Bunda. Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joseph Kasheku, maarufu Msukuma amesema majungu ndani ya chama hicho ndiyo yaliyosababisha mgombea ubunge Bunda Mjini, Ester Bulaya kuhamia upinzani.
Msukuma ameyasema hayo mjini Bunda leo Jumamosi Septemba 13, 2025 kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi za chama hicho jimboni humo, huku akiwataka wakazi wa jimbo hilo kukipigia kura za ndiyo chama hicho kwa asilimia 100.
Amesema Bulaya alihamia upinzani huku akiipenda CCM na sasa amerudi nyumbani wakazi wa jimbo hilo wanapaswa kumuunga mkono na kumtuma ili akawatumikie.
“Bulaya ana roho ya CCM hata alipokuwa kule bado roho yake ilikuwa CCM ila sababu ya majungu yetu hakuwa na namna ikabidi aende kule, lakini pamoja na kuwa alikuwa upinzani bado aliendeleza moto wake uleule wa kuwasemea wana Bunda Mjini,” amesema Msukuma.
Amefafanua kuwa kutokana na umuhimu wake chama hicho kiliamua kumteua kuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo ili akaendelee na kazi nzuri ya kuwawakilisha wana Bunda.
“Sio kwamba waliokuwepo hawafai hapana, ila ubunge ni kazi ya kupokezana vijiti sasa ni zamu ya Bulaya wana Bunda msifanye makosa mtumeni akawatumikie kama ambavyo amekuwa akifanya siku zote,” amesema.
Amesema miongoni mwa mambo aliyofanya akiwa mbunge wa upinzani ni pamoja na suala la wakazi wa Kata ya Nyatwali wilayani humo, waliokuwa wanatakiwa kupisha ushoroba wa wanyama katika eneo hilo.
Amesema Bulaya alisimamia jambo hilo kwa ukamilifu wake hali iliyosababisha asilimia zaidi ya 90 ya wakazi wa eneo hilo kulipwa fidia na kupisha.
“Bado kuna watu wachache hawajalipwa na hili liko chini ya uwezo wa Bulaya, mpeni kura akalifanyie kazi mapema sana Bulaya ni jembe mtumeni akawatumikie,” amesema.
Amesema Bulaya amechagua chaguo sahihi kurejea CCM hivyo ni wakati wa wana Bunda kunufaika na uwepo wake ndani ya chama hicho.
Amewataka wana CCM kuvunja makundi yaliyotokana na kura za maoni kwani sasa mgombea ni mmoja na jukumu lililo mbele yao ni kutafuta kura za ushindi wa chama hicho.
Bulaya amesema yeye ni yule yule kilichobadilika ni njia ya kuingia bungeni tu hivyo wakazi wa jimbo hilo wanatakiwa kuendelea kumuamini, kwani anamaanisha maendeleo na maisha bora kwa wana Bunda.
Amesema uwezo wa kujenga hoja anao na kubwa zaidi amerudi nyumbani hivyo anajua wapi pa kupita ili miradi iweze kutekelezwa kwa wakati.
“Nitaanza na ujenzi kilomita 23 za barabara za lami za mitaa ya Bunda mjini, ujenzi wa stendi ya kisasa, soko la kisasa tunataka hadhi ya jimbo la Bunda iendane na jina lake na kwenye hili upele umepata mkunaji,” amesema.
Bulaya amesema kati ya wagombea ubunge anaoshindana nao, yeye ana sifa kuliko wote amesema ana wazidi vitu vingi ikiwamo uwezo wa kujenga hoja, unyeyekevu, weledi na dhamira njema hivyo kuwataka wana Bunda wote kauchana na itikadi ya vyama vya siasa na wachague mtu sahihi kwa maendeleo ya jimbo lao.
Amesema bungeni hakuna suala la itikadi bali ni masuala ya maendeleo ya kitaifa na jimbo na kazi hiyo anaiweza kuliko yoyote, hivyo akichaguliwa kuwa mbunge atawalipa wakazi wa Bunda kwa utumishi uliotukuka.
“Hii kazi naiweza, hili jimbo nalifahamu sana changamoto zake zote nazijua, bungeni napajua sana nipeni imani yenu nami nitawalipa kwa utumishi uliotukuka,” amesema Bulaya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bunda, Abraham Mayaya amesema chama chake kinaomba kuingia mkataba na wananchi ili kiweze kukamilisha na kuanzisha miradi mingine mipya kwa ustawi wa jamii ya Bunda mjini.
Amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali ya CCM imefanya mambo makubwa ya maendeleo kwa wakazi wa jimbo hilo na kupitia ilani yao ya uchaguzi, yapo mengi yaliyopangwa kufanyika na kuwataka wakazi wa jimbo hilo kukipigia kura chama hicho.
Amesema Bulaya amefanya kazi kubwa kwa ajili ya wakazi wa jimbo hilo kabla na baada ya kujiunga na Chadema, hivyo chama hicho kimemteua kugombea ubunge jimboni humo kwani wana imani na utendaji wake wa kazi.
“Alipokuwa CCM aliwasemea wana Bunda na hata alipokuwa Chadema aliendelea kuwasemea wana Bunda sasa tuna wasiwasi gani, sisi tunachotakiwa kufanya ni kumpigia kura yeye pamoja na wagombea wote kupitia CCM,” amesema.
Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Joyce Mang’o amesema Bulaya ni mtu sahihi kwa wakazi wa jimbo hilo hivyo itakapofika Oktoba 29, 2025 wakazi wa jimbo hilo wahakikishe wanampigia kura nyingi.
“Sisi wakati Ester yuko upande wa pili tulikuwa tunamtamani, sasa amekuja kwetu niwaombe kwa umoja wetu tumtume akatutumikie bila kumsahau Rais wetu na madiwani wetu,” amesema Mang’o.