Nyambui ashauri mambo matatu kukuza riadha

‎DAMIAN MASYENEN‎‎KUENDELEA kusuasua kwa riadha nchini kumemuibua mwanariadha mkongwe na kocha wa mchezo huo, Suleiman Nyambui ambaye ameshauri mambo matatu yatakayoupa hadhi mchezo huo.

Nyambui ameyataja mambo hayo kuwa ni kupata wadhamini, mbio zinazoandaliwa katika maeneo mbalimbali nchini kuwa na maandalizi bora yatakayovutia wanariadha kushiriki pamoja na wadau na wanariadha kujitokeza kwa wingi pale mbio zinapoandaliwa.

‎Mwanariadha huyo wa zamani ameyasema hayo jijini Mwanza katika hafla ya miaka mitano ya mbio za Lake Victoria Marathon ambazo katika msimu wake wa tano zitafanyika Oktoba 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

‎”Ili kufanikisha mchezo huu tunahitaji mambo matatu ambayo ni kupata wadhamini, kufanya maandalizi mazuri na kupata watu wengi kwenye mbio. Tukifanikisha hayo basi..,” amesema Nyambui.

‎Ameongeza kuwa, “siyo kitu kinafanyika maandalizi ni mabovu, watu hawapati zawadi, hakuna wadhamini, njia ni mbovu vitu kama hivyo vinavunja mioyo ya wakimbiaji.”

‎Nyambui ambaye aliiletea sifa Tanzania kupitia mchezo wa riadha ikiwemo Olimpiki 1980 nchini Urusi, alivitaka vyama vya mchezo huo kuwasiliza wanariadha juu ya mahitaji yao ili kuzifanikisha na kuzifanya kuwa kubwa na zenye mvuto.

‎”Mimi ni mtu wa Mkoa wa Mwanza ninajiskia vizuri ninapoona mbio zinafanyika hapa na vipaji vipya vinazaliwa. Nawapongeza Lake Victoria Marathon msikate tamaa mnapopata changamoto mzitumie kuboresha na kuwapa nguvu ya kufanya vizuri zaidi,” amesema Nyambui.

‎Muasisi na mbio hizo, Halima Chake amesema katika msimu wa tano wanatarajia washiriki zaidi ya 2,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini watakaochuana katika kilomita 2.5 kwa watoto na watu wasiojiweza, tano, 10 na 21 kwa wakimbiaji wazoefu, huku wakizitumia kukusanya fedha za kusaidia watoto njiti 10,000 katika mkoa huo.

‎”Mwaka jana tulisaida matibabu ya watoto wenye saratani. Mwaka huu tunalenga kuokoa maisha ya watoto njiti ambapo kupitia kampeni yetu tuweze kufikia watoto walau 10,000 katika hospitali zetu za Mkoa wa Mwanza,” amesema Chake.

“Niwaombe wakimbiaji na wana mazoezi wote watuunge mkono kwenye mbio hizi. Tunaomba sapoti kutoka kwa jamii, mashirika na Serikali tufikie lengo la kusaidia hawa watoto.”

‎Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa amesema Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kuhakikisha mbio hizo zinafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kusaidia matibabu ya watoto njiti.

“Tunahamasisha kila mmoja ashiriki mbio hizi ili zifanikiwe na kutimiza lengo lililokusudiwa kwani uwepo wake unaleta manufaa kwenye mkoa wetu. Serikali tuko tayari kutoa ushirikiano ili kuzifanya kuwa kubwa nchini na duniani,” amesema.