Albania yateua waziri roboti wa kupambana na ufisadi

Tirana. Albania imeweka rekodi ya dunia kwa kuwa nchi ya kwanza kuteua waziri aliyeundwa kwa akili bandia (AI), siyo waziri wa teknolojia ya AI, bali waziri halisi wa kidijitali, aliyeundwa kwa misimbo na kuendeshwa na mfumo wa kisasa wa akili bandia.

Jina lake ni Diella, linalomaanisha ‘mwanga wa jua’ kwa Kialbania ndilo jina la roboti, atasimamia shughuli zote za manunuzi ya umma, kama alivyoeleza Waziri Mkuu Edi Rama.

Aliteuliwa rasmi Alhamisi ya Septemba 11, 2025, ambapo Rama alimtambulisha kama ‘mwanachama wa baraza la mawaziri asiye na uwepo wa kimwili’, ambaye atahakikisha kuwa zabuni za umma zitakuwa huru kwa asilimia 100 dhidi ya ufisadi.

Wakati wa majira ya kiangazi, Rama alidokeza kuwa siku moja Albania inaweza kuwa na waziri wa kidijitali  hata Waziri Mkuu wa AI,  lakini ni wachache waliotarajia hatua hiyo itachukuliwa haraka kiasi hiki.

Kwenye mkutano wa Chama cha Kijamaa uliofanyika katika mji wa Tirana, Rama alitangaza mawaziri waliobaki na waliokatwa, alimtambulisha pia Diella  mwanachama pekee wa Serikali asiye binadamu.

“Diella ni mwanachama wa kwanza wa baraza la mawaziri asiye na uwepo wa kimwili, bali aliyeundwa kwa akili bandia,” aliwaambia wanachama wa chama hicho.

Rama alisema uamuzi kuhusu zabuni utahamishwa kutoka wizara mbalimbali na kuwekwa mikononi mwa Diella, ambaye sasa atakuwa mtumishi wa manunuzi ya umma.

Alibainisha kuwa mchakato huo utaanza hatua kwa hatua, lakini Albania itakuwa nchi ya kwanza ambapo zabuni za umma zitakuwa asilimia 100 huru dhidi ya ufisadi, na kila senti ya fedha za umma itakayopitia mfumo huo itakuwa inayosomeka na inayodhibitiwa kikamilifu.

“Hii si hadithi ya kubuni  ni jukumu halali la Diella,” aliongeza Rama.

Amesema Diella tayari anawafahamu wananchi wa Albania kupitia jukwaa la e-Albania, ambapo amekuwa akitoa huduma karibu zote za Serikali kwa njia ya kidijitali.

Pia, ana avatar, anayejitambulisha kama mwanamke kijana aliyevaa vazi la jadi la Albania.

Majukumu ya Diella yatakuwa pamoja na kuchambua zabuni, na atakuwa na uwezo wa kuajiri vipaji kutoka kote duniani, lengo likiwa ni kuondoa upendeleo na urasimu unaozuia ufanisi katika utawala wa umma.

Kwa miaka mingi, Albania imekuwa ikikabiliwa na tatizo sugu la rushwa, hasa katika utawala wa umma na michakato ya zabuni. Masuala haya yamekuwa yakitajwa mara kwa mara kwenye taarifa za kila mwaka za Umoja wa Ulaya kuhusu utawala wa sheria.

Kwa muda mrefu, utoaji wa zabuni umekuwa chanzo kikuu cha ufisadi katika taifa hilo lenye idadi ya watu takribani milioni 2.8, ambalo lina ndoto ya kujiunga na Umoja wa Ulaya (EU).

Ufisadi umebainishwa kuwa ni mojawapo ya changamoto kubwa katika safari ya Albania kuelekea uanachama wa EU.

Bado haijafahamika iwapo waziri mkuu huyo atawasilisha uteuzi wa Diella kwenye Bunge kupigiwa kura, licha ya wabunge hivi karibuni kutarajiwa kulipigia kura baraza lake jipya la mawaziri.

Wataalamu wa sheria wanasema bado kuna kazi ya ziada ya kisheria inayohitajika ili kubaini hadhi rasmi ya Diella, ambaye kwenye skrini huwasilishwa kama mwanamke aliyevaa vazi la kitamaduni la Kialbania.

Gazmend Bardhi, kiongozi wa wabunge wa chama cha Demokrasia, amekosoa uteuzi huo akisema hadhi ya uwaziri kwa Diella ni kinyume cha katiba.

“Upuuzi wa Waziri Mkuu hauwezi kugeuka kuwa sheria ya Taifa la Albania,” aliandika Bardhi kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Waziri Mkuu Rama hakutoa maelezo kuhusu mfumo wa usimamizi wa kibinadamu juu ya Diella, wala hatari ya AI kudukuliwa au kuchezewa, ambayo ni hoja kuu ya ukosoaji wa hatua hiyo.

Diella alizinduliwa mapema mwaka huu kama msaidizi wa mtandaoni kupitia jukwaa la huduma za umma la e-Albania, ambapo amekuwa akiwasaidia watumiaji kutafuta huduma mbalimbali na kufikia takribani nyaraka milioni moja za kidijitali.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa hadi sasa, Diella amesaidia kutolewa kwa nyaraka 36,600 za kidijitali, pamoja na kutoa huduma 1,000 tofauti kupitia jukwaa hilo.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.