Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimekataa kupokea gari jipya lililotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kila mgombea wa nafasi ya urais kikisema kiko vizuri katika rasilimali.
Tukio hilo limetokea leo Septemba 13, 2025 baada ya Mpina kurejesha fomu INEC, Dar es Salaam za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Mpina amefika ofisi za INEC zikiwa siku mbili zimepita tangu ashinde kesi dhidi ya INEC, akipinga kuenguliwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Mpina alienguliwa katika kinyang’anyiro hicho na INEC Agosti 26, 2025, hivyo pamoja na Bodi ya Wadhamini ya ACT-Wazalendo walifungua kesi dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Agosti 27, 2025.
Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma katika uamuzi iliyoutoa juzi ilisema INEC ilimwengua Mpina katika mchakato huo isivyo halali kwa kuwa haikumpa haki ya kumsikiliza na haikustahili kufuata maelekezo ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hivyo iliamuru apewe fursa haraka iwezekanavyo ya kuwasilisha fomu na mchakato wa kuzipokea uendelee ulipoishia Agosti 27, 2025.
ACT-Wazalendo kilifungua kesi kutokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais na INEC kumzuia kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa.
Shauri hilo lilisikilizwa na majaji, Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza, kwa njia ya maandishi.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kuomba uteuzi wa INEC kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025
Hata hivyo Agosti 26, Msajili wa Vyama vya Siasa, alitangaza kubatilisha uteuzi wake kutokana na pingamizi lililowasilishwa kwake na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala, aliyedai uteuzi wa Mpina ni batili kwani hakuwa na sifa kwa mujibu Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Chama, Toleo la mwaka 2015.
Mpina amefika ofisi za INEC akiongozana na viongozi wa chama hicho akiwamo Dorothy Semu na kupokewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Ramadhani Kailima.
Akizungumza baada ya kupokea fomu, Kailima amesema wagombea waliopendekezwa na ACT-Wazalendo kuwania urais na makamu wa Rais wametimiza masharti ya ibara ya 39 (1) (41) na ibara ya 47 (4) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 20(5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani za 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imemteua Luhaga Mpina kuwa mgombea urais na Fatma Abdul Ferej kuwa mgombea kiti cha makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo,” amesema Kailima.
Baada ya uteuzi huo walikabidhiwa seti moja ya fomu za uteuzi na nakala ya tamko la kuheshimu na kutekeleza Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za mwaka 2025 kwa ajili ya kumbukumbu zao.
Hata hivyo, ilipofika wakati wa kukabidhiwa gari kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine 17 wa nafasi ya urais, chama hicho kupitia mwanasheria wake, Omar Issa Shaaban kilikataa kuchukua gari hilo.
Awali, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele aliwapongeza kwa kuteuliwa kuwania nafasi hizo, huku akisema INEC ingependa kumkabidhi gari jipya aina ya Toyota Land Cruiser kwa ajili ya kampeni ambalo pia litakuwa na dereva.
Baada ya kauli hiyo, mwanasheria wa ACT-Wazalendo, Shaaban amesema: “Kwa niaba ya chama naomba kushukuru juu ya uamuzi wa kutaka kutupatia gari jipya kwa ajili ya shughuli zetu, lakini katika upande wa rasilimali tupo vizuri.”
Jaji Mwambegele alikubali uamuzi huo akisema: “Kama mmekataa ni sawa, kwani lengo la kutoa gari hili ilikuwa ni kusaidia katika kufanya kampeni ili kuweka uwanja sawa kwa wagombea wote. Kama ninyi hamtalihitaji, basi tutalitumia kwa shughuli nyingine.”
Gari alilopaswa kukabidhiwa kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine ni aina ya Toyota Land Cruiser GX VXR.
Baada ya shughuli za uteuzi kukamilika, Mpina na msafara wake aliondoka kwa kutumia gari alilokuwa amekwenda nalo ofisi za INEC, huku lile alilokuwa akabidhiwe likiachwa katika ofisi hizo.