Bado Watatu – 27 | Mwanaspoti

Raisa alinieleza: moyo wangu ulikuwa unakwenda kasi kama saa! Nilikuwa nimemtolea macho nikimsikiliza. Sikuwa hata na la kupinga, kwani ukweli ukidhihiri uongo hujitenga.
Raisa alipoona nipo kimya aliendelea kuniambia:
“Sasa, mwenzangu, nawasha kitochi ili niione: kuna mtu alikorupuka na kuingia kwenye gari, akarudi nyuma na kuondoka. Haya niambie — ulikwenda kutupa nini usiku ule? Hata huogopi!”
Kumbe — hukuona nilichokitupa au unaniuliza tu? Nitasema nini? Nikajisemea kimoyomoyo.
Kwanza nilijidai kuguna, kama vile hilo jambo alilonieleza nilikuwa silijui. Nilijua kuwa nitajiingia kusema ni mimi, moja kwa moja nitahusika na kifo cha Shefa. Nitaonekana nimemuua mimi kisha nikaenda kumtupa makaburini.
“Mbona, shoga, jana sijatoka. Nilikuwa hapa nyumbani,” nikamwambia huku nikijaribu kuifanya sauti yangu kuwa tulivu, isiyo na taharuki.
“Hujatoka! Mbona niliona mtu kama wewe?”
“Siye mimi. Binadamu tunafanana tu.”
“Kwani kuna mtu ulimuazima gari lako jana?”
Nilitaka nikubali kuwa nilimuua mtu, lakini nilijiuliza: nitakapokuja kuulizwa nilimuazima nani nitajibu nini? Nikaona nikatae.
“Sijamwazima mtu. Hilo gari naliendesha mwenyewe tu, na tangu jana sijatoka nalo. Nitoke niende wapi, shoga?”
“Mmh…! Basi mimi nilidhani ni wewe; ndio maana nilikufuata. Kumbe siye!”
“Hicho kitu alichokitupa huyo mtu kilikuwa kitu gani?” nikamuuliza ili nijue kama ameugundua mwili wa Shefa.
“Sijakiona. Mahali palikuwa na giza. Nilipoona mtu mwenyewe anakimbia nikaondoka. Nafikiri bodaboda wangu alizisoma namba za lile gari, nitakwenda kumuuliza.”
“Si uliache tu, shoga? Pengine mtu amekwenda kutupa makafara yake makaburini, utajuaje?”
“Inawezekana. Hata mimi kuna siku niliambiwa na mganga nikazike kitu kwenye kaburi, nikashindwa.”
Nikajidai kucheka lakini sikuweza. Uso wangu ulikuwa umekakamaa wala haukutaka kukunjuka kutokana na hofu na fadhaa niliyokuwa nayo.
“Kwenda makaburini usiku kunataka moyo sana. Maiti ikikufufukia utafanyaje?” nikamwambia Raisa kwa lengo la kuigeuza ile mada ya awali.
“Hapo sasa! Mimi nilishindwa lakini wapo wanaoweza.”
“Wapo. Unajua kila mtu ana moyo wake. Kama kuna mtu anaiba nywele za maiti, atashindwa kwenda kaburini usiku?” nikamuuliza kisha nikajijibu mwenyewe.
“Hawezi kushindwa.”
“Unajua, shoga, kilichonileta kwako asubuhi hii ni hilo tukio la jana; nilidhani ni wewe. Kama hukuwa wewe basi naenda zangu.”
“Si ungenipigia simu tu ukaniuliza, mpaka usumbuke mwenzangu?”
“Kuna mambo mengine si ya kuongea kwenye simu. Ilibidi nikufuate mwenyewe nikuulize.”
“Basi nashukuru, shoga, kwa kunitembelea. Mwenyewe hata sijapika chai.”
“Nimeshakunywa huko kwangu; wewe kaa na uvivu wako.”
Raisa akainuka huku akicheka baada ya kuniambia nikae na uvivu wangu. Mimi nikajidai kucheka uongo. Nilimsindikiza kwenye mlango kisha nikaagana naye; akaenda zake.
Moyo wangu kidogo ulitulia baada ya kumdanganya kwamba sikuwa mimi aliyeniona.
Lakini ilipofika saa sita mchana niliona taarifa ya polisi kwenye televisheni yetu ya Tanga. Taarifa hiyo ilieleza kuwa kulikutwa maiti iliyotupwa kwenye eneo la makaburi ya Msambweni. Baada ya ripoti kutolewa na polisi kufika eneo hilo, walibaini maiti hiyo ilikuwa ya mtu anayetafutwa na polisi, anayetambulika kama Shefa Mohamed. Polisi waligundua ni Shefa kutokana na leseni yake iliyokutwa mfukoni mwa suruali yake.
Taarifa iliwataka ndugu na jamaa zake kufika kituo cha polisi cha Chumbageni kwa maelezo zaidi na ilisema polisi walikuwa bado wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Taarifa hiyo ya polisi ilinishtua sana. Kwanza, nilishtuka kwa kujua Shefa alikuwa ameshagunduliwa. Pili, nilishtuka kwa sababu polisi pamoja na jamaa zake walijua Shefa ameuawa na kutupwa kwenye eneo la makaburi. Tatu, nilishtuka kwa sababu nilijua Raisa akiipata taarifa hiyo mara moja atanishuku mimi kuhusiana na mauaji ya Shefa. Japokuwa nilimwambia sikuwa mimi aliyeniona kule makaburini, lakini akisikia kuna maiti ya Shefa imeonekana pale, atajua niliyeutupa mwili huo nilikuwa mimi na kwamba nilikataa tu kuficha ukweli.
Nilivyomjua Raisa alivyo na kidomodomo, suala hilo anaweza kulieleza kwa mke wake Shefa, hasa kwa kuamini kuwa siku aliyopotea Shefa alikuwa amekuja kwangu. Isitoshe, gari la Shefa bado lipo hatua chache tu kutoka nyumba yetu, hali iliyoonyesha aliliegesha wakati alipokuja kwangu.
Hapo nilijiona sikuwa na ujanja tena. Niliitupa ile maiti ili kujisalimisha; kumbe ndiyo nilijiangamiza! Ilikuwa ukweli kwamba sikumuua Shefa, lakini kitendo changu cha kwenda kuitupa maiti yake kisirisiri kitaonesha kwamba nilimuua mimi.
Hii imeshakuwa balaa! Nitafanya nini, jamani? Nikalaani. Nikaanza tena kulia. Wakati nalia nikapata wazo la kwenda kwa wazazi wangu nikawaeleze ukweli kabla sijakamatwa, lakini pia niliogopa kufanya hivyo. Niliogopa kwa sababu ningewashitua na pia niliogopa wangehisi mimi ndiye niliyemuua Shefa kutokana na kitendo changu cha kuficha maiti yake na kwenda kuitupa. Pia ningeshindwa kueleza wazi Shefa alifuata nini nyumbani kwangu usiku huo mpaka akauawa.
Nikaamua nisiende kuwaeleza wazazi wangu bali nisubiri nione nini kitatokea. Pia nilikuwa na wazo la kwenda kazini, lakini wazo hilo lilinitoka kichwani mwangu; nilikuwa tu nikizunguka nyumbani: mara sebuleni, mara chumbani. Mara kwa mara nilikuwa nikipenua pazia kulitazama gari la Shefa ambalo niliamini ndilo litakalonisababisha nishukiwe. Pamoja na kujua hivyo, sikuweza kuliondoa pale, ingawa funguo za gari hilo nilikuwa nazo.
Mpaka saa kumi jioni, nilikuwa sebuleni nikiendelea kutazama televisheni kwa kutegemea kuona taarifa nyingine ya Shefa. Raisa akanipigia simu.
“Shoga, una habari gani?” akaniuliza.
“Sina habari yoyote.”
“Shefa ameuawa, na maiti yake imekutwa makaburini Msambweni leo asubuhi.”
Aliponiambia hivyo nilishituka. Nilishituka kwa kujua Raisa alikuwa ameshayapata.
“Eti nini… unasema?” nikamuuliza nikijifanya sikumsikia vizuri.
“Kumbe Shefa ameuawa. Maiti yake imekutwa Msambweni makaburini leo asubuhi.”
“Khaa… unasema kweli, shoga?”
“Nasikia taarifa ilitolewa kwenye televisheni. Mimi nilipopata habari hizo nikampigia mke wake kumuuliza. Simu ilipokelewa na mdogo wake akaniambia ni habari ya kweli na wao walikuwa kituo cha polisi.”
“Sasa ameuawa na nani, jamani?”
“Haijajulikana. Polisi ndio wanafanya uchunguzi kumtafuta aliyemuua. Lakini mimi nadhani aliuawa na mwanamke ambaye tulimuona jana usiku akitupa kitu pale makaburini. Nafikiri ndiye alikuwa anamtupa.”
“Kumbe vile ulivyoniambia — umeona mwanamke ametupa kitu makaburini, alikuwa ni Shefa aliyetupwa!”
“Alikuwa yeye. Sijui walikosana nini mpaka akamuua mwenzake.”
“Na kupatikana tena si rahisi.”
“Anaweza kupatikana. Nadhani yule bodaboda wangu aliziona namba za gari lake nilipomwambia alifuate lile gari. Mimi nilikuwa nyuma yake, sikushughulika na namba hizo kwa vile nilivyohisi ni gari lako.”

Moyo wangu ukapiga kwa nguvu.
“Unadhani bodaboda wako atakuwa ameziona?”
“Bila shaka. Sasa hizi namba zikijulikana, lile gari linaweza kukamatwa.”
“Wasije wakalikamata gari langu kwa kufananisha namba!”
“Gari lako haliwezi kukamatwa. Namba za magari hazifanani.”
“Huyo bodaboda wako akikosea namba tu anaweza kuniponza.” Raisa akacheka.
“Raisa, usicheke, nakwambia kweli.”
“Hatakuponza. Gari lako linafahamika, shoga; ondoa hofu.”
Hapo nikajidai kucheka. Kwa vile hakuoni, nilitoa kicheko cha uongo huku uso wangu ukiwa na huzuni.
“Haya, shoga, baadaye,” Raisa akaniambia na kukata simu.
Nikashusha pumzi ndefu. Akili yangu ilikuwa ikinituma mawazo ya ajabu: niliyehamishie lile gari langu Sahare kwa wazazi wangu; akili nyingine ikaniambia niondoe tu nitakamatwa nalo. Nilihisi kwamba gari litabaki pale nyumbani kwangu na polisi wakija wanaweza kuliona na kulitia shaka.
Kabla akili yangu haijanipa ufumbuzi wa tatizo hilo la gari, ikanituma nimpigie Raisa ili nimshawishi twende pamoja msibani tukamfariji mke wa marehemu Shefa. Lengo langu lilikuwa kujikosha ili Raisa asinitilie mashaka. Akili nyingine ikaniambia nikate tiketi ya basi niende Dar na nikakae huko mpaka matatizo yatakapokwisha.
Lakini nikajiuliza nitamwambia nini mume wangu aliyeniambia kuwa anaweza kuja Tanga? Nikajiambia, nikifanya hivyo sitaeleweka na mume wangu na pia sitaeleweka na Raisa. Raisa ataona nimekimbia — jambo ambalo litamzidishia mashaka kwamba mimi ndiye niliyemuua Shefa.
Jinsi akili yangu ilivyokuwa ikihangaika, nilijihisi niliyechanganyikiwa. Nikaingia chumbani na kujilaza kitandani. Nikapitiwa na usingizi hapo hapo. Nikaota ndoto: niliona siku ile niliyolala na Shefa, wakaja wezi wawili. Wakavunja dirisha. Mmoja akaingia akiwa ameshika rungu. Wakati ule Shefa alikuwa anatoka msalani; akakutana na mwizi uso kwa uso. Shefa alitaka kupiga kelele, mwizi akamwahi kwa kumpiga rungu kichwani. Shefa akaanguka chini na kufa hapo hapo. Mwizi huyo akarudi kwenye dirisha na kumwambia mwenzake, “Imekuwa noma, twenzetu.”
“Kumetokea nini?” mwenzake akamuuliza.
“Nimeshaua.” Waizi wakakimbia.
Nikaamka hapo hapo. Niliinuka, nikakaa kitandani na kujiuliza ni kwanini nimeota ndoto ya aina ile. Niliwahi kusikia kwamba ndoto hutoa tafsiri za maisha ya watu. Nikajiuliza: je, kulikuwa na ukweli juu ya kile nilichokiota kwamba kuna mwizi aliyekuja na ndiye aliyemuua Shefa na kunisababisha mimi matatizo? Lazima alikuwa mwizi tu, nikajiambia. Haiwezekani mtu mwingine avunje dirisha kisha amuue kijana wa watu bila kosa.
Inaendelea…