Askofu Sosthenes azikana nyaraka kesi ya Askofu Sepeku

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes amezikana nyaraka za ofisi yake zilizotolewa na watangulizi wake kuhusu uamuzi wa kumzawadia shamba na nyumba Askofu mwanzilishi wa dayosisi hiyo na kanisa hilo nchini, hayati John Sepeku.

Wakati watangulizi wake katika ushahidi wao na nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo wakibainisha zawadi ilitolewa kwa kuzingatia taratibu zote kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo, Askofu Sosthenes amepingana nao akisema waliotoa zawadi hiyo hawakuwa na mamlaka.

Askofu Sosthenes ametoa msimamo huo, akihojiwa na mawakili wa upande wa madai katika kesi inayosikilizwa na Jaji Arafa Msafiri, kwenye Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, kuhusu maelezo ya ushahidi wake wa maandishi aliouwasilisha mahakamani juzi.

Kesi hiyo imefunguliwa na Bernado Sepeku, mtoto wa Askofu Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Bernado ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yao anapinga uamuzi wa dayosisi hiyo chini ya uongozi wa Askofu Sosthenes kuwanyang’anya zawadi ya shamba alilopewa baba yao, na kumgawia mwekezaji, Kampuni ya Xinrong.

Anaiomba mahakama iamuru alipwe fidia ya Sh3.72 bilioni anayodai ni thamani ya shamba hilo kwa sasa, pamoja na Sh493.65 milioni kama fidia ya hasara ya mazao yaliyoharibiwa katika shamba hilo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi hiyo zilizoko mahakamani, Desemba 8, 1978, Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo, Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao ilipendekeza kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi ekari 20 na nyumba katika kutambua utumishi wake.

Sinodi ya dayosisi hiyo katika kikao cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia pendekezo hilo na iliazimia kumpatia Askofu Sepeku, shamba la ekari 20 lililoko Buza, wilayani Temeke na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Hata hivyo, baadaye uongozi wa sasa wa dayosisi uliligawa shamba hilo kwa mwekezaji, Kampuni ya Xinrong, ambaye alifyeka mazao yaliyokuwa yamelimwa, kisha akajenga kiwanda na nyumba yenye thamani ya Sh165 milioni.

Askofu Sosthenes ambaye ni shahidi wa tano wa utetezi, baada ya maelezo ya ushahidi wake wa maandishi kupokewa mahakamani, alihojiwa maswali ya dodoso na jopo la mawakili wa mdai, Deogratius Butawantemi, Gwamaka Sekela na Eric Amon.

Akihojiwa na wakili Sekela, Askofu Sosthenes amedai vikao vya mamlaka zinazodaiwa kupendekeza na kumpa Askofu Sepeku shamba hilo, Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, hazina mamlaka ya kugawa mali ya kanisa.

Amedai dayosisi hiyo haina mamlaka ya kutoa zawadi au mali yoyote, kwani siyo mmiliki wa mali bali Bodi ya Wadhamini ndiye mmiliki na msimamizi wa mali hizo. Amedai ndiyo yenye mamlaka ya kuamua na kuzigawa mali hizo.

Shahidi huyo amedai hajawahi kuona kumbukumbu za kikao cha wadhamini kilichopendekeza na kupitisha uamuzi wa kumpa zawadi Askofu Sepeku.

Akihojiwa na wakili Butawantemi, kuhusu ushahidi wa mtangulizi wake, Askofu mstaafu Dk Valentino Mokiwa, kuwa kumbukumbu zilizoko ofisini hapo ni kuwa Askofu Sepeku alipewa zawadi hiyo kihalali, Askofu Sosthenes alidai hakumbuki kuwapo kumbukumbu hizo ofisini hapo.

Alipoonyeshwa taarifa ya ugawaji kipande cha ardhi cha ekari tano katika shamba hilo lenye mgogoro kwa Manispaa ya Temeke, kwa ajili ya ujenzi wa stendi, Askofu Sosthenes amekiri imetoka ofisi yake na kwamba, saini iliyopo ni yake.

Hata hivyo, alipotakiwa kuitoa mahakamani kama kielelezo amedai haihusiani na kesi hiyo. Mahakama haikuipokea, lakini wakili Butawantemi akamtaka asome aya ya mwisho ya taarifa hiyo naye akaisoma.

Aya hiyo inaeleza uamuzi wa kuipatia Manispaa ya Temeke eneo hilo uliofanywa na Halmashauri ya Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kisha uamuzi ulipelekwa kwa Bodi ya Wadhamini kwa ajili ya kutoa kipande hicho kwa manispaa.

Alipoulizwa tofauti ya utaratibu kati ya alioutumia yeye kuigawia Manispaa ya Temeke eneo hilo na ule uliotumika kumpatia zawadi Askofu Sepeku, shahidi Askofu Sosthenes amedai hajawahi kuona nyaraka iliyopelekwa kwa Bodi ya Wadhamini kujadili na kuamua kumpatia Askofu Sepeku zawadi hiyo.

Pia amekana kuwapo mawasiliano baina ya watoto wa Askofu Sepeku na Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhusu mchakato wa familia kupata hatimiliki ya eneo hilo alilopewa zawadi baba yao.

Wakili Butawantemi alimuonyesha Askofu Sosthenes barua ya Januari 7, 1999 na ya Januari 15, 1999 za Dayosisi ya Dar es Salaam kwenda kwa familia ya Askofu Sepeku.

Barua hizo zinaielekeza na kusisitiza familia hiyo ishughulikie upatikanaji wa hatimiliki ya shamba hilo walilopewa zawadi pamoja na nyumba iliyoko Buguruni, ili kuepusha matatizo kati ya Serikali na dayosisi ikieleza kuwa Serikali inaweza kulichukua shamba hilo.

“Mimi siifahamu ndiyo naiona hapa lakini pia naikataa kwa sababu aliyeandika, Katibu hana mamlaka ya kufanya alichokifanya,” amedai.

Miongoni mwa mashahidi wa upande wa madai ni maaskofu, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa kanisa hilo na Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo mstaafu, Dk Valentino Mokiwa. 

Mashahidi hao walikiri kutambua, kuona na kushiriki vikao vilivyoridhia na kupitisha pendekezo la kumpa zawadi Askofu Sepeku, wakisema Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam ina mamlaka ya kufanya hivyo.

Maaskofu hao walifafanua kuwa Sinodi ni Mkutano Mtakatifu wa Juu unaowahusisha Askofu wa Dayosisi, mapadri na waumini kwa ajili ya kufanya uamuzi wa kanisa na kwamba, uamuzi wake hauwezi kupingwa popote wala kutenguliwa na mtu yeyote.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Oktoba 13, 2025, ambayo mawakili wa utetezi wataendelea kumhoji maswali ya dodoso Askofu Sosthenes.