Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina amesema ataanza na hotuba ya saa sita ili Watanzania waijue nchi yao kikamilifu, kabla ya kutumia siku 45 za kampeni zilizobakia.
Amesema kinachofuata baada ya kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni kuzindua ilani, kueleza maono ya mgombea na uzinduzi wa kampeni.
Mpina amesema kupitia msukumo ulio ndani yake anaamini atashinda uchaguzi kwa asilimia 70 na 30 zilizobakia watagawana wagombea wa vyama vingine.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari ikiwa ni saa chache tangu INEC imteue kuwa mgombea urais na Fatma Fereji kuwa mgombea mwenza.

Mpina amesema anafahamu kuwa wanaingia kwenye uchaguzi zikiwa zimepita siku 15 za kampeni kati ya 60 zilizotolewa kwa wagombea, lakini atahakikisha siku 45 zilizobaki wanazitumia vyema.
“Pamoja na hayo yote yaliyotokea nahodha mahiri hafundishwi kwenye maji yaliyotulia bali ya dhoruba, hivyo siku zilizobaki zinatutosha.
“Tutatembea majimbo yote Tanzania Bara na visiwani, yote 272 kipindi hiki kilichobakia, wagombea wetu wa nafasi za ubunge na udiwani msiwe na mashaka katika hilo, tunakwenda kufanya kampeni na tutazindua haraka iwezekanavyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele akimkabidhi nakala ya fomu za uteuzi Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina (kulia), aliyeambatana na mgombea mwenza wake, Fatma Ferej, baada ya kuteuliwa rasmi kuwania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025. Picha na INEC.
Amesema ili kuhakikisha hawapotezi muda zaidi watafanya mambo yanayohitajika kwa haraka ikiwemo uzinduzi wa ilani yao ya mwaka 2025.
“Sisi tuko tayari kwa ajili ya kampeni, Watanzania wote na wapenda mabadiliko najua huzuni na majonzi mliyokuwa nayo baada ya mgombea wa ACT Wazalendo kuzuiwa kurejesha fomu, na ninajua furaha yao baada ya uteuzi huu.
“Niwahakikishie kuwa, tunajua tumeomba hizi nafasi tukiwa tayari tuna uzoefu wa kutosha, tunayajua matatizo ya Watanzania na tuko tayari kuyashughulikia na kufanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania,” amesema.
Amesema mapengo ambayo yalikuwa yakionekana katika kampeni yatazibwa na ili hilo lionekane ataanza kwa kuhutubia Taifa kwa saa sita, kueleza kwa makini namna walivyojipanga kulitoa Taifa na kulipeleka sehemu linapostahili.
“Tumezaliwa kwa ajili ya hilo hatuwezi kukaa nyumbani na haki za Watanzania zikiwa mbaya, tutaanza na mkutano wa saa sita na baadaye kwenye uzinduzi wa kampeni na siku zote 45 zilizobakia,” amesema.
Amesema kupitia uteuzi uliofanyika leo sasa safu ya ACT Wazalendo imekamilika hiyo ni baada ya Othman Masoud Othman kuteuliwa kuwania urais Zanzibar na tayari amefungua rasmi kampeni zake, huku yeye akiwania nafasi hiyo kwa upande wa Tanzania Bara.
“Walisema hatutakuwepo kwenye sanduku la kura sasa tumekuwemo, pia tupo kwenye karatasi za kupigia kura na kampeni zitaanza mara moja ili kutopoteza muda,” amesema.
Amesema anaamini kama mgombea mwenye sifa na vigezo anakwenda kushinda uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 70 na nyingine watagawana wanaobakia.
“Tunakwenda kuibuka kidedea katika uchaguzi wa mwaka 2025, kwa asilimia 70, hizo nyingine zilizobakia watagawana wenyewe,”amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuitaka INEC na mamlaka zote za umma zifanye kazi kwa mujibu wa sheria kama zinavyowataka wafanye, kwani Taifa ni la watu wote na vyama vya siasa vimeruhusiwa kikatiba na wapinzani si wahalifu katika nchi yao.
“Hakuna sababu ya kutumia mamlaka ya umma kuviadhibu vyama vya siasa, tulijenge Taifa kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali zinafanya kazi kwa usawa kwa vyama vyote na endapo wakienda kwa ubaguzi tutaenda hadi mahakama za kimataifa,” amesema.
Amesema kama chama wakiona kuna aina ya upendeleo watakuwa wakisema kwa uwazi ili kuhakikisha kila kitu kinafanywa kwa mujibu wa Katiba.
Mgombea mwenza, Fatma Fereji amesema wako tayari sasa na wataendelea kuwa tayari kuhakikisha wanachanja mbuga kwa siku zilizobaki ili waweze kupata ushindi.

Kwa upande wake, kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amesema wakati wakipambania haki ya kushiriki Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu zilikuwa wiki mbili ngumu za ujasiri kujitoa, lakini za kujiamini kuwa mabadiliko ya Taifa yataletwa na wao wenyewe.
Hilo limefanya ACT Wazalendo kuwa chama tumaini, tegemeo na hilo litadhihirika Oktoba 29, huku akisema hawana shaka kwani waliandaa wagombea makini watakaonadi ilani ya chama na kuwafanya waibuke washindi.
“Haikuwa wakati rahisi lakini tumeona uimara, ukomavu wa chama cha ACT Wazalendo, tunawashukuru viongozi wote ambao waliendelea kukinadi chama na kutoa matumaini kwa wananchi kuwa tutarudi.
“Kampeni zilipoa hatukuona kilichokuwa kikiendelea, tumerudi na tumerudi imara,” amesema Semu.
Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Issa Shaaban amesema wamekataa gari kwa sababu uwanja sawa wa wagombea hauwezi kutengenezwa kwa kupewa gari ya kifahari wakati Watanzania wanakufa njaa.
“Hatuwezi kuwa na uwanja sawa wakati vyama vingine wagombea wake wameenguliwa na chama kingine hawajaguswa, uwanja sawa hauwezi kuwa kupewa gari bali kuweka usawa katika kila kitu ikiwemo kwenye vyombo vya habari. Gari tumeikataa hapa Tanzania Bara na Zanzibar pia uwanja sawa tunaoutaka ni mabadiliko ya sheria na uchaguzi huru,” amesema.
Akizungumzia suala hilo, Mpina amesema kukataa gari ni msimamo wa chama na yeye mwenyewe lakini walichukua mlinzi kwa sababu ni suala la kisheria.
“Sisi chama tunayo magari ya kutuwezesha kuzunguka nchi nzima kufanya kampeni, kwa nini tuchukue gari ambalo linaweza kufanya kazi nyingine,” amesema.