Wadau wataka mabadiliko ya sheria wanaojaribu kujiua

Dodoma. Wakati wataalamu wa afya ya akili na wanasheria wakishauri kufanyika marekebisho ya sheria ili wanaojaribu kujiua wapewa tiba  saikolojia, badala ya kukabiliwa na mashtaka, baadhi ya waliofikwa na kadhia hiyo wameeleza wanayopitia.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu mtu yeyote anayejaribu kujiua ana hatia ya kosa.

Akizungumza Septemba 10, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzuia kujiua duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mirembe, Dk Paul Lawala alishauri kufanyika marekebisho ya sheria akieleza kosa hilo siyo la jinai bali ni matatizo ya afya ya akili yanayohitaji tiba.

Takwimu zilizokusanywa na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi zinaonyesha vifo vinavyotokana na kujiua nchini kuanzia Januari mwaka 2024 hadi Juni mwaka 2025 ni 1,141, huku wanaume wakiongoza kwa asilimia kubwa.

Takwimu hizo katika kipindi cha miezi 18 zinaonyesha watu 162 walijiua kwa kunywa sumu, 960 walijinyonga, 13 walijichoma kisu na sita walijipiga risasi.

Akizungumza na Mwananchi Septemba 11, 2025, wakili Dk Rugemeleza Nshala alisema sheria iliyopo ina upungufu, hivyo inafaa kurekebishwa, hasa katika wakati huu ambao tatizo la changamoto ya afya ya akili linaongezeka miongoni mwa jamii.

Dk Nshala alisema Serikali ina wajibu wa kuimarisha vitengo vya afya ya akili ili kuweka kinga ya jamii na kuwatibu waathirika wa afya ya akili mapema kabla hawajafikia hatua ya kujiua.

“Hata ukimpeleka gerezani itasaidia nini? Huyu mtu amejaribu kujiua kutokana na changamoto aliyopitia,” alisema Nshala.

Alisema Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inalinda haki ya kuishi ya kila raia.

“Walichosema wataalamu kama jamii pamoja na Serikali tuna jukumu kusaidia jamii kuendelea kuishi. Waliokata tamaa sababu ya madeni, uhusiano, masononeko inachangia kupata changamoto ya afya ya akili, akifikia hatua hiyo asaidiwe na si mashtaka,” alisema.

Mkazi wa Mtaa wa Image, Kata ya Kilimani, jijini Dodoma, Joyce Chigunda (43) anasimulia alivyonusurika kufa baada ya kunywa dawa nyingi mchanganyiko, baada ya mama mkwe wake kukataa asiolewe na mwanaye.

Akizungumza na Mwananchi Septemba 11, Joyce alisema alifikia uamuzi huo ili kuepuka aibu ya kuzaa akiwa nyumbani kwao kabla ya ndoa, kwa kuwa wakati huo alikuwa na ujauzito wa miezi minane.

Alisema yeye na mchumba wake hawakuwa na shida, bali ilijitokeza baada ya mama mkwe kuwa amemchagulia mchumba wa kumuoa kijana wake, hivyo alikataa Joyce asiolewe.

“Tatizo lilikuwa kwa mama yake, kijana alikuja kwetu akalipa mahari bila kumshirikisha mama yake. Alipojua alikuja nyumbani kwetu akasema hataki mwanaye anioe, nikajua hapa hakuna ndoa,” alisema Joyce na kuongeza:

“Ili kukwepa aibu ya kuzalia nyumbani bila ndoa niliamua kujiua kwa kumeza dawa nyingi nikaenda kulala, baada ya muda nilianza kuhisi kichefuchefu, hivyo nikaenda chooni kutapika. Namshukuru Mungu dawa zote zilitoka sijawahi kujaribu tena kujiua maishani mwangu.”

Joyce alisema alijifungua salama na binti yake kwa sasa yupo chuo kikuu anaendelea na masomo. Alieleza hakuolewa na baba wa mtoto wake lakini aliolewa na mwanamume mwingine.

Mkazi mwingine wa Mtaa wa Kisasa, Kata ya Dodoma Makuru, Yakobo Stanel aliyezaliwa mwaka 1994 anasimulia alijaribu kujiua mara kadhaa kutokana na changamoto zilizokuwa zikimkabili.

Anasema mara ya kwanza alisaga betri za redio na kunywa unga wake baada ya kutoelewana na baba yake. Anaeleza wanafamilia walimuwahi na akapatiwa huduma akanusurika kifo.

Stanel anasema hali ya kutaka kujiua humjia mara kwa mara akihisi sauti za watu ambao hawaonekani zikimsemesha kumtaka ajiue.

“Nahisi nina changamoto ya akili kwa sababu kuna wakati nakuwa mzima, lakini nyakati zingine nasikia sauti za watu ambao siwaoni wanaotaka nijiue ni stori ndefu lakini kifupi ni hivyo,” anasimulia.

Mbali na hao, zipo familia zilizopoteza wapendwa wao waliojiua kama anavyoeleza Charles Leshami. Anasema familia yao ilipata pigo la kufiwa na mama yao waliyemkuta shambani amejinyonga kwa kutumia kanga.

Leshami anasema siku hiyo mama yao aliamka asubuhi na mapema kwenda shambani, baadaye walipata taarifa amejinyonga kwa kutumia kanga.

“Baadaye tulipata taarifa kuwa walikuwa na mgogoro na baba kuhusu kupotea kwa pesa ndani ya nyumba. Baba alimtuhumu mama kuwa ameiba fedha hizo, lakini baadaye zilipatikana kwenye shimo la panya na wakati huo mama alikuwa tayari amefariki dunia,” anasema.

Anasema msiba huo ulikuwa pigo kwa familia, kwani ulitokea ghafla na hakuna aliyejua kama kulikuwa na upotevu wa fedha ndani, akieleza wangejua wangemsaidia kulipa ili asijidhuru.

Akilizungumzia hilo, Daktari bingwa wa afya na magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Mirembe, Veronica Lyimo anasema zipo sababu nyingi za watu kujitoa uhai ikiwamo sonona, kiwewe, ulevi kupindukia, matumizi ya dawa za kulevya na magonjwa sugu.

Anasema kuna vitu ambavyo mtu anaweza kupitia mpaka akafikiria kujiua, inaweza kuwa jambo moja kubwa au mengi ambayo yameambatana na kumpa fikra za kujiua zinazosababishwa na sababu za kibaiolojia, saikolojia na kijamii.

Upande wa kibaiolojia anasema kuna umri mtu akifika anaweza kuongeza hatari ya kufikia mawazo au fikra za kutaka kujiua kwa kuwa uwezo wa ubongo wa kutafakari au kufanya uamuzi unakuwa bado haujapevuka kwa asilimia 100 hasa vijana.

“Lakini pia anaweza kuwa anapitia vitu fulani ambavyo vikaharibu ubongo wake kwa namna fulani na kuongeza hatari au kuwa na mawazo ya kutaka kujiua,” anasema.

Dk Lyimo anasema kisaikolojia kuna wale ambao wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili au kingono na kumsababishia mwathirika kuanza kuwaza maisha hayana thamani na kufikiria kujiua.

Anasema watu wanaopitia msongo wa mawazo kwa muda mrefu pia huweza kufikiria kujiua.

“Kwa upande wa kijamii mambo ni mengi hasa kwa wale ambao wana uwezo wa kumiliki silaha akipata mawazo ya kujiua anaweza kujitoa uhai wake papo hapo. Miongoni mwa hayo ni kutokuwa na kazi, kufiwa na wapendwa na kupitia jambo gumu ambalo hujawahi kulipitia,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo, siyo sababu moja inayoweza ni muunganiko wa nyingi kwa pamoja zinaweza zikaleta hiyo hali.”

Anataja viashiria vya mtu kutaka kujiua kuwa ni kuongelea sana kuhusu kujiua na vitu vinavyoonyesha hali hasi, kama vile kukosa furaha na kila jambo analoliongelea kuwa la huzuni.

Pia mtu kuonyesha hajipendi au kufanya vitu ambavyo vinamweka kwenye hatari ya kupoteza maisha kama vile kuendesha vibaya ili mradi mwisho wa siku afanikishe kile ambacho anakifikiria.

“Wengine ni wepesi wa hasira, wanajitenga na watu wengine, anaweza akaandika kabisa urithi au akaandika barua kwamba nimeshashindwa maisha au akakosa furaha, kwa hiyo vitu vingi vinaweza vikajumuisha, lakini wakipata msaada wanaweza kusaidika na kuondokana na hali hiyo anayopitia,” anasema.

Dk Lyimo anasema kuna upungufu wa wataalamu na wauguzi wa kutoa huduma ya afya ya akili, hivyo upo umuhimu wa kuwaongeza pamoja na vituo vya huduma ili wanaopata changamoto waanzie ngazi ya chini.

Kwa kufanya hivyo anasema Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe iwe ni rufaa kwa wagonjwa hao.

Anasema hata vituo vilivyopo, zikiwamo hospitali za rufaa za mikoa hazitoi huduma zenye ufanisi kwa kukosa wataalamu wa afya ya akili.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ilibainisha upungufu katika maeneo 12 ya utoaji huduma kwa jamii, ikiwamo ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya afya ya akili.

Katika ripoti ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili, CAG alieleza kuwapo ongezeka la wagonjwa na vifo.

Alieleza vituo vingi havipati huduma za utengamo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa kupona na kwamba, kati ya mikoa 28, ni mitano pekee yenye vituo vya utengamo vya huduma za afya ya akili.

Wizara ya afya baada ya ripoti hiyo ilisema afya ya akili ni eneo nyeti ambalo linafanyiwa kazi kuhakikisha mifumo inaimarishwa ya watu kupata huduma stahiki.