BODI YA WADHAMINI MFUKO WA WANYAMAPORI KUJA NA MIKAKATI MIPYA

…………….

Na Saidi Lufune, Arusha

BODI ya Wadhamini ya Mfuko wa Wanyamapori Tanzania (TWPF) imepanga kuja na mikakati mipya ya usimamizi na uendeshaji kwa lengo la kuimarisha uhifadhi na kulinda rasilimali za wanyamapori nchini.

Akizungumza jijini Arusha wakati wa kufunga kikao cha kwanza cha bodi hiyo iliyopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, cha kujadili utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kuweka mikakati mipya ya mwaka 2025/26,  Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Jafar Kidegesho, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo unaleta matokeo chanya.  

Aidha, ametoa wito kwa sekretarieti ya bodi hiyo kuyatekeleza kwa vitendo maazimio yaliyopitishwa ili kusaidia kwa vitendo usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori nchini.

“Nendeni mkafanye kazi kwa ushirikiano kwa kutumia maarifa, utalaamu na weledi na kufanyia kazj maazimio tuliyokubaliana ili mwisho wa siku  tufanikiwe majukumu tuliyopewa,” amesisitiza Prof. Kidegesho.

Pamoja na hayo, Prof.Kidegesho amempongeza Mtendaji Mkuu wa Mfuko na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alexander Lobora, kwa kusimamia vyema utekelezaji wa majukumu, ikiwamo kuvunja mitandao ya ujangili na kuboresha hadhi ya baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa.

Kwa upande wake, Dkt. Lobora amesema Mfuko utaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 na  kubuni miradi mipya na kuongeza vyanzo vya fedha vitakavyosaidia kulinda rasilimali za taifa.

Aidha, amefafanua kuwa Bodi hiyo inajumuisha Mtendaji wa Mfuko, Katibu Tawala, pamoja na wajumbe kutoka vitengo vya Uendeshaji wa Miradi, Uhasibu, Uelimishaji na Uhamasishaji pamoja na Ugavi.