SAA chache tangu Pamba Jiji itwae kombe ikiwa Kenya mbele ya wenyeji wao, Shabana FC, kocha mkuu wa timu hiyo, Francis Baraza amesema kikosi hicho kipo tayari kwa mechi ya kwanza wa Ligi dhidi ya Namungo itakayopigwa Septemba 18.
Pamba Jiji iliyotwaa taji hilo kwa penalti 5-4 baada ya sare ya mabao 2-2 itaanza Ligi Kuu ugenini kwenye Uwanja wa Majaliwa na imefichuka kabla ya kuanza mbio za ligi uongozi wa timu hiyo umeandaa Dinner Gala kwa wachezaji wao tayari kwa msimu mpya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema timu yake ipo tayari kwa asilimia 90 huku 10 zilizobaki zitakuwa ni maandalizi ya mwisho ya mbinu na maelekezo madogo kwa wachezaji wa timu hiyo.
“Timu ipo tayari nafurahishwa na namna wachezaji wote walivyo na utayari na kila mmoja akihitaji namba kikosi cha kwanza kitu ambacho kinanipa nguvu ya kuanza vizuri msimu,” alisema Baraza na kuongeza;
“Utayari wa wachezaji wangu utathibitika baada ya dakika 90 za mchezo wetu wa kwanza wa Ligi ugenini tukiikabiri Namungo hautakuwa mchezo rahisi kutokana na sajili zilizofanywa na wapinzani si timu moja tu ni timu zote.”
Baraza alisema malengo msimu huu ni kuhakikisha mzunguko wa kwanza wanaanza vizuri kwa kukusanya pointi nyingi, ili duru la pili wasiwe na presha na wanaamini wana kila sababu ya kuwa bora kutokana na kikosi walichonacho. “Duru la kwanza hautokuwa rahisi, lakini ndio unatatoa changamoto kutokana na wachezaji kuwa na nguvu ya kuonyesha kwa benchi la ufundi ili waweze kuaminiwa hivyo huo ndio wa kuutumia vizuri ili kuweza kufikia malengo,” alisema Baraza na kuongeza;
“Hatutakuwa na sababu uongozi umefanya jukumu kwa kusajili na mimi kama kocha nimefanya kazi yangu kuandaa timu kilichobaki ni uwajibikaji kama timu kuhakikisha tunapata matokeo matumaini ni makubwa bado utekelezaji.”