Dar es Salaam. Zaidi ya miaka minne tangu kifo chake, jina la Maalim Seif Sharif Hamad bado linaendelea kutikisa mijadala ya kisiasa nchini, safari hii likiibuka kila mara kwenye kampeni zinazoendelea.
Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa akipatiwa matibabu.
Kifo chake kilikuwa simanzi kubwa kwa wapenda demokrasia, hasa katika siasa za Zanzibar ambako ndiko ilikuwa ngome yake ya muda mrefu.
Mwanasiasa huyo mkongwe wa Zanzibar, aliyejulikana kwa uthubutu na ujasiri wa kusimama na wananchi na wafuasi wake, sasa amekuwa rejea muhimu kwa baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Maalim Seif aliyeingia kwenye siasa akiwa mwanachama chama tawala, baadaye akashiriki kuasisi Chama cha Wananchi (CUF), kabla ya kutimkia ACT-Wazalendo baada ya mivutano, falsafa yake kuu ilikuwa demokrasia ya kweli, mshikamano wa kitaifa, mamlaka kamili ya Zanzibar na uadilifu wa viongozi.
Aliamini katika siasa safi, akihubiri uwajibikaji wa viongozi na haki kwa wananchi wote bila kujali rangi, dini au nafasi ya kijamii.
Ndoto kuu ya Maalim Seif ilikuwa Zanzibar yenye umoja na heshima ndani ya Muungano na Tanzania yenye vyama vingi vinavyoshindana kwa sera, si kwa vitisho.
Katika maisha yake ya kisiasa, mara kadhaa alikumbana na changamoto, ikiwamo kukamatwa, kufungwa na madai ya kunyimwa ushindi alioamini alikuwa anaupata kwenye chaguzi mbalimbali alizoshiriki.
Hata hivyo, Maalim Seif hakukata tamaa, jambo lililomfanya aaminike kama alama ya mwanasiasa imara, mvumilivu na mwenye ndoto ya kuona mshikamano na haki vinatawala katika Taifa.
Mwangwi wa sifa na msimamo wa Maalim Seif umekuwa ukisikika kwenye kampeni za uchaguzi mkuu, wagombea kadhaa wamekuwa wakijinasibu kutaka kutekeleza matamanio yake endapo watapata ridhaa ya kuliongoza Taifa hili.
Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amekuwa akimtaja Maalim Seif kama kielelezo cha mapambano ya haki Zanzibar.
Kwake, kuzungumzia Maalim Seif ni kuwakumbusha wananchi kuwa mabadiliko si ndoto mpya, bali ni urithi ulioachwa na shujaa huyo wa siasa za upinzani Zanzibar, ambaye anastahili kuenziwa kwa kuendeleza mapambano ya kisiasa na utawala bora nchini.
“Maalim Seif ni kiongozi aliyesimama imara bila kukata tamaa katika kudai mageuzi ya kisiasa licha ya mazingira aliyokumbana nayo enzi za uhai wake,” alisema Salum Mwalimu katika mkutano na wananchi mjini Karatu, Agosti 21, 2025.
ACT-Wazalendo, nacho kimejenga kampeni zake katika misingi ya urithi huo wa kiongozi wake na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Ndani ya mikutano yao, jina la Maalim Seif hutajwa kama kiongozi wa falsafa ya uwajibikaji na mikakati ya chama inayoelezwa kufuata dira yake ya siasa safi. Kwa ACT-Wazalendo, kumbukumbu ya Maalim Seif ni nyenzo ya kudumisha mshikamano na kuonyesha kuwa upinzani unaweza kuwa na nidhamu na maadili.
Kwa upande mwingine, Licha ya CUF kumpoteza Maalim Seif kutokana na mpasuko, kwake jina lake halikufutika. Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF, amewahi kusema wazi kuwa: “Roho ya Maalim Seif inaililia CUF hii.”
Kauli hiyo imeibua hisia kwamba hata ndani ya chama hicho, historia ya Maalim Seif bado ni kioo kionyeshacho pengo lililopo.
Katika jimbo la Mbagala, ambako CUF imesimamisha mgombea ubunge, kumbukumbu ya Maalim Seif imetumika kama chachu ya kuwavuta wapigakura hasa katika mikutano ya kampeni za chama hicho ndani ya jimbo hilo.
Katika mikutano yake, Mgombea ubunge Mbagala kwa tiketi ya CUF, Said Kinyogoli, alama ya Maalim Seif inaonekana dhahiri kupitia nembo za chama hicho.
Kofia zenye rangi za chama hicho zilizopambwa kwa picha za Maalim Seif zinatumiwa na wafuasi wa chama hicho, hali inayoashiria hisia za kiongozi huyo kuonyensha kumuenzi Maalim Seif katika siasa zake jimboni humo.
Mbali na CUF, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina anaonyesha dhahiri kuenzi siasa za Maalim Seif katika mbio zake za kisiasa.
Akizungumza Zanzibar alipowasili kujimbulisha baada ya kuteuliwa na chama chake kuwania nafasi hiyo Agosti 9, 2025, alisema yeye na wagombea wenzake wa chama hicho ni zao la Maalim Seif, akiahidi kuendeleza mapambano aliyoyaanzisha.
“Sisi mnaotuona hapa na kina Othman Masoud (mgombea urais wa ACT-Wazalendo Zanzibar) ndizo damu za kina Maalim Seif na nitakwenda Pemba kuomba baraka kwenye kaburi lake, hatutakuwa wanyonge kwenye kupigania masilahi ya Taifa letu,” alisema.
Tukio hilo linaonyesha namna mwanasiasa huyo anavyotumia turufu ya Maalim Seif katika safari yake ya kisiasa, hasa kwa Wazanzibari ambao walimwamini zaidi kiongozi huyo nguli wa siasa za upinzani visiwani humo.
Kwa wananchi na hasa vijana, jina la Maalim Seif linabaki kama ishara ya uthubutu. Alisimama imara kudai haki hata pale njia zilionekana kuwa ngumu, akiamini siasa za heshima na ukweli ndizo msingi wa maendeleo.
Ni wazi kuwa, katika uchaguzi huu, kumbukumbu ya Maalim Seif imekuwa turufu ya kisiasa. Wanasiasa wanamrejea si kwa ukumbusho pekee, bali kama mwanga wa hoja za sasa.
Hii inaonyesha kuwa urithi wa Maalim Seif si hadithi ya jana, bali ni dira inayoendelea kushawishi mustakabali wa siasa za Tanzania.
Mchambuzi mkongwe wa siasa na utawala bora nchini, Dk Conrad Masabo anasema Maalim Seif ni utambulisho wa mabadiliko na misimamo isiyotiliwa shaka mbele ya jamii, akidai hiyo ndiyo sababu wanasiasa wengi wanaonyesha kujinasibisha na jina lake.
“Kwenye jamii huwa kuna watu wanakuwa utambulisho wa mambo fulani, kwa siasa za Zanzibar, Maalim Seif alijijengea taswira kama mtu mwenye msimamo thabiti katika kupigania mageuzi, alipitia misukosuko hadi kufungwa bado hakutetereka.
“Bara na visiwani hakuna asiyeamini misimamo ya Maalim Seif, watu wanapambana kutumia jina hili kutafuta kujifananisha naye kupata uhalali wa kukubalika,” amesema.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anasema heshima aliyoitengeneza na kujenga imani ya wananchi ndiyo imebaki kuwa kivutio kwa wanasiasa wanaotaka kueleweka kwa jamii ambayo ilimwamini yeye.
“Ni kama kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mtu akigusia suala la mapambano dhidi ya rushwa utaiona taswira ya Mwalimu Julius Nyerere, ndivyo hivyo kwa Maalim Seif kwa wapinzani wanaotaka siasa za mageuzi hawawezi kuliweka kando jina hilo,” amesema.
Kwa upande mwingine, mchambuzi wa siasa na utawala bora Zanzibar, Profesa Mohamed Makame anasema Maalim Seif anakosekana kwa mara ya kwanza katika uchaguzi tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza nchini, hali inayofanya pengo lake kuonekana.
Profesa Makame anaona hii inafanya wanasiasa wajihusishe naye ili kutafuta kujaza pengo lake wapate uungwaji mkono na waliokuwa wafuasi wake.
“Kwa mara ya kwanza tangu Tanzania iingie kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Maalim Seif ndiyo amekosekana katika kinyang’anyiro cha kuwania urais. Tangu Mwaka 1995 amekuwa mshindani mkuu wa nafasi hiyo na kujijengea umaarufu mkubwa,” amesema.
Profesa Makame amesema umaarufu huo umejenga historia ambayo wanaomfuata hutaka nao wavae viatu vyake kwa kutafuta kuungwa mkono, kwa kuwa Maalim Seif aliweza kuwa na ushawishi mkubwa.
“Kwa upande wa pili mafanikio na kushindwa kwake ni mfano kwa pande zote mbili, upinzani na chama tawala. Upinzani unaona aliweza kujenga upinzani na kufanikiwa na watawala wanaona mbali na hayo, alishindwa kupata nafasi ya kuwa Rais, hivyo kila upande utazungumza kwa kigezo chake,” anasema Profesa Makame, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza).