Wiki ya Wananchi, kishindo cha vaibu

KILELE cha wiki ya Mwananchi kimehitimishwa kwa kishindo, huku kila shabiki akitoka meno nje akitamba mambo freshi na msimu mpya uanze.

Yanga ilifanya tamasha hilo leo ambapo kilele chake kilikuwa palepale Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na mashabiki wa klabu hiyo kufurika kwa wingi.

*Vinywaji kibao*
Mapema tu ilikuwa mashabiki wakiwa wanaingia uwanjani, walikutana na zuio la kutoingia na chupa yoyote ya kinywaji uwanjani na zote ziliishia kwenye mageti nje.
Hata hivyo, kumbe ndani mashabiki hao wakakutana na mambo mazuri wakipewa vinywaji baridi na maji bure vilivyotengenezwa na mfadhili wa klabu hiyo GSM.

*Hakuna vurugu*
Hatua zote za kuingia uwanjani kwa mashabiki hakukuwa na vurugu zozote ambapo watu wa usalama walisimamia vizuri makundi ya mashabiki hao.

*Burudani za kutosha*
Ndani ya Uwanja kulikuwa na burudani za kutosha kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Dully Sykes, Meja Kunta, Kontawa, Dogo Patern, mchekeshaji Leonardo, D Voice na Zuchu.

*D Voice, Zuchu shoo kali*
Kama Kuna wasanii waliutikisa umati huo walikuwa D Voice ambaye aliuteka umati huo na shoo zake kali za muziki akiungana na msanii mkubwa wa tamasha hilo, Zuchu ambaye alitoa burudani kwa dakika 47.

D Voice aliwaamsha mashabiki jukwaani alipomchezesha singeli beki mpya wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wakati akiingia na wenzake kwa mara ya kwanza wakitaka kuwasalimia mashabiki wa timu hiyo kama kawaida yao.

Mbali na wasanii hao pia Madj Mamie na Ally B walitoa burudani kubwa iliyowakosha mashabiki hao wakicheza majukwaani huku wakishangilia.

*Manara kama kawa*
Wakati linaanza tukio la utambulisho wa wachezaji ghafla uwanja ukampokea Haji Manara na kuibua shangwe kubwa.

Manara kama kawaida yake aliliteka tukio hilo akiwataja kwa mambo mbalimbali wachezaji, huku utambulisho uliowateka wengi ni ule wa Tshabalala ambaye ametua Yanga akitokea Simba na Clement Mzize, Lassine Kouma alipompa kazi kipa wa timu hiyo Djigui Diara kumtambulisha, Pacome Zouzoua ambaye akimfuata ndani na kutoka naye kisha kumfunga kamba za viatu.

*Hati ya eneo la uwanja*
Tukio lingine kubwa lilikuwa ni uongozi wa Yanga kukabidhiwa rasmi hati ya ongezeko la eneo pale jangwani.

Itakumbukwa wiki iliyopita, Waziri wa ardhi Deogratius Ndejembi ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo, wakati wa mkutano wa Yanga akiongea kwa simu moja kwa moja aliwaambia wanachama wa mkutano mkuu wa klabu hiyo kuwa maombi yao yanafanyiwa kazi na ndani ya wiki mbili watakabidhiwa hati hiyo.

Hata hivyo, hata kabla ya muda huo kufika, Ndejembi leo akaukabidhi uongozi wa klabu hiyo, hati hiyo kisha akitaka kuona hatua za ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo zinaanza mara moja.

Yanga hapo hapo bila kuchelewa Rais wa klabu, Injinia Hersi Said akamtambulisha GSM kuwa ndiye atakuwa mwekezaji wa ujenzi wa uwanja huo.

*Rais Samia atuma salamu*
Wakati viongozi wa Yanga wakiwa mbele ya mashabiki wao, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa akapiga simu kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kama ilivyokuwa kwenye tamasha la Simba Day, akiwatakia kila la kheri katika kilele cha tamasha hilo.

Yanga ikawajibu Simba kwa kuujaza uwanja huo ambapo ilipofika saa 10:46 jioni tayari  ulikuwa umeshajaa majukwaa yote.

Baada ya kujaa uwanjani Yanga ikaweka televisheni eneo la geti la kuelekea Chuo cha Elimu (DUCE) ili mashabiki wengine waliokosa nafasi, kuangalia matukio yote wakiwa kwenye luninga hiyo

Burudani kubwa iliyofunga tamasha hilo ilikuwa mechi kati ya Yanga dhidi ya Bandari ya Kenya ambapo kocha wa wenyeji Romain Folz kukigawanya kikosi chake kwenye vikosi viwili.

Kikosi cha kwanza kilikuwa na kipa Djigui Diara, Israel Mwenda, Bakari Mwamnyeto, Frank Assinki, Aziz Andambwile, Maxi Nzengeli, Lassine Kouma, Celestin Ecua, Farid Mussa, Shekhan Abdallah, Prince Dube.

Katika kikosi hicho kilichocheza kwa dakika 45 za kwanza kilionyesha soka la pasi za haraka,huku pia kukaba kwa nguvu na kuwaweka Bandari kwenye wakati mgumu.

Ilikuwa dakika ya pili tu Yanga ikatangulia kupata bao mfungaji akiwa Ecua alimalizia kwa kichwa krosi ya Dube.

Ecua alionyesha kiwango kizuri sambamba na Kouma, ambao walitawala na kushangiliwa dakika hizo 45 za kwanza ambazo zilimalizika kwa Yanga kuongoza kwa bao 1-0 huku pia wakiutawala vizuri mchezo.

Kipindi cha pili Folz alibadilisha kikosi chake akiwarudisha Mwamnyeto na Assinki pekee timu ikiwa na kipa Aboutwalib Mshery, Mwamnyeto, Assinki, Kibwana, Shadrack Boka, Duke Abuya, Salum Abubakar Sure Boy, Offen Chikola, Mamadou Doumbia, Edmund John, Denis Nkane.

Katika timu hiyo iliyocheza kwa dakika 25 pekee alikuwa Doumbia ambaye alikuwa kivutio kwa pasi zake za kuachia haraka na kasi.

Dakika ya 70 Folz akafanya mabadiliko mengine sita yaani akibadili nusu ya kikosi hicho akiwatoa Assinki, Mwamnyeto na Boka kwenye ukuta wakiingia Tshabalala, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’.

Pia akawatoa Sure Boy, Abuya na Nkane nafasi zao wakiingia Mudathir Yahya, Moussa Bala Conte na Andy Boyeli mabadiliko ambayo yaliishangiliwa na mashabiki majukwaani.