Dar es Salaam. Kiongozi mstaafu wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman kwa tiketi ya chama hicho ndiye anayefaa kuongoza kisiwa hicho kutokana na kuwa mstari wa mbele wa kupigania masilahi ya Wazanzibari.
Zitto ameeleza hayo leo Jumamosi Septemba 13, 2025 wakati wa ufunguzi wa kampeni za mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, maarufu OMO, kwa tiketi ya chama hicho uliofanyika katika uwanja wa Tibirinzi Chakechake, Pemba.
“Mimi ni mdogo kwa Othman, sijakutana naye shule wala chuoni au katika kazi za kitalaamu, bali nimemsoma na kumfahamu Othman kwa sababu nilitaka kumfahamu zaidi,” amesema Zitto.
Amesema Othman ni miongoni mwa watu waliomfanya kuijua Zanzibar na masilahi yake kupitia maandiko na machapisho yake.

Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akiwaeleza wafuasi wa ACT Wazalendo kwa nini mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud anapaswa kuchaguliwa.
“Dunia inajua ukiweka masilahi yake binafsi Othman na Zanzibar, ukamwambia achague, anachagua Zanzibar. Wazanzibari wanajua na Watanzania wanajua si jambo la kuhadithia, mmeona hili,” ameeleza Zitto.
Amesema Othman anabebwa na rekodi mbalimbali za utumishi wake usiotiliwa shaka, akitolea mfano mwaka 2014 alivyokwenda kinyume na msimamo wa Serikali wa kutopiga kura ya ‘Ndiyo’ katika Bunge Maalumu la Katiba kuhusu muundo wa Serikali.
Ingawa msimamo huo ulimgharimu Othman ambapo, Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Dk Ali Mohamed Shein, alitangaza kumvua wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutokana na kupiga kura ya Hapana, jambo hilo lilitafsiriwa kwenda kinyume.

Mgombea urais wa Zanzibar ( ACT Wazalendo), Othman Masoud akizungumza na wananchi wa Pemba katika ufunguzi wa kampeni zilizofanyika uwanja wa Tibirinzi wilayani Chakechake.
Amesema changamoto zinazoikabili Zanzibar, ikiwemo ugumu wa maisha na umasikini licha ya kisiwa hicho kubarikiwa rasilimali zenye utajiri, dawa yake ni moja kumpeleka Othman ikulu.
“Dawa ni moja Othman Masoud Othman, akiwa Rais wa Zanzibar haki itatamalaki. Akiwa Rais wa Zanzibar, Zanzibar itachukua haki ya mamlaka kamili inayostahiki, atatengeneza sera zitakazotengeza unafuu wa maisha yenu, akiwa Rais atakayeigeuza Zanzibar kushika nafasi yake ya kuwa na uchumi wa Bahari ya Hindi.
“Othman ndio kiongozi anayehitajika, ni kiongozi tunayemhitaji. Othman ndiye kiongozi tunayetakiwa kumpambania kuhakikisha anashinda. Tunajua sisi tunaeneza sera… sasa natoa salamu haki itendeke ili Wazanzibar wachague kiongozi wanayemtaka,”amesema Zitto huku akishingaliwa.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya ACT – Wazalendo, Mansour Yusuf Himid amesema hatua ya chama hicho kuzindulia kampeni Tibirinzi kimeweka historia pasipo kuwepo kwa mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi wa ACT Wazalendo, Zanzibar, Mansour Yusuf Himid akihutubia mkutano ufunguzi wa kampeni Pemba.
“Mungu amlaze mahali pema peponi, leo hatunaye tena, lakini tunaye Othman Masoud. Mzee wetu Maalim yupo radhi huko aliko, lakini na sisi tuliobaki tupo radhi na Othman. Yalinigusa niliposikia tunazindua kampeni Tibirinzi, kwa sababu hata mimi nilitolewa na Maalim Seif hapa hapa,”
“Alinishika mkono na kunikabidhi kwenu hapa, zaidi ya muongo mmoja sasa. Mlinipokea na mimi sikukengeuka, kwa uwezo wa Mungu tutakwenda wote katika safari hadi mwisho, tayari ninaiona bandari salama,” amesema Mansour.

Amesema ACT -Wazalendo, inatafuta uongozi wa Zanzibar si kushindanisha wakandarasi na matuta, bali Zanzibar inahitaji kiongozi mwadilifu, atakayekivusha kisiwa hicho.
“Katika hili, Othman ndiye chaguo sahihi na amejipambanua mapema, na Serikali atakayoiunda itawajibika kwa wananchi wake na si vinginevyo,” amesema Mansour.