Singida BS yaifuata Al Hilal fainali CECAFA Kagame Cup

MIAMBA ya soka la Sudan, Al Hilal Omdurman ilikuwa timu ya kwanza kutinga fainali za Kombe la Cecafa Kagame baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya APR kwenye Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam.

Al Hilal itacheza fainali dhidi ya Singida BS iliyoifunga KMC mabao 2-0 yaliyofungwa na Clatous Chama na Andy Kofi kwenye uwanja huohuo baada ya nusu fainali ya kwanza kumalizika na kushuhudiwa ndoto ya APR kutwaa ubingwa wa nne ikisitishwa ndani ya dakika 120.

Katika mechi awali ambayo ilichezwa kwa dakika 120 baada ya 90 kushindwa kutoa mbabe (1-1), APR ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa William Togui.

Bao hilo lilifungwa dakika ya 32 na kuwafanya mabingwa hao mara mbili wa Kagame kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele.

Tofauti na walivyocheza katika kipindi cha kwanza, Al Hilal ilionekana kuwa bora zaidi kipindi cha pili huku ikitengeneza mashambulizi mfululizo kupitia pembeni na kupata bao la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili, lililofungwa na kiungo Abdelrazig Omer.

Hadi dakika 90 za mechi hiyo zinamalizika mzani ulikuwa sawa hivyo ilibidi timu hizo kuongezwa dakika 30 ambazo Al Hilal ilizitumia vyema kulipa kisasi cha msimu uliopita wa Kagame.

Ikumbukwe kuwa msimu uliopita, APR iliing’oa Al Hilal katika hatua ya nusu fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya kutoka suluhu.

Al Hilal ilijipatia bao lake la pili kupitia Abdel Raouf dakika ya 91 huku ikijihakikishia ushindi katika dakika ya 106 kupitia kwa Ahmed Salem na kuwa timu ya kwanza msimu huu kutinga fainali ya michuano hiyo mikongwe ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kuondolewa kwa APR katika hatua ya nusu fainali ina maana kuwa fainali ya msimu huu, itachezwa na timu ambazo hazina historia ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo. APR ndio ilikuwa timu pekee iliyoshiriki msimu huu yenye historia ya kutwaa mataji mengi zaidi (3).

Rekodi ya jumla kwa timu iliyotwaa mataji mengi zaidi katika mashindano hayo inashikiliwa na Simba (6) ambayo haikushiriki machuano ya msimu huu.