Dk Mwinyi ataja mambo matatu atakayoyapa msukumo akipewa ridhaa tena

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amesema katika kipindi kijacho cha uongozi, atajielekeza kwenye maeneo makuu matatu ambayo yataacha alama isiyofutika atakapomaliza muda wake madarakani.

Akitaja vipaumbele hivyo, Dk Mwinyi amesema ni kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kukuza uchumi, na kuboresha huduma za kijamii kwa manufaa ya Wazanzibari wote.

Ametoa kauli hiyo leo, Septemba 13, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika katika viwanja vya Mnazimmoja, Unguja.


“Tutaondoa masuala ya ubaguzi wa kila aina, ukabila, dini, rangi, ukanda wa Pemba na Unguja, Ukaskazini na Ukusini, katika awamu ijayo tutaendelea kudumisha amani na  umoja wetu kama nilivyoahidi mwaka 2020,” amesema.

Dk Mwinyi amesema wanatarajia kufanya kampeni za kistaarabu, bila kumtukana mtu kwa kueleza ambayo wanatarajia kuwafanyia Wazanzibari ili kuondoa changamoto zao.

Dk Mwinyi amesema iwapo atarejea madarakani atahakikisha anashughulikia ajira kwa vijana ambalo ni tatizo kubwa.


Amesema licha ya ilani ya chama hicho kuahidi ajira 350,000 lakini ana imani zitazidi kwa sababu wanakwenda kuongeza mkakati katika ujenzi wa viwanda na kilimo.

Amesema imani yake uchumi utakuwa kutoka asilimia 7.4 ya sasa hadi kufika asilimia 10 kabla ya kuondoka madarakani.

“Ndugu zangu tumefanya mengi na tutahakikisha tunaendeleza yale ambayo tuliyafanya, naomba mtuchague tena ili tukayamalizie haya,” amesema.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi  kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili wapate ushindi mkubwa ambao utaondoa malalamiko ya kuibiwa kura.

“Ndugu zangu ushindi unapokua mdogo unaibua manung’uniko, sasa kwa wingi wetu huu naomba tujitokeze tushinde kwa kishindo tusiwape nafasi ya kudai hayo,” amesema.