Wenyeji wa mchezo Yanga Princess wameshindwa kutambiana na Mashujaa Princess kwenye mchezo wa ufunguzi wa kilele cha tamasha la Wiki ya Wananchi baada ya suluhu katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mchezo huo umechezwa kwa dakika 40 ikiwa ni 20 kila kipindi na hakuna timu iliyotikisa nyavu, huku Yanga ambayo imeanza kwa utambulisho wa wachezaji wake wa msimu huu imepiga kona tatu pekee ambazo hazikuwa na madhara kwa wapinzani.
Mchezo umeanza kwa Mashujaa kuonyesha kuhitaji matokeo kipindi cha kwanza ambapo imepata nafasi ya kupeleka mashambulizi langoni mwa Yanga Princess, lakini umakini wa safu ya ulinzi uliwanyima nafasi ya kupata bao wala kona kwenye dakika zote 40.
Kipindi cha kwanza Mashujaa walionyesha uhai eneo la kiungo na safu ya ulinzi wakitawala mchezo na kumlazimisha kocha wa Yanga Princess, Edna Lema kufanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuingiza sura mpya.
Licha ya mabadiliko hayo, Yanga Princess imeishia kutawala mchezo kwa kupasiana pasi ikionana, lakini haijapata mwanya wa kukwamisha mpira wavuni hadi mwamuzi alipopuliza kipyenga kuashiria dakika 40 za mchezo kumalizika.