DK.SAMIA ATOA RAI WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA KIGOMA KUFANYABIASHARA NA NCHI JIRANI

 *Aweka wazi mipango itakayokwenda kutekelezwa na serikali miaka mitano ijayo

*Azungumzia mbolea ,pembejeo za ruzuku zilivyoongeza uzalishaji mazao Kigoma

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kigoma

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imefanya maendeleo makubwa katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ambayo kwa ujumla imefungua fursa kwa wananchi wa mkoa huo.

Akizungumza leo Septemba 13,2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kasulu

mjini mkoa Kigoma Dk.Samia ametumia mkitano huo kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kutafuta utatuzi wa changamoto zilizokuwa zinawakabili wananchi wa Wilaya hiyo.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji mbolea amesema kuwa Serikali  imetoa mbolea ya ruzuku  kwa wilaya hiyo ambapo imewahufaisha wakulima 23,200 kutoka Kasulu vijijini na wakulima 63,300 wa mji wa Kasulu.

“Ninapopita barabarani ninaona uzalishaji ni mkubwa. Nimeambiwa mazao ni mengi kuanzia maharage, mahindi na mazao ya mbogamboga ninayaona yamepangwa barabarani.

“Imani yangu ni kwamba mbolea zile zimeleta mazao mengi, masoko yapo wazi, nchi jirani inanunua kila kitu wenzetu wa Burundi. Mimi niwaombee biashara njema ya mazao ya kilimo,” amesema Dk.Samia.

Kuhusu sekta ya maji, ameeleza kwamba Serikali imefanya kazi kubwa lakini bado kuna upungufu wa uhitaji wa maji huku akifafanua mradi wa maji miji 28 unaendelea kutatua changamoto ya maji lakini pia serikali imeweka magari ya kuchimba visima kila mkoa.

“Katika maeneo yasiyokuwa na vyanzo vya maji, Serikali  itachimba visima virefu ili maji yapatikane kwa wananchi.

Akizungumzia ujenzi wa reli ya SGR Dk.Samia Suluhu Hassan amesema mradi huo mkubwa wa kitaifa Mkoa wa Kigoma utakuwa  na vituo vingi kuliko mikoa mingine.

“Kwa sababu reli hii kwa Tanzania itafika Kigoma, fursa kubwa za kibiashara zitapatikana hapa. Lengo ni kuufungua Mkoa wa Kigoma kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ili uwe kitovu cha biashara.”

Hivyo ametoa mwito kwa wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa kwa kufanyabiashara na nchi jirani na hata ndani ya nchi.

Kwa upande wa nishati ya umeme Dk. Samia amesema Serikali imefikisha huduma ya umeme ikiwemo kutengeneza mazingira ya fursa za uwekezaji na kufafanua Kigoma tayari imeanza kupata uwekezaji katika viwanda vikubwa. 

“Kuna kiwanda cha saruji kipo Kigoma, kuna kiwanda cha sukari Kasulu na kuifanya Kigoma kuwa mkoa wa kimkakati kwenye uzalishaji sukari nchini.Mbali ya viwanda hivyo ni waahidi tunakwenda kuandaa zaidi mazingira ili wawekezaji zaidi waje Kigoma.”

Akieleza zaidi Dk.Samia amesema kwa sababu mkoa huo kuna reli zote mbili, wawekezaji watajitokeza kwa wingi kwa sababu usafirishaji kwenda masoko ya jirani utakuwa umerahisishwa.

“Mwekezaji atakayejenga kiwanda chake sasa pindi atakapokamilisha miaka miwili ijayo atakuta ujenzi wa reli umefikia hatua kubwa zaidi.Ataweza kufanyabiashara zake vizuri. 

“Kile kiwanda cha sukari ambacho kipo Kasulu kimetengeneza ajira 500 kwa vijana wa mji wa Kasulu. Hii ni hatua kubwa sana.Huu ni mwanzo jinsi kinavyoendelea ajira zitaendelea kutengenezwa na vijana watapata ajira,” amesema Dk.Samia.

Amesisitiza katika miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji huduma za kijamii kwa kuzingatia utu wa Mtanzania.