Kasulu. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwavutia zaidi wawekezaji kwenda kuwekeza Kigoma ili kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Samia amebainisha hayo leo Septemba 13, 2025 wakati wa mkutano wake wa kampeni katika Jimbo la Kasulu mkoani Kigoma ambao umehudhuriwa na maelfu ya makada wa CCM na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza wakati akiomba kura, Samia amesema mkoa huo una fursa nyingi zinazoweza kuufanya kuwa wa kimkakati katika uzalishaji na biashara katika ukanda huo.

Amesisitiza kwamba akipatiwa ridhaa, atakwenda kuendeleza miundombinu itakayowezesha mkoa huo kufanya biashara kikamilifu.
“SGR ni mradi wa kitaifa na bahati nzuri Kigoma mmebahatika, mtakuwa na vituo vingi zaidi kuliko mikoa mingine, lakini kwa sababu reli hii inamalizika Kigoma, fursa kubwa sana za kibiashara zitakuwa hapa Kigoma.
“Lengo ni kuufungua Mkoa wa Kigoma kwenye ukanda huu wa Ziwa Tanganyika ili uwe ndiyo kitovu cha biashara. Kwa hiyo ndugu zangu wa Kigoma changamkieni fursa hizo, kufanya biashara na nchi jirani, na hata ndani ya Tanzania,” amesema Samia.

Amesema wamepeleka umeme ili kufungua fursa za uwekezaji na sasa Kigoma imeanza kupata uwekezaji kwenye viwanda vikubwa kwani sasa kuna kiwanda cha saruji na kiwanda cha sukari.
“Tunakwenda kuifanya Kigoma mkoa wa kimkakati kwenye uzalishaji wa sukari, pia, saruji ndani ya nchi hii. Tunakwenda kuandaa mazingira zaidi ili wawekezaji wengi waje Kigoma,” amesema mgombea huyo.
Samia ameongeza kuwa: “Kwa sababu kuna reli inaishia Kigoma na Kigoma mna reli zote mbili; ile ya zamani na hii mpya, wawekezaji watakuja kwa wingi kwa sababu usafirishaji kwenda nchi za jirani utakuwa umerahisishwa, anayejenga kiwanda chake leo, atakutana sisi kwenye SGR tumekwenda mbali zaidi, hivyo atafanya kazi zake vizuri.”

Ameongeza kuwa kiwanda cha sukari kilichopo Kasulu kimeajiri watu 500 na kwamba wana matumaini kitaajiri vijana wengi zaidi siku zijazo baada ya kukua na kuongeza uzalishaji.
Kwa upande wa umeme, Samia amekiri kwamba mkoa huo unakabiliwa na changamoto kubwa inayosababishwa na kuwa mbali na vyanzo vya kuzalisha umeme, hivyo wanakwenda kuzalisha umeme wa megawati 49.5 kwenye Mto Malagalasi kwa ajili ya baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kigoma.
Amesema kabla mkoa huo haujaunganishwa kwenye gridi ya Taifa, walikuwa wakitumia Sh58 bilioni kwa ajili ya kununulia mafuta na vipuli, lakini sasa fedha hizo zinatumika kusambaza umeme kwenye vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo.
Wagombea ubunge watoa neno
Mgombea ubunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako amesema katika sekta ya elimu, wamepatiwa Sh15 bilioni ambapo wamejenga shule za msingi 16 na za sekondari tisa.

Mgombea ubunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako
Amesema wakati anaingia madarakani, Kasulu walikuwa na shule moja ya kidato cha tano na cha sita, lakini sasa wameongezewa shule nyingine moja iliyojengwa kwa gharama ya Sh1 bilioni.
“Kwenye sekta ya afya, tulikuwa na kituo cha afya kimoja, lakini sasa tuna vituo vitatu. Na siyo vituo kwa maana ya majengo tu, bali vina vifaa tiba na dawa, wagonjwa wanapata huduma kikamilifu,” amesema mgombea huyo.
Kwa upande wa umeme, amesema wanashukuru Kasulu sasa imeunganishwa katika gridi ya Taifa, jambo ambalo lilikuwa halijafanyika tangu uhuru. Hata hivyo, amesema bado baadhi ya vitongoji havijafikiwa na huduma hiyo, hivyo ameomba miradi iliyopo iwafikie wananchi.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Kasulu Vijijini, Edibily Kimnyoma amesema kila mwaka wanatengewa Sh2 bilioni kwa ajili ya miradi ya barabara katika jimbo lake.

Amesema katika jimbo lake kuna mgogoro kati ya wananchi na Mamlaka ya Hifadhi ya Misitu (TFS), hata hivyo amempongeza kwa jitihada anazozifanya kumaliza mgogoro huo ikiwamo kugawa ardhi kwa wananchi ekari 1,445.
“Maeneo mengine bado kuna changamoto, beacon zinazotumika ni za tangu wakati wa vijiji vya ujamaa. Naomba ukirudi ofisini, utusaidie kutatua mgogoro huu,” amesema mgombea huyo.
Amemuahidi mgombea urais kwamba wanakwenda kumpigia kura siku ya uchaguzi ili ashinde kwa kishindo pamoja na wagombea wengine wote wa CCM.
Mgombea ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Kigoma, Zainabu Katimba amesema Sh11.4 trilioni zilizopelekwa katika mkoa huo, zimeleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.

Mgombea ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Kigoma, Zainabu Katimba
Amesema moja ya mapinduzi makubwa yaliyofanyika ni mkoa huo kuunganishwa katika gridi ya Taifa, jambo ambalo limechochea kuanzishwa kwa viwanda na sasa wawekezaji wanaendelea kwenda Kigoma kuanzisha viwanda kwa kuwa kuna uhakika wa umeme.
“Ile dhamira yako ya kuifanya Kigoma kuwa kitovu katika ukanda wa maziwa makuu, sasa tunaiona, unatujengea meli kubwa ambayo itarahisisha shughuli za uchukuzi katika ukanda huu, tunakushukuru sana mgombea wetu,” amesema Katimba.
Pinda ataka kura mashinani
Waziri Mkuu mstaafu, ambaye pia ni mratibu wa kampeni katika kanda ya Magharibi, Mizengo Pinda amewaomba wanachama wa chama hicho kutoka kwenda kupiga kura ili kumpatia ushindi mgombea wao.

“Kazi ya kuhamasisha hili nawapa mabalozi wa nyumba 10. Nendeni mkahamasishe wanachama wenu wakapige kura, tuna watu wengi huko, mkienda kupiga kura tutapata ushindi wa kishindo,” amesema Pinda.
Pinda amesema wakati wa utumishi wake alikuwa anakwenda sana Kasulu akiwa Waziri Mkuu na alipokuwa Tamisemi, amekiri kwamba Kasulu imebadilika ukilinganisha na wakati ule.
Amesisitiza umuhimu wa kutunza amani hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwapuuza watu wanaotaka kuitetelesha. Amewataka wote kutunza amani kwa mustakabali mwema wa Taifa hili.