Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo, Omar Issa Shaaban ameeleza kuwa chama hicho kimekataa gari lililotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya mgombea wao wa urais, Luhaga Mpina, kwa kuwa wanamini kuwa usafiri huo si kigezo cha uwanja sawa katika uchaguzi.
Amesema sababu zilizotolewa za INEC kuwa lengo la kutoa magari hayo ni kuweka uwanja sawa kwa wagombea na vyama kwenye uchaguzi hazina uhalisia.
Hata hivyo, Mpina ameeleza kuwa askari polisi waliopewa kwa ajili ya kuwalinda yeyw na mgombea mwenza, wamewakubali kwa sababu ni suala la kisheria.
Shaaban ametoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao umefanyika leo Septemba 13, 2025, makao makuu ya chama hicho Magomeni jijini Dar es Salaam.
INEC iliamua kutoa magari kwa wagombea urais ikisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na usawa katika kampeni za wagombea urais wa vyama vyote. Wagombea wote waliyakubali isipokuwa wa ACT – Wazalendo.
Kwa upande wa Zanzibar Tume ya Uchaguzi (ZEC), iliripotiwa kuwa ilitoa magari tisa kati ya 11 yaliyotarajiwa, kwa ajili ya wagombea wa urais wa Zanzibar.
Hata hivyo, wagombea wawili – Dk Hussein Mwinyi wa CCM na Othman Masoud Othman wa ACT-Wazalendo hawakupokea magari hayo kwa kuwa tayari wanamiliki magari ya Serikali kutokana na nyadhifa zao.
Leo mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina na mgombea mwenza wake Fatma Abdulhabib Fereji wamepitishwa rasmi na INEC kuwania urais, kisha wakalikataa gari aina ya Toyota Land Cruiser GX VXR.
Awali, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele, baada ya kupokea fomu za Mpina amesema wameamua kutoa magari kwa wagombea wote wa urais ili kuhakikisha usawa katika kampeni.
“Tume imeamua kumpatia kila mgombea gari moja pamoja na dereva kwa matumizi ya kampeni,” amesema.
Hata hivyo, baada ya maelezo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Omar Shaaban alisimama na kueleza kuwa chama hicho hakitapokea gari hilo.
“Kwanza tunashukuru sana kwa ukarimu mliotuonyesha, lakini tumependelea kutochukua gari. Tupo vizuri na tunaomba raslimali hiyo isaidie kwenye matumizi mengine,” amesema.
Akijibu kauli hiyo, Jaji Mwambegele amesema, “Sawa, ni mapenzi yenu. Lengo la magari haya lilikuwa ni kuweka usawa katika kampeni, lakini kama hamtalihitaji, tume italitumia kwa matumizi mengine.”
Ufafanuzi wa kukataa gari
Baadaye kwenye makao makuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Shaaban amesema: “Tunapozungumzia usawa wa wagombea na vyama kwenye uchaguzi kipimo chake si kupewa gari la kifahari wakati Watanzania wanakufa njaa.
“Kipimo cha uwanja sawa kwenye uchaguzi hakiwezi kuwa gari, wakati tayari watu wana Sh100 bilioni kwa ajili ya uchaguzi na kuna vyama havina hata Sh100.
“Tunaposema uwanja sawa haiwezi kuwa gari wakati kuna vyama wagombea wake wameenguliwa, wengine wagombea wao hawajaguswa, hiyo haiwezi kuwa uwanja sawa kwenye uchaguzi.”
Shaaban amesema wamekataa gari kwa sababu kipimo cha mazingira ya usawa kwenye uchaguzi ni wagombea wote kupewa fursa sawa.
“Fursa sawa hiyo ni kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kutangaza sera zao, tunapozungumza hivi sasa huko Zanzibar kuna chombo cha habari hakitoi taarifa zozote za mgombea wetu wa urais na uwakilishi, lakini ukienda kwenye chombo hicho hicho kuna picha za wagombea wa chama tawala.
Kwa upande wake Mpina amefafanua zaidi sababu za kukataa gari la INEC kwamba ndio msimamo wa chama na mgombea.
“Tulichofanya pale kulikuwa na mambo mawili makubwa, moja ni mlinzi ni jambo la kisheria ambalo mgombea urais lazima upewe hakukuwa na tatizo katika tatizo na mlinzi ametolewa na yupo.
“Jambo la pili ni gari, suala la gari kauli aliyoitoa mwanasheria wetu ni msimamo wa ACT – Wazalendo na mgombea wa nafasi ya urais na makamu wake, mfano chama na mgombea tunayo magari ya kutuwezesha kuzunguka nchi nzima kufanya kampeni.
“Kwa nini tuchukue hili gari ambalo linaweza kufanya kazi zingine, sisi tunataka ikawe hapa kazi tu, kama tunataka ikawe hapa kazi tu halafu una gari tu.”
Mpina amesema kucheleweshwa kwa siku 17 kuingia kwenye uchaguzi huo, watashinda kwa zaidi ya asilimia 70 na asilimia 30 zilizobaki CCM itagawana na vyama vingine,” amesema.