa taya ya mtu mzima hivyo huondolewa kwa mpangilio wa asili,’’ anaeleza.

Sababu nyingine ni homoni na seli zinazoitwa ‘odontoclast’ kuchochea kuvunjika kwa mizizi ya meno ya maziwa. Aidha, homoni za ukuaji kama Growth hormones (GH), na Thyroid hormones (TH), nazo huchangia ukuaji wa taya na meno mapya.

‘’Sababu nyingine ni mpangilio wa kijenetiki. Vinasaba huamua wakati wa kuota na kung’oka kwa meno. Mchakato huo ni wa kurithi na hufanyika kwa mpangilio maalumu unaoendana na umri wa mtoto.

Dk Pius anaeleza kuwa hakuna hitaji la lazima la kutunza meno ya maziwa baada ya kung’oka japo baadhi ya wazazi huchagua kuyatunza kama kumbukumbu ya utoto wa mtoto.

Anasema hakuna madhara ya kiafya yanayotokana na kutupwa au kutunzwa meno ya maziwa, kwani hilo  ni suala la uchaguzi binafsi.