Dk Nchimbi: Tutaziunganisha kaya zote na umeme

Kilimanjaro. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema, shabaha ya chama hicho miaka mitano ijayo ni kuhakikisha kaya zote nchini zinaunganishwa na umeme ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumamosi, Septemba 13, 2025 katika mikutano ya kampeni ya uchaguzi mkuu kwenye baadhi ya majimbo mkoani Kilimanjaro alikowasili leo akitokea Arusha.

Lengo la mikutano ni kusaka kura za mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.


Akisalimia wananchi na wanachama wa chama hicho eneo la Bomang’ombe, Jimbo la Hai, Dk Nchimbi ameeleza jinsi Serikali ya CCM itakavyokwenda kushughulika na matatizo ya wananchi katika miaka mitano ijayo.

Suala la umeme amelizungumzia akijibu maombi ya mgombea ubunge wa Hai, Saashisha Mafuwe ambaye ameeleza mambo mbalimbali yaliyofanyika ikiwemo baadhi ya vijiji kuunganishwa umeme na vingine bado.

Mafuwe amegusia suala la miundombinu hususan ya barabara, akimwomba mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan na Dk Nchimbi kuliangalia ili barabara hizo zipitike wakati wote.

“Wilaya ya Hai ni ya CCM, tulikuwa na shida ya maji na sasa yanapatikana.

Mateso ya barabara kwa miaka 20 lakini sasa tunazo na taa juu. Lakini tunaomba gari la visima, lije hapa lichimbe visima ili maji yawepo ya kutosha,” amesema Mafuwe.

Aidha, amesema kuna shule chakavu zinahitaji ukarabati. Pia, ujenzi wa shule mpya zaidi ya 10, vituo vya afya na zahanati zimejengwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mafuwe amesema: “Tumeonja utamu wa CCM, haturudi nyuma tena.”

Jimbo la Hai kwa muda mrefu limekuwa ngome ya upinzani likiongozwa na Freeman Mbowe kama mbunge wake. Mbowe amewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema kwa zaidi ya miaka 20.

Mara baada ya Mafuwe kumaliza kuzungumza, Dk Nchimbi akasema: “Mbunge wenu, amefanya kazi kubwa, kuwatetea, kuwapigania. Huo ndio uzuri kuwa na mwakilishi kutoka chama makini na yeye ni mtu makini. Wanapokupa miaka mitano mingine, usibadilike.”


Dk Nchimbi amejibu hoja za Mafuwe kwa kueleza wanachokwenda kukifanya miaka mitano ijayo, kwamba ilani ya uchaguzi 2025/2030 imetaja mambo watakayohangaika nayo, likiwemo la barabara ili zipitike muda wote.

“Huduma ya umeme si vijiji vyote bali kaya zote nchini ziunganishwe na umeme,” amesema Dk Nchimbi.

Mgombea mwenza huyo akasema:”

Chama chetu chini ya Rais Samia, Kimedhamiria kwenda mchakamchaka kuleta maendeleo ya wananchi wetu.”

Katika eneo la kilimo, amesema vifaa vya kupima ubora wa ardhi vipo Hai na zaidi ya sampuli 800 zimepimwa na mkulima anakuwa ma uwezo wa kuamua analima nini na wakati gani.

“Kitu kinachohitajika na kukiomba ni kura za kutosha. Kwa hiyo, Chama cha Mapinduzi hakijabadili utamaduni wake kwamba jukumu ni kuhakikisha tunashughulika na matatizo ya wananchi,” amesema.

“Rais wetu amehangaika sana na matatizo ya wananchi kwa miaka minne, anafanya hivyo bila kuchoka sasa kwa nini sisi tusisimame siku moja tu ya kupiga kura, ili tumchague kwa kishindo na CCM imejizatiti kufanya mabadiliko zaidi, imejizatiti kuleta maendeleo,” amesema.


Kuhusu maji amesema, tunakwenda kuondoka na tatizo la maji, kuleta gari la kuchimba visima hilo limeisha, sisi kama chama ni kuchukua hatua na hili limeisha.

Sumaye: Samia ametuheshimisha

Katika mkutano wa Jimbo la Siha, uliofanyika Sanya Juu, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema kuna watu walikuwa wanasema: “Mama ataweza kweli kuzunguka nchi nizma, lakini tunavyomwona kila siku kama ndiyo anaanza. Anachapa kazi kweli kweli.

“Tuna Rais anayeheshimika ndani na nje. Matumizi kama ya nishati safi yamesababisha mikutano mingi duniani imeletwa Afrika kwa sababu ya Mama Samia. Kwa hiyo ni Rais ambaye dunia inamtegemea na anaishangaza,” amesema.

Sumaye ambaye ni mratibu wa kampeni za CCM Kanda ya Kaskazini, amesema anayoyafanya Rais Samia tangu ameingia madarakani: “Ametuheshimisha, na sisi tarehe 29 tujitokeze kwa wingi kumchagua kwa kishindo.”

Baadaye Nchimbi atafanya mikutano Vunjo na Moshi Mjini.