Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 386 na gramu 80.
Pia, jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa mwingine kwa madai ya kutengeneza na kusambaza pombe kali feki kwa kutumia majina ya kampuni mbalimbali za kutengeneza pombe kali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, ameiambia Mwananchi Septemba 12, 2025, kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 4, 2025, katika Kijiji cha Ipande, Kata ya Nkokwa, Tarafa ya Ntebele, Wilaya ya Kyela.
Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, waliokamatwa ni Editha Samweli, maarufu kama Mwasekaga (36), Furaha Seme (22), Sunday Mwaipopo (23), Ezekiel Mwatonola (20) na Jackson Chipeta (18), ambao ni wakazi wa vijiji mbalimbali vilivyopo katika Kata za Mbugani, Kasumuru, Ibanda na Lubele, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya.
“Watuhumiwa hawa walikamatwa Septemba 4 mwaka huu wakiwa na dawa za kulevya aina bangi zenye uzito wa kilogramu 387 na gramu 80 wakiwa wamehifadhi kwenye mifuko laini 185 na kisha kuficha kwenye sandarusi kubwa tano na kusafirisha kwa kutumia pilipiki tatu tofauti, zote aina ya Boxer,” amesema.
Kuzaga amesema Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya aina ya bangi sambamba na masoko yake.
Amesema watuhumiwa watafikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio la pili, Stella Hance (50), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutengeneza pombe kali za bandia za aina mbalimbali.
Kuzaga amesema mtuhumiwa baada ya kufanyiwa upekuzi ndani ya nyumba yake alikutwa na katoni 142 za pombe bandia aina mbalimbali, chupa tupu, mifuko mitatu, madumu sita na kopo lenye gundi ya kubandikia nembo.
Ametaja vingine vilivyokamatwa ni stika 941 aina tofauti na madumu mawili ya lita ishirini, yenye kimimimika cha pombe kali bandia iliyokuwa imezalishwa tayari kwa kuingizwa sokoni.
Kuzaga amefafanua kuwa mtuhumiwa alikamatwa Septemba 7, mwaka huu katika Mtaa wa Isyesye jiji la Mbeya kwenye msako endelevu unaofanywa na polisi wa kuzuia na kupambana na matukio ya uhalifu.
“Nitoe onyo kwa wananchi wanaojihusisha na biashara haramu na utengenezaji wa pombe bandia, polisi hatujalala na tutawasaka na kuwabaini mahala popote walipo,” amesema.
Mfanyabiashara wa vileo, Stella Moses amesema kwa sasa kumeibuka wimbi kubwa la kutengeneza pombe kali bandia zenye nembo za makampuni kutoka nje ya nchi, jambo ambalo limeharibu soko ya pombe halisi.
“Mara kadhaa tunakutana na kasheshe ya pombe bandia, lakini tukibaini tunawafuatilia wasambazaji kwa sababu tunawajua,” amesema.
Amesema wanaomba Polisi kupitia watuhumiwa waliokamatwa wawe chachu ya kutoa taarifa ya mtandao wao ili kudhibiti bidhaa bandia ambazo zinachangia kupunguza nguvu kazi kwa vijana.
Mmoja wa watumiaji wa pombe kali aina ya Master Wine John amesema wanabaini zilizo bandia kutokana na radha yake kuzidi ukali na kuleta madhara ya kubabua ngozi baada ya siku kadhaa.