TRA Kagera, yawashika mkono watoto wenye mahitaji maalumu

Bukoba. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Mkoa wa Kagera wamekabidhi msaada wa vitu vyenye thamani ya Sh5 milioni katika kituo cha kulelelea watoto wenye mahitaji maalumu cha Nusulu Yatima, Kashai Bukoba.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Septemba 13, 2025 Meneja wa TRA Mkoa Kagera, Castro John amesema lengo la msaada huo ni kurudisha kwa jamii sehemu ya kodi zinazotolewa na wananchi kama kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu.

“Tumekuja kurudisha kwenye jamii na kushirikiana na wanaotoa huduma hapa ya kuwalea watoto hawa kama mnavyojua sisi TRA ni sehemu ya jamii ndiyo maana tumeleta vitanda, vyakula na magodoro watoto wapate kula na kulala vizuri,” amesema.

John, ameongeza kuwa watoto wenye changamoto za malezi mbalimbali jamii ikiwakumbuka na kuwalea vizuri baadaye wanakuja kuwa viongozi wakubwa, hivyo wameamua kuunga mkono kituo hicho kwa ajili ya kuendelea kutoa malezi bora.

Kituo cha Nusulu Yatima Kashai kinapatikana katika kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, kinahudumia na kulea watoto 78 wenye mahitaji maalumu.


Ambapo watoto 10 wapo masomoni katika ngazi mbalimbali ikiwamo sekondari na vyuo, huku   68 wanaishi kituoni hapo wakitegemea misaada kutoa kwa wadau mbalimbali.

Aidha, Mwenyekiti wa bodi na mlezi wa kituo hicho, Fatma Mohamed amesema changamoto kubwa inayoikumba jamii na kusababisha ongezeko la watoto wenye mahitaji maalumu mitaani ni migogoro inayosababisha kuvunjika kwa ndoa, kutelekeza familia, vifo vya wazazi na walezi.

Fatma, ameishukuru TRA mkoani humo kwa kuwapatia msaada  wa vyakula, vitanda, taulo za kike, sabuni na magodoro vitu vitakavyowasaidia   kuwatunza watoto hao huku akiendelea kuomba na wadau wengine wazidi kujitokeza.

Ameongeza kuwa watoto wanaowahudumia wanawapata kwa njia mbalimbali kama jamii yenyewe kuwapeleka baada ya kutelekezwa na wazazi, kutoka ofisi za ustawi wa jamii pamoja na dawati la jinsia la Jeshi la Polisi.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Rumuli Bukoba, Yasinta Francis anayelelewa katika kituo hicho, amesema anasoma kwa bidii huku akikumbuka kuna wenzake wanahitaji msaada, ameomba jamii kutokata tamaa ya kuendelea kuwasaidia.

Naye, mwanafunzi mwingine wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan iliyopo Kata Kahororo Manispaa ya Bukoba ambaye pia analelewa na kituo hicho, Idrisa Mulangira amesema kituo hicho kinakumbwa na ufinyu wa sehemu za kulala wanabanana sana, hivyo ameomba wadau wajitokeze wawanunulie kiwanja na kuwajengea nyumba.