Musoma. Jeshi la Polisi mkoani Mara limepokea magari mapya 16 kwa ajili ya kuboresha utendaji wao wa kazi huku Kamanda wa Polisi mkoani humo, Pius Lutumo akitoa onyo kwa madereva wa magari hayo kuepuka uendeshaji usiofuta sheria za usalama barabarani ikiwemo mwendokasi.
Akikabidhi magari hayo kwa watendaji wa jeshi hilo ngazi ya mkoa na wilaya, Kamanda Lutumo amesema madereva wote wakiwamo wa Jeshi la Polisi wanapaswa kufuata na kuzingatia sheria za usalama barabarani, ili kuepuka ama kupunguza ajali zinazotokana na uzembe wa madereva.
“Hatutamuonea huruma dereva yeyote atakayevunja sheria za usalama barabarani, ziko palepale haijalishi wewe ni dereva wa wapi ukienda kinyume utachukuliwa hatua kama wengine wanavyochukuliwa,” amesema na kuongeza;
“Zingatieni hilo na pale inapolazimu kuendesha mwendo kasi, basi fanyeni hivyo kwa kuzingatia miongozo sio kuendesha mwendokasi kila mahali na kila saa.”
Kuhusu umuhimu wa magari hayo kwa jeshi hilo, Kamanda Lutumo amesema ni moja ya vitendea kazi ambavyo jeshi hilo lilikuwa linahitaji ili kuboresha utendaji na ufanisi katika majukumu yao ya kila siku.
Amefafanua kuwa kati ya magari hayo moja ni la Kamanda wa Mkoa huku mengine yakiwa ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa (FFU).
Mengine wamepewa wakuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa wilaya nne zinazounda mkoa wa kipolisi wa Mara, huku mengine yakielekezwa kwenye kufanya doria na operesheni mbalimbali kwa ajili ya kupambana na kutokomeza uhalifu mkoani humo.
“Niwahakikishie wananchi wa Mara kuwa ufanisi wetu utaongezeka zaidi, kwani sasa tuna uwezo wa kuwahi kwenye tukio tofauti na zamani ambapo tulikuwa tunachelewa kutokana na uhaba wa magari, ” amesema.
“Tunatarajia kuona huduma za Polisi kwa jamii zikiimarika zaidi ya ilivyokuwa mwanzo, Polisi walikuwa wanachelewa sana kufika kwenye matukio na hii ilikuwa inatokana na hali halisi ya magari yao, sasa wana magari mapya hakuna kisingizio watimize wajibu wao ipasavyo,” amesema Emmanuel Majura, mkazi wa mkoani Mara.
Amesema ufanisi wao utachangia zaidi kuimarika kwa amani na utulivu sambamba na usalama wa raia na mali zao kwa muda wote.
“Mimi nilikuwa naona kero, unafika kituo cha Polisi kutoa taarifa za mhalifu ama una mashtaka dhidi ya mtu lakini askari walikuwa wanashindwa kwenda kumkamata wanasema hakuna gari, naipongeza Serikali kwa hatua hii sasa ule wimbo wa hatuna gari Polisi umefika mwisho wake,” amesema Makore Jumanne.
Wakati huohuo, Kamanda huyo ametoa wito kwa wakazi ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria kuendelea kuzisalimisha kabla ya Oktoba 31, 2025.
Agosti 27,2025 Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime lilitoa wito kwa Watanzania wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha hizo polisi ndani ya miezi miwili na hawatachukuliwa hatua zozote.
Kamanda Lutumo amesema licha ya muda wa kusalimisha silaha hizo kuanza tangu Septemba Mosi hadi sasa, hakuna mtu aliyesalimisha ambapo amesema watu wanaomiliki wanapaswa kutumia muda uliotolewa kuziwasilisha.
“Hakuna hatua za kisheria zitakazochukuliwa kwa watakaofanya hivyo na wala hapatakuwa na masharti yoyote, nitoe wito kwa wote wenye silaha hizo kuzisalimisha kabla muda haujaisha,” amesema.