Dk Dimwa ataja vipaumbele 10 vya CCM akijinasibu kushinda

Unguja. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema chama hicho kimekuja na upepo mpya wa siasa za mshikamano na demokrasia ya kweli.

Dk Dimwa ametoa kauli hiyo leo Septemba 13, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika viwanja vya Mnazimmoja Unguja, Zanzibar ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.

“Tunaamini umoja wetu, sera zetu zinatupeleka kupata ushindi wa kishindo katika kipindi hiki cha pili,” amesema.

Dk Dimwa ametaja maeneo 10 mahususi ya vipaumbele vya CCM ambavyo vimeanishwa katika ilani ya chama hicho ya mwaka 2025/30.

Mambo hayo ni pamoja kuendeleza na kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ili kuzidi kuleta maendeleo na mafanikio, kuleta uchumi imara na ajira kwa vijana ambapo wanatarajia kuzalisha ajira 350,000.

Kipaumbele kingine ni kujenga maghala makubwa ya chakula, kuendeleza wananchi kiuchumi na kuanzisha makazi bora na kukua teknolojia na kudhibiti taka ili kuweka miji katika hali ya usafi.

Dk Dimwa ametaja jambo lingine ni kuanzisha hifadhi ya mafuta ya petroli na dizeli ili kuondoa changamoto ya bidhaa hiyo kupanda gharama kila mara.

Amesema miongoni mwa vipaumbele vyao ni kuandaa vivutio maalumu vya kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya utalii, ambapo tayari wametenga maeneo maalumu ya uwekezaji kwenye eneo la viwanda la Dunga Zuze, Unguja na Micheweni, Pemba.

“Kingine tumesema kwenye ilani tutaimarisha hifadhi za jamii kwa wananchi wetu,” amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar mstaafu, Vuai Ali Vuai amesema Dk Hussein Mwinyi ahitaji kuzungumzwa, kwani alichokifanya kinaonekana kwa macho hivyo wanayo kila sababu ya kumpa kura za kishindo.

Amesema alipoingia madarakani alitoa ahadi nyingi zingine zikiibua mijadala namna anavyoweza kuzitekeleza lakini ametekeleza kwa vitendo.

“Wakati anaingia madarakani alisema anawaunganisha Wazanzibari, tumeona alivyofanya, aliunda kamati mbalimbali za maridhiano,” amesema Vuai.

Amesema sifa kubwa aliyonayo Dk Mwinyi anashauriwa na kushaurika ndio maana amefanikiwa kutenda mambo makubwa kiasi hicho.