Maximo ataka KMC itue anga za Azam

KOCHA wa KMC, Marcio Maximo ameanza kuipigia hesabu ndefu timu hiyo akitaka iwe kituo cha kuzalisha mastaa wakubwa wa Tanzania.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maximo alisema kikosi chake kinaundwa na wachezaji wengi vijana ambao ana hesabu nao kubwa.

Maximo ambaye amewahi kuifundisha Yanga na Taifa Stars, alisema kiu yake kubwa ni kuwasuka vijana hao kuja kutawala vikosi vyote vya timu ya taifa.

“Wakati nikiwa hapa Tanzania huko nyuma nilifanya kazi hiyo, lakini haikuwa kwa ukubwa kama nilivyotaka,” alisema Maximo.

“Hapa sasa (KMC) kuna nafasi ya kulifanikisha hili. Tunaweza kuifanya KMC kuwa timu kubwa itakayokuwa na wachezaji wengi kwenye timu zote za Taifa.”

Maximo aliongeza kuwa KMC Inaweza kufanya ambacho inafanya Azam FC kwa kuwa na mchango mkubwa wa wachezaji wengi wanaozichezea timu za Taifa.

“Angalia Azam FC kwenye kila timu ya taifa ina wachezaji. Tanzania imebarikiwa vipaji vikubwa. Nataka KMC iwe hivyo.

“Hapa tuna vijana wana vipaji sana. Nimewaambia wajipange kufuata maelekezo ili wawe kama kina Pipino wengine.”

Msimu wa 2025/26 unatarajiwa kuanza siku chache zijazo, huku Maximo akiwa ndiye kocha mkuu wa kikosi hicho.