Wauguzi, wakunga wakumbushwa kuzingatia maadili ya kazi zao

Tanga. Katibu Mkuu wa Chama Cha Wauguzi Tanzania, (Tanna), Geofrey Chacha amewataka wauguzi kuhakikisha wanazingatia kanuni na sheria za kazi zao, ili kuweza kuepukana na kashfa na tuhuma dhidi yao ambazo zinaweza kuwachafua kwenye taaluma.

Akizungumza kwenye mkutano wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Tanga uliofanyika wilayani Muheza Jumamosi Septemba 13, 2025 kujadili mipango ya maendeleo ya chama hicho, Katibu huyo amesema wanapokea malalamiko kuhusu wakunga na wauguzi kufanya makosa mbalimbali, ambayo mengine wanaweza kuyaepuka wakizingatia maadili.

Amesema ni vizuri kila mmoja katika eneo ambalo yupo azingatie taratibu za kazi ambazo zitaweza kumlinda hata kama ikitokea changamoto, ila wengine wanafanya makosa ambayo hata chama kinashindwa kujua kitawasaidia vipi kutokana na baadhi ya makosa kukiuka kanuni.

Chacha amesema wapo baadhi ya wakunga na wauguzi wanakutwa na tuhuma mbalimbali wakiwa kazini, lakini kama wangefanya kazi kwa kufuata taratibu za kazi ni rahisi   kuwasaidia kupata haki zao, ikiwa  kinyume na hapo ni changamoto kwao.

“Tumekuwa tukipokea kesi tofautitofauti za kutetea wauguzi na wakunga katika maeneo yao ya kazi, aidha katika kufanya kwao kazi wanakutwa na tuhuma mbalimbali sasa naomba niseme kidogo, unapovunja sheria na kanuni za kitaaluma unatupa wakati mgumu  kukutetea, zingatieni miongozo,” amesema Chacha.

Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Peter Chambo amesema wanaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara ya kuwakumbusha wauguzi na wakunga kuzingatia miongozo ya kazi, ambayo hutolewa kila baada ya miezi mitatu.

Amesema mkoa huo una wauguzi   1,200 idadi ambayo amesema bado haitoshelezi, licha ya juhudi za Serikali kuajiri wauguzi. Hivyo ameiomba Serikali kila inapopata nafasi ya kuajiri kuikumbuka kada hiyo ambayo bado haina watumishi wengi, ila ndio inategemewa zaidi kwenye utoaji huduma.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dk Fani Mussa, ambae alifungua kikao hicho amesema Serikali inaendelea kuboresha stahiki za wauguzi ili zilingane na kada nyingine.

Ametaja stahiki hizo ikiwa ni pamoja na fedha za likizo na kujikimu kwa ajira mpya na  sare.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Wauguzi Wilaya ya Muheza, Hilda Mkuyu amesema wamepokea maelekezo ya viongozi wao na wanakwenda kuyafanyia kazi.