TANZANIA NA ALGERIA KUSHIRIKIANA KATIKA UPATIKANAJI WA DAWA SALAMA,BORA NA FANISI

::::::

Tanzania na Algeria zimekubaliana kushirikiana katika kuboresha uhusiano kwenye upatikanaji na uzalishaji wa dawa zenye usalama, ubora na ufanisi katika nchi hizo. Hayo yamebainishwa na Waziri wa Dawa nchini Algeria alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Wizara ya Afya Tanzania uluoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkr. Adam Fimbo pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai wakati wa ziara ya kiudhibiti iliyofanyika sambamba na maonesho ya biashara ya kimataifa (IATF,2025).

Katika ziara hiyo iliyolenga kuimarisha mahusiano na kubadilishana uzoefu na kuhamasisha uwekezaji katika eneo la dawa ilihusisha maafisa weilngine kutoka Wizara ya Afya na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Jumla ya viwanda vikubwa saba (7) vilitembelewa ikiwemo kiwanda cha Saidal kinachomilikiwa na Serikali ya Algeria, kiwanda cha Sophal, Orion Laboratories, Biopham, Biocare na Frater Raizers. Viwanda hivi vimeonesha nia ya kuwekeza Tanzania kwa kuanza na uuzaji wa bidhaa ambazo ni haba na zenye uhitaji mkubwa ikiwemo dawa za matibabu ya saratani.

 Aidha viwanda hivi vimeahidi kuanzisha viwanda vya dawa nchini Tanzania hatua itakoyasaidia kupunguza gharama za upatikanaji wa dawa na utegemezi katika kuagiza dawa nje ya nchi.